Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

Umuhimu wa uhifadhi wanyamapori hususan tembo umesababisha kuchelewa kuanza kwa majaribio ya safari za treni ya SGR, maarufu kama treni ya mwendokasi nchini; imeelezwa.

Safari za majaribio zilitarajiwa kuanza mwezi huu kati ya Dar es Salaam na Morogoro, kipande ambacho ujenzi wake umekamilka kwa asilimia 97.91.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, amesema TRC ilikuwa tayari kuanza safari za majaribio.

“TRC tunafahamu umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori ndiyo maana tuliposhauriwa kujenga uzio maalumu wa kuzuia tembo wasiingie maeneo ya SGR, tulikubali,” anasema.

Kazi ya ujenzi wa uzio huo unaofahamika kama ‘elephant fence’ ni ya kitaalamu na Kadogosa anasema Afrika Kusini wanaifahamu zaidi kazi hiyo.

Tayari mkandarasi mkuu wa mradi, Yapi Merkezi, kampuni kutoka nchini Uturuki, ameanza kujenga uzio huo.

“Si kazi rahisi kwa kuwa eneo husika, la kwanza, ni la Ngerengere lenye urefu wa kilomita tisa. Uzio unajengwa kila upande. Hivyo kufanya ujenzi kuwa wa kilomita 18.

“Eneo jingine ni kati ya Mkata na Kimamba (kipande cha Morogoro – Makutupora). Hili lina urefu wa takriban kilomita 90. Uzio unajengwa pande mbili hivyo kuufanya ujenzi kuwa wa jumla ya kilomita 180,” anasema Kadogosa.

Uzio wa kuzuia tembo kuingia kwenye mradi wa SGR ambao gharama yake haikupatikana mara moja umekuja baada ya kikosi kazi maalumu kilichoundwa na serikali kikiwashirikisha wadau wa mazingira na uhifadhi kutembelea mradi mwaka jana na kushauri hatua kadhaa zinazostahili kuchukuliwa katika kuimarisha uhifadhi endelevu.

Kadogosa anataja sababu nyingine ya kuchelewa kuanza kwa majaribio ya safari hizo ni ujenzi wa barabara za juu (madaraja/vivuko) katika maeneo ya jijini Dar es Salaam.

“Hii ni treni inayokwenda kwa kasi sana. Watu au wanyama hawatakiwi kupita (relini) wakati huduma inaendelea. Ni hatari. Huwezi kuanza kuipitisha treni wakati kuna maeneo hayajakamilia sawasawa.

“Mfano ni Vingunguti, Uwanja wa Ndege na Staki Shari (Njia panda ya Segerea). Mkandarasi yupo ‘site’ (eneo la mradi) na ujenzi unaendelea kwa kasi kubwa. Tumemuuliza, anasema atamaliza kazi Aprili mwaka huu,” anasema Kadogosa akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kifedha kutekeleza majukumu yao.

Kauli ya mkandarasi na uhalisia wenyewe ni vitu viwili tofauti ndiyo maana Kadogosa hataki kusema kwa uhakika ni lini hasa safari za majaribio zitaanza, akifahamu fika kwamba wakati wowote mwenzi ujao msimu wa masika utaanza na huenda ukapunguza kasi ya ujenzi.

“Lakini kwa vyovyote vile, mwaka huu safari zitaanza,” anasema mtaalamu huyo wa uhasibu ambaye tangu aingie TRC mwaka 2016, ameshirikiana na menejimenti kufanya mageuzi makubwa ndani ya shirika.

Serikali yawekeza matrilioni

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Gabriel Migire, anasema serikali imekuwa ikiwekeza fedha nyingi SGR kwa kuwa ni mradi mkubwa zaidi wa kimkakati.

“Sekta ya uchukuzi ni muhimu katika kuchochea uchumi wa taifa, ndiyo maana kati ya Sh trilioni 41 ya bajeti ya serikali, Sh trilioni 4 zimeelekezwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Hii ni asilimia tisa ya bajeti nzima.

“Serikali imeweka ‘commitment’ ya Sh trilioni 23 katika mikataba ya miradi ya kimkakati ya reli,” anasema.

Migire anaamini kuwa mwenendo mzuri wa utekelezaji wa mradi wa SGR na miradi mingine nchini unatokana na utulivu uliopo Tanzania kwa sasa.

Anasema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika utulivu uliopo akishauri viendelee kufanya hivyo.

“Kuna mwanafalsafa mmoja amewahi kusema kwa Kiingereza kuwa: ‘No publicity, no public support, therefore a nation must decay’. Huwezi kutenganisha habari, mawasiliano, utulivu na maendeleo.

“Maana yake ni kwamba, maendeleo yanachagizwa na mawasiliano/habari. Na wananchi lazima wapate habari sahihi na kwa wakati sahihi,” anasema Migire akinukuu kaulimbiu ya semina ya wahariri wa vyombo vya habari iliyoandaliwa na TRC, akisisitiza kuwapo kwa uratibu makini katika utoaji na upatikanaji wa habari.

Mtaalamu mwingine aliyezungumza ni Mkurugenzi Miundombinu wa TRC, Mhandisi Machibya Masanja, akisema ujenzi wa reli ya SGR umezingatia  usalama na ufanisi kwa taifa.

Anasema mbali na kwamba reli hii haitakuwa rahisi kuhujumiwa, anasema itakuwa na uwezo wa kusafirisha treni yenye urefu wa kilomita mbili ikifungasha makontena 200 ya futi 40.

Kina Dk. Gwajima na treni binafsi

Katika hatua nyingine, Kadogosa anasema tayari muswada wa sheria mpya upo bungeni na utakapopitishwa, watu na taasisi binafsi wataalikwa kutoa huduma kwenye mfumo wa SGR.

“Zitakuwa na huduma za kiushindani na sisi (TRC) tutakuwapo. Mtu atakuwa anachagua treni anayoitaka. Akitaka kupanda treni yetu sawa, au treni ya mtu (kampuni) mwingine. Itakuwa ni ‘open access’,” anasema.

Anasema kwa upande wa mizigo zipo kampuni zenye mabehewa yake na hutembea katika miundombinu inayomilikiwa na TRC, akitoa mfano wa Azam, inayomilikiwa na bilionea Said Salim Bakhresa.

Taarifa hii huenda ikapokewa kwa furaha na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Dk. Josephat Gwajima, aliyewahi kuwaambia waumini wake kuwa ana mpango wa kununua treni ya umeme.

Kauli ya Gwajima aliitoa Februari 2017 kanisani kwake Ubungo, Dar es Salaam na kuzua mjadala mrefu mitandaoni.

“Nimedhamiria kununua treni ya umeme baada ya Rais John Magufuli kuonyesha dhamira ya kujenga reli ya kisasa (SGR),” ananukuliwa akisema Dk. Gwajima Februari 23, 2017, siku chache baada ya utekelezaji wa ujenzi wa reli hiyo kuanza.

Sasa Kadogosa anaweka wazi uwezekano wa Gwajima na wawekezaji wengine kuingia na kutoa huduma kwenye miundombinu hiyo, ambapo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kusafirisha hata treni 10 kwa wakati mmoja zikiwa katika mwelekeo mmoja.

Please follow and like us:
Pin Share