Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Serikali imewataka Wawekezaji na wamiliki wa viwanda nchini kuzingatia Sheria ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira zilizoanishwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi Mazingira(NEMC) wakati wa uanzishaji, uendelezaji wa viwanda nchini.

Agizo hilo limetolewa jana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazohusu sekta ya mazingira aliyoifanya katika viwanda vya Multi Cable Ltd na Nyakato Steel Mills Ltd vilivyopo Wilaya ya Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima akifurahia jambo na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis mara baada ya kumaliza mazungumzo yao ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kabla ya kuanza kwa ziara yake ya kukagua miradi ya sekta ya mazingira mkoani humo Februari 22, 2023. Kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana.

Amesema dhamira ya Serikali ni kuinua uchumi wa viwanda ili kuweza kukuza Pato la Taifa, kukuza wigo wa ajira kwa vijana na kutengeneza uhusiano mzuri baina ya Serikali na wawekezaji, hivyo yapo masuala muhimu ya kimazingira yanayopaswa kupewa kipaumbele na wawekezaji na wamiliki wa viwanda hivyo nchini.

Khamis ameyataja masuala hayo ni pamoja na viwanda kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya shughuli za mazingira katika jamii inayozunguza mradi wa uwekezaji ambapo wamiliki hawana budi kusaidia vifaa muhimu vinavyosaidia usafi wa mazingira katika eneo husika.

Aidha, amesema jambo lingine muhimu ni pamoja kutenga bajeti maalum ya utunzaji na upandaji miti pamoja na Mpango Kabambe wa kubadiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoikabili nchi na dunia kwa ujumla.

“Nimetembelea na kuona uzalishaji katika kiwanda cha Multicable kuna matumizi ya miti ya asili tuliyoipanda. Kwa tafsiri ya haraka hapa tumeharibu mazingira, nawakumbusha wamiliki kuwasiliana na Ofisi yetu ya NEMC ili kuweza kuingia katika teknolojia ya kisasa ya nishati mbadala,” amesema Naibu Waziri Khamis.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Khamis Hamza Khamis akisalimiana na Viongozi na Watendaji wa Kiwanda cha Multi Cable Ltd kinachozalisha vifaa vya umeme na bidhaa za plastiki za majumbani wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Kiwanda hicho kusikiliza na kutatua changamoto za sekta ya mazingira katika Mkoa wa Mwanza.

Naibu waziri huyo pia aliwakumbusha wawekezaji na wamiliki wa viwanda nchini pia kuhakikisha wanadhibiti utilishaji wa majitaka kutoka viwandani kwenda katika makazi ya wananchi sambamba na kuiagiza NEMC Kanda ya Ziwa kufanya kaguzi za mara kwa mara ili kuona utekelezaji wa maagizo hayo aliyotatoa kwa wawekezaji na wamiliki wa viwanda hivyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Hassan Masala aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kutembelea Wilaya hiyo na kusikiliza na kutatua changamoto za sekta ya mazingira katika Wilaya hiyo ambayo imekuwa na idadi kubwa ya viwanda vya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.

Kwa niaba ya Wilaya, nakushukuru Mhe. Naibu Waziri kwa kutenga muda na kutembelea Viwanda vilivyopo Ilemela. Nitoe wito kwa ofisi yako kutenga muda zaidi wa kufanya kaguzi za kimazingira ikiwemo kelele na mitetemeko ya sauti katika maeneo ya burudani na starehe” amesema Masala.

Kwa upande wake Meneja uzalishaji Kiwanda cha Multi Cable Ltd, Hamisi Maleta amesema kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 2004 kinajishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za plastiki za majumbani pamoja na vifaa vya umeme, kimekuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira kwa kupunguza mrundikano mkubwa wa taka katika maeneo ya mjini ambazo ni malighafi muhimu za kiwanda hicho.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Khamis Hamza Khamis akipata maelezo kuhusu mradi wa uzalishaji wa bidhaa za plastiki za majumbani kutoka kwa Meneja uzalishaji wa Kiwanda cha Multi Cable Ltd cha kilichopo Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza, Hamisi Maleta wakati wa ziara yake ya kukagua mradi huo.

Aidha Maleta alisema miongoni mwa changamoto inayokikabili kiwanda hicho kwa sasa ni upatikanaji wa nishati ya uhakika ya umeme kwani umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara na kuleta athari katika uzalishaji wa bidhaa kiwandani hapo.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza, Alfred Yonas amesema ofisi yake imepokea changamoto zote zilizopo katika kiwanda hicho ikiwemo upatikanaji wa maji na kuahidi kukifanyia kazi kwa wakati.

Niwaombe wamiliki wa kiwanda waendelee kuvuta subira kwani mwezi mwezi April tunakwenda kuzindua mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya sh.bilioni 4 na hii itasaidia kumaliza changamoto hii hapa kiwandani,” amesema Yonas.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) akitazama mtambo wa uzalishaji wa bidhaa za plastiki za majumbani zinazozalishwa katika Kiwanda cha Multi Cable Ltd kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto za sekta ya mazingira katika Mkoa wa Mwanza.
Please follow and like us:
Pin Share