Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo na Biashara Tanzania (TanTrade) wamefungua rasmi maonesho ya pili ya Kimataifa ya wazalishaji Tanzania (TIMEXPO 2024).

Maonesho hayo yanatarajiwa kufanyika Septemba 26 hadi 29, mwaka huu katika uwanja wa maonesho wa Mwalimu Julius Nyerere maarufu kama Sabasaba.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 20, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Leodegar Tenga amesema kauli mbiu ya maonesho hayo ni ‘Kutengeneza Daraja kati ya Viwanda vya ndani na nje ya nchi’.

“Kauli mbiu hii inatumika katika maonesho haya kwaajili ya kuunganisha wazalishaji wa Viwanda vya ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujifunza teknolojia mbalimbali ili kuweza kuboresha bidhaa zetu za ndani ili kukidhi vigezo vinavyohitajika katika soko la kimataifa.

“Hivyo nachukua fursa hii kuwaambia kuwa usajili tayari umefunguliwa hivyo Watanzania na watu wa mataifa mengine waendelee kujisajili,” amesema Tenga.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Tantrade, Mkurugenzi Idara ya Ukuzaji Biashara Tantrade, Fortunatus Mhambe amesema lengo kuu la maonesho hayo no kuchochea ukuaji wa Viwanda nchini kwa kukuza Viwanda vya ndani na kuvutia wadau mbalimbali wa kitaifa na kimataifa na hivyo kuendeleza mazingira mazuri ya kubadilishana maarifa, ushirikiano na uvumbuzi.

“Naomba nitoe rai kwa wadau na washirika wote kushiriki katika maonesho haya ya TIMEXPO 2024 ambayo yatashirikisha kampuni/washiriki zaidi ya 500 kutoka ndani na nje ya Tanzania. Hivyo, yatatoa fursa kwa washiriki na wadau kutangaza bidhaa na huduma mbalimbali zinazozalishwa nchini,” amesema na kuongeza kuwa:

“Pia kuwaunganisha wenye viwanda na wazalishaji mbalimbali wa malighafi na huduma zingine zinazotumika viwandani, wazalishaji kujifunza teknolojia mpya, kupata semina na mijadala mbalimbali ya kitaaluma kuhusiana na maendeleo ya uzalishaji Tanzania, kutangaza fursa mbalimbali za masoko ya ndani na nje ya nchi na kutoa fursa kwa Watanzania kutambua wazalishaji na viwanda vilivyopo nchini,”.

Naye Mkurugenzi ya Kampuni ya Kaypee Motors ambayo inatengeneza gari ndogo za umeme, Masudi Kipanya amesema: “Nayafurahia maonesho haya kwasababu yanatuwezesha kutambulika sisi kama wazalishaji wa ndani. Hivyo Watanzania wajitokeze kuonesha bidhaa zao na kuja kutembelea,”.