Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waogeleaji wanne wa timu ya taifa ya kuogelea wanatarajiwa kuondoka Juni 21 mwaka huu kwenda Nairobi, Kenya kushiriki mashindano yatakayofanza Juni 22 na 23, mwaka huu nchini humo. 

Akizungumza na waogeleaji hao wakati akiwakabidhi bendera ya taifa, Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Abel Odena amewataka kupambana kuhakikisha wanarudi nyumbani na medali. 

“Nendeni mkaipeperushe vyema bendera ya taifa. Mrudi na medali za dhahabu kwa kuwa kila kitu kinawezekana,” amesema Odena.

Timu ya taifa ya kuogelea itashiriki mashindano hayo yatakayoshirikisha klabu kadhaa za Kenya kama mgeni mwalikwa.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Alexander Mwaipasi, ameahidi timu hiyo kushindana, si kushiriki.

“Tumejipanga vizuri, tuko tayari kupambana na ushindani utakaokuwapo ingawa wachezaji wetu wamezoea kuogelea kwenye bwawa la mita 25,” amesema Mwaipasi.

Mashindano haya yanafanyika Kasarani Complex kwa kutumia bwawa la mita 50.

Hata hivyo, nahodha Romeo Mihaly amesema hakuna kitakachoharibika, akiahidi kutumia maelekezo waliyopewa na viongozi kupambana kwenye bwawa la mita 50. 

Watatu kati ya waogeleaji wanne watashiriki ‘mbio’ nane huku mmoja akicheza mbio saba. 

Meneja wa timu, Francisca Binamongo, amesema waogeleaji wameandaliwa vyema wakiwa wamepewa mazoezi ya nguvu ili kurudi na ushindi.