Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kibaha

Msimu unaokuja wa mvua za Vuli Oktoba hadi Desemba ni miongoni mwa misimu muhimu ya kilimo katika baadhi ya maeneo hapa nchini, hivyo ni muhimu kwa wananchi na watumiaji kupata taarifa sahihi na kwa wakati ili kuweza kupanga na kutekeleza shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo kilimo kwa tija na ufanisi zaidi.

Hayo yamesemwa na Dkt. Ladislaus Chang’a, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, kwenye Warsha ya mafunzo kwa wanahabari kuhusu Msimu wa Mvua za Vuli 2023.

Dkt. Chang’a ameongeza kuwa msimu unaokuja wa Oktoba hadi Desemba 2023 utachagizwa na uwepo wa El Nino ambayo ni hali ya kuongezeka kwa joto la uso wa bahari kwa eneo la kitropiki la kati ya Bahari ya Pasifiki.

Amesema kuwa hali ambayo husababisha kuongezeka kwa viwango vya mvua na joto kwa baadhi ya maeneo hapa nchini, hivyo kufanya msimu wa mvua kuwa ni miongoni mwa misimu muhimu ya kilimo hapa nchini hususani maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Aidha, Dkt. Chang’a ameeleza awali kuwa Serikali imeendelea kuijengea uwezo TMA na kuifanya iendelee kuimarisha huduma ikiwemo utoaji wa taarifa hizo kuwafikia watumiaji kwa wakati na kufanya maamuzi sahihi kwa wakati muafaka.

Akihitimisha hotuba yake Dkt. Chang’a amewashukuru wanahabari kwa kuitikia mwaliko wa kuhudhuria warsha na aliwakumbusha kuendelea kuwa mabalozi wa TMA kwa jamii kwa kuimarisha usambazaji wa taarifa za utabiri na tahadhari.

TMA imekuwa na utaratibu wa kuandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanahabari hususani wakati wa maandalizi ya utabiri wa mvua za msimu, ambapo wanahabari hao wanapata fursa ya kujadili na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusiana na msimu husika.

Mamlaka inatarajia kutoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Vuli 2023 kupitia vyombo vya habari,Agosti 24, 2023 saa 5:00 asubuhi, Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

By Jamhuri