Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ipo katika hatua ya kukamilisha maandalizi ya Mwongozo wa kuratibu na kusimamia upangaji na upimaji shirikishi katika jiji la Dodoma utakaoweka utaratibu unaopaswa kuzingatiwa katika utekelezaji zoezi hiyo.

Hatua hiyo inafuatia utekelezaji mpango wa Upimaji Shirikishi katika jiji la Dodoma kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa uwazi katika utekelezaji wa makubaliano ya mgawanyo wa asilimia 30 kwa 70.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Ardhi Maliasili na Utalii tarehe 23 Agosti 2023 mkoani Dodoma, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema katika utekelezaji wa makubaliano hayo baadhi ya watendaji wamekuwa wakitekeleza majukumu yao pasipo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo na hivyo kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi.

‘’Ili kukabiliana na changamoto upangaji na upimaji shirikishi katika jiji la Dodoma, Wizara ipo katika hatua za kukamilisha maandalizi ya mwongozo wa kuratibu na kusimamia upangaji na upimaji Shirikishi’’ alisema Dkt Mabula.

Ameeleza kuwa, Wizara yake inaendelea na utekelezaji wa mpango wa upimaji shirikishi ulioanzishwa ili kuongeza kasi ya upangaji na upimaji wa ardhi katika jiji la Dodoma baada ya Serikali kuhamishia shughuli zake jijini Dodoma julai 2016.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, hali hiyo ya Serikali kuhamia Dodoma imesababisha kuongezeka kwa mahitaji makubwa ya ardhi iliyopangwa na kupimwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Akielezea zaidi kuhusiana na Program ya Urasimishaji Makazi yasiyopangwa nchini, Waziri huyo wa Ardhi aliweka bayana kuwa, kupitia program hiyo jumla ya vipande vya ardhi 2, 480,165 vimetambuliwa ambapo kati ya hivyo viwanja 2,474,329 vimepangwa na kurasimishwa, viwanja 1,264,855 vimepimwa na kuidhinishwa na viwanja 1,114,296 upimaji wake haujakamilika.

Aidha, alisema hadi kufikia julai 31, 2023 jumla ya ankara za umilikishaji wa viwanja vya urasimishaji 601, 076 zimetolewa ambapo kati ya hizo jumla ya hatimiliki 203,290 zimeandaliwa.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, Dkt Mabula alisema, program ya urasimishaji makazi inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mwitikio hafifu wa wananchi kuchangia gharama za upimaji na umililkishaji hali inayosababisha miradi kutotekelezwa kwa wakati.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Malisili na Utalii mbali na kuipongeza wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kazi kubwa inayofanya lakini wameitaka kujipanga na kuongeza kasi ya umilikishaji ardhi huku ikihakikisha inasambaza vifaa vya kutosha kwenye ofisi zake.

‘’Kazi inafanyika lakini ukiangalia bado changamoto ni kubwa hivyo mnatakiwa kuongeza kasi na kuhakikisha kunakuwa na usimamizi mzuri kwa mfano mtu anaanza kujenga nyumba na inafikia hatua kubwa halafu anaambiwa amejenga bila kufuata taratibu hii siyo sawa’’ alisema Makamu Mwenyekiti wa Kamati Najma Giga.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imepangiwa kuwasilisha mbele ya kamati taarifa mbalimbali kama vile utendaji wa Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi, utekelezaji program ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi, utekelezaji program ya urasimishaji makazi yasiyo pangwa nchini, utekelezaji wa mpango wa upimaji shirikishi katika jiji la Dodoma pamoja na utatuzi wa changamotio za upimaji ardhi nchini mbalimbali.

By Jamhuri