Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2024 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 22, 2024 jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a amesema kuwa maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a amesema kuwa vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza hivyo kuweza kusababisha mafuriko, milipuko ya magonjwa pamoja na athari nyingine zitokanazo na mvua nyingi.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa rasmi ya utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2024 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka.

Katika hatua nyingine, Dkt. Chang’a ameshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa na hivyo kuiwezesha TMA kufikia hatua ya kuongeza usahihi wa utabiri.

Dkt. Chang’a amesisitiza jamii kuendelea kufuatilia taarifa za mara kwa mara zinazotolewa na TMA kwa vile ni za uhakika, huku akibainisha kuwa usahihi wa msimu wa Vuli 2023 ulikuwa asilimia 98.

By Jamhuri