Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar

Shirika la Posta Tanzania (TPC), limesaini makubaliano na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ili kurahisisha huduma kwa waombaji wa mikopo kupata unafuu na usaidizi pindi wanapoomba mikopo yao hasa kipindi hiki dirisha la maombi limefunguliwa.

Hayo yamesemwa na Postamasta Mkuu Macrice Mbodo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa makubaliano hayo yatawawezesha waombaji wa mikopo kuomba mikopo yao bila kuwepo na makosa mbalimbali.

Wanasheria wakitoa maelekezo kwa Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

Amesema kuwa pia watapata usaidizi kutoka kwa watumishi wa Shirika la Posta ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kuhakiki nyaraka zao za kuomba mikopo.

“Tumejipanga kikamilifu kuwasaidia waombaji ili kufikia malengo yao waliyojiwekea ya kusoma elimu ya juu kwa kupata mikopo ambayo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan aliahidi kulitekeleza kwa kiwango kikubwa.

“Lengo la Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ni kuwasaidia wote wanaotaka kwenda chuo kupata mikopo kwa kulitambua Shirika la Posta.

“Tumepanga kwa kuandaa intanenti cafe zaidi ya 36 na madirisha zaidi ya 100 lengo ni kumsaidia rais kutimiza malengo yake ya kila mwanachuo kupata mkopo,” amengeza.

Kulia ni Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Mbodo akipeana mkono na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Abdul-Razaq baada ya kusaini mkataba wa makubaliano.

Macrice Mbodo amesisitiza na kutaja faida kuwa unapofanya maombi kupitia TPC inakurahisishia kupata uhakika wa kutokukosea maombi yako lakini pia huduma zote zinapatikana kwa pamoja kupitia huduma pamoja kama RITA.

Aidha amewaondoa hofu waombaji na kuwaeleza wafike kwa wingi kwani TPC wimejipanga vya kutosha kuhakikisha wanawapatia huduma iliyo bora.

Pia ametoa rai kwa waombaji kuwa wasiende kuomba mikopo yao kupitia mafichoni kwani itawaletea usumbufu maana huko hawana utaalamu wa kutosha lakini pia hawana huduma za pamoja kama ilivyo TPC.

Amewataka waombaji kutongoja mpaka mwisho wa maombi ndipo wakimbizane na muda baala yake waanze sasa.

Naye Mtenaji Mkuu wa Bodi Ya Mikopo Ya Elimu Ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru amesema kwa sasa wanakoleza mashirikiano ya huduma baina ya TPC na HESLB kwa kuwa walishaanza kushirikiana tangu muda mrefu katika maeneo mbalimbali na sasa ni kongeza zaidi.

Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo ,kulia na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Abdul-Razaq wakionyesha hati za makubaliano ya mkataba wa uombaji wa mikopo wa wanafunzi wa elimu ya juu.

“Kwa sasa tuna kama mwezi tangu dirisha la maombi lifunguliwe hivyo ni fursa kwa waombaji wote kwenda katika ofisi za TPC ili kupata msaada wa kufanya maombi kupitia mtandao,” ameongeza.

Katika kuonyesha kuwa HESLB imefanya mabadiliko katika maombi ya mikopo amesema kwa sasa waombaji wanapoomba mkopo hawalazimiki kutuma nakala ya maombi yao badala yake unaomba kupitia mtandaoni pekee.

“Iili uweze kufanikiwa maombi yako basi ni vyema uombe kupitia TPC ili upate usimamizi sahihi.
Tangu dirisha la maombi lifunguliwe wameshaomba wengi sana lakini nikuhakikishie wengi walioomba kwa usahihi wamepitia TPC” amesema Badru

By Jamhuri