Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Katika kusherehekea siku ya Wanawake Duniani Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa tuzo ya mwanamke Mlipakodi namba moja Tanzania kwa mwaka 2023.

Mwanamke huyo ni Zainab Addan Ansell ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Utalii ya Zara International Travel Agency kutoka Mkoa wa kodi Kilimanjaro.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo leo Machi 8, 2024, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Hassan Mcha amesema hiyo ni hatua kubwa na yenye umuhimu katika kuleta mabadiliko na kuvutia mwanga kwa wanawake katika ulimwengu wa kodi.

“Tunakupongeza kwa juhudi zako katika kufanya kazi ya Utalii na mchango wako wa kipekee kuwa na ari kufanya tofauti. Endelea kung’aa na kuhamasisha wanawake wengine kufuata nyayo zako za mafanikio,” amesema Mcha.

Aidha ametoa wito kwa wanawake wa TRA kuendelea kuwa walinzi wa taswira nzuri ya Mamlaka hiyo kwa kuwa vinara wa uadilifu, weledi, uwajibikaji, na uaminifu katika kutekeleza majukumu ya utumishi wa umma ndani ya Mamlaka.

“Hii itaendelea kuweka taswira nzuri kwa wateja wetu tunaowahudumia na wakati huo huo tukijenga mahusiano mazuri na kuongeza ari ya ulipaji kodi wa hiari. Sote tunatambua kuwa wanawake ni jeshi kubwa hivyo mkisimama kidete katika hili mtaleta mabadiliko makubwa sana katika jamii yetu na kuiwezesha TRA kutimiza malengo yake ya ukusanyaji kodi kwa maendeleo ya taifa letu huku tukiunga mkono juhudi za Dk. Samia Suluhu Hassan,” amesema Mcha.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mwakilishi wa Kampuni ya Utalii ya Zara International Travel Agency, Leila Lakhan ameishukuru TRA kwa kutambua mchango wao.

“Nimefurahi sana na ninaahidi tutaendelea kulipa kodi zaidi. Hii tuzo inatuhusu tena mwakani,” amesema Leila.

Awali akitoa salam kwa niaba ya wafanyakazi wanawake wa TRA, Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala, Renalda Lyimo amesema kuwa wanatambua juhudi zinazofanywa na wanawake wa Mamlaka hiyo katika kuhakikisha malengo ya Taasisi yanafikiwa kwa kuweza kukabiliana na majukumu mazito ya kukusanya Mapato ya Serikali kwa ufanisi wa hali ya juu ilihali wakiwa wana endelea kufanya majukumu yao ya kifamilia pia.

By Jamhuri