Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Katika kusherehekea Siku ya Wanawake dunia ambayo hufanyika Machi 8, kila mwaka, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) umekuja na kampeni maalum ya kuhamasisha wanawake na wasichana kujisajili na umoja huo kielekloniki (Kidigitali).

Akiitambulisha kampeni hiyo, leo Machi 7, 2024 Katibu Mkuu wa UWT, Jokate Mwegelo amesema lengo la kuja na kampeni hiyo ni kutokana na mabadiliko ya teknolojia.

“Dunia ya sasa hivi imebadilika tunataka kuna jeshi la wanawake likiwa kidigitali…hii itasaidia kujua tuna wanawake wangapi na jinsi ya kuweza kuwasaidia.

“Tumetoa maagizo kwa makatibu wa kila mikoa kulisimamia hili kuhakikisha wanawake wote wanajisajili. Na tunatoa wito kwa wanawake nchi nzima kujitokeza kwa wingi kujisajili kidigitali,” amesema Jokate.

Aidha Jokate ametoa wito kwa UWT kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo, Jokate amehamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi hususani katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

“Katika uchaguzi tutahakikisha wanawake wanajitokeza katika nafasi mbalimbali. Lazima tukagombee kwenye nafasi hizo, kwani takwimu zilizopo hata asilimia 10 hatujafikia.

“Ifike mwisho wanawake kuwa ndugu watazamaji, tunaye kinara wetu Rais Samia…hivyo tutahakikisha kama kuna mwanamke anagombea anapitishwa na Chama na anashinda. Tutakesha kwenye Mitaa kuhamasisha wanawake kugombea na ninaomba niwatie moyo wanawake, hii ni fursa na akitokea mwanamke kugombea tusimkatishe tamaa,” amesema Jokate.

By Jamhuri