Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekutana na wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga jijini Dar es Salaam na kuafikiana kiwango cha kodi kwa kundi hilo ambalo limesema lipo tayari kushiriki katika ujenzi wa taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa TRA Mkoa wa Kikodi Kariakoo, Kabula Mwemezi amesema baada ya kutoa elimu ya mabadiliko ya sheria za kodi zilizopitishwa na Bunge la Bajeti Juni mwaka huu, wamachinga wamekubali kulipa Sh. 100,000 kwa mwaka.

Amesema kodi hiyo inalipwa kwa awamu nne ndani yam waka husika na itawahusu wamachinga wenye mzunguko wa mauzo ya Sh. 4,000,000 na zaidi.

“Nimefarijika kukutana na wamachinga na mwitikio wenu umenipa hamasa ya kufanyakazi. Tumesikiliza maoni na niseme tu tutaendelea kufanyakazi nanyi kwa karibu ili kwa pamoja tuijenge nchi yetu,” amesema.

Awali akifungua mafunzo hayo, Kaimu Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Edmund Kawamala, amesema wananchi wa ngazi zote wanapaswa kulipa kodi ili nchi iweze kutoa huduma muhimu zenye ubora kwa wananchi kama elimu, afya, maji na miundombinu.

.“Nia ni kuisaidia serikali yetu na Rais wetu ili aweze kutekeleza miradi yote ya kimkakati nchini,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wamachinga Kariakoo, Stephen Lusinde, ameishukuru TRA kwa kuwapa elimu na kueleza kwamba wafanyabiashara hao wapo tayari kulipa kodi.

“Hakuna hata mmoja wetu ambaye hayupo tayari kulipa kodi, tunachokiomba siku zote ni kututengenezea mfumo ambao utatuwezesha kulipa kodi katika mazingira yetu,” amesema.

Ameongeza: “Siyo haki wamachinga tupite bure kwenye barabara nzuri na watoto wetu wakisoma bure, tunatamani sana tushiriki kikamilifu kuijenga nchi yetu na nikuhakikishie kwamba hawa unaowaona hapa wote wako tayari kulipa kodi.

”Baadhi ya wamachinga waliozungumza katika mkutano huo wamesema kuwa TRA inapaswa kutoa elimu zaidi kwa kundi hilo ili waweze kushiriki kulipa kodi zote za serikali.

Raibu Omari ambaye ni mchuuzi wa viungo Kariakoo, amesema kabla sheria haijatungwa, TRA inapaswa kupata maoni ya kundi hilo ili utekelezaji wake uwe rahisi.

Naye Ummy Juma, anayeuza vijora Kariakoo, amesema wamachinga walikuwa wanagombana na mamlaka hiyo kwa kuwa hawakuwa wamewekewa mfumo rafiki wa kuwawezesha kulipa kodi.

“Kwa sasa tuko tayari kulipa kodi TRA ili tupate dawa kwenye hospitali zetu, tujenge barabara na watoto waende shule,” amesema.Kwa mujibu wa TRA, mmachinga anaweza kulipa kodi kwa kutengeneza namba ya malipo serikalini kupitia mfumo wa kielektroniki.

Kaimu kamishna wa kodi za ndani kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA), Edmund Kawamala akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 24,2023 jijini Dar es Salaam mara baada ya kufungua semina elekezi kwa baadhi ya wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) kuhusiana na mabadiliko ya elimu ya sheria za kodi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wamachinga Kariakoo, Stephen Lusinde, akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 24,2023 jijini Dar es Salaam mara baada ya kufunguliwa kwa semina ya kuwapatia elimu wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) kuhusiana na mabadiliko ya elimu ya sheria za kodi.

Ummy Juma mmoja kati ya wafanyabiashara ndogondogo

Baadhi ya wafanyabiashara wakiwa katika Mkutano na TRA.

By Jamhuri