Sitaki kuzungumzia matokeo ya mechi kati ya Yanga dhidi ya Simba. Kila mtu anajua matokeo yake. Kuna yaliyowafurahisha na wengine wamekereka. Ila kwa ujumla ninataka tutazame juu ya waamuzi wetu ndani ya Ligi Kuu. Na sitaitumia tu mechi hiyo kuangalia hilo, nitarudi nyuma kidogo kwa sababu kumekuwa na mlolongo wa matukio kama hayo katika ligi zetu.

Kuna wakati niliwahi kumtumia ‘e-mail’ ya maswali ya ‘kijinga’ mwamuzi aliyepata kuheshimika duniani, Pierluigi Collina. Kuna vitu nilitaka kujua kutoka kwake. Alinifundisha, alinielekeza.

Kile nilichopata kutoka kwake, nilimlazimisha mtu mmoja akasomee uamuzi. Nilitaka aandike kitu anachojua. Nafaurahi amekuwa mmoja kati ya waamuzi bora wa kike wa sasa na mara nyingi ‘anabishana nami’.

Kikubwa ambacho lazima tukikubali ni kwamba, ‘waamuzi wa Tanzania wanaisigina Ligi Kuu,’ ikiwa na maana wanaifanya ionekane ya ovyo. Mashabiki wamelalamika mno na wataendelea kulalamika kuhusu vitendo vya waamuzi wa soka kushindwa kuzitafsiri vema sheria zinazotawala mchezo huo, aidha kwa makusudi au kutojua, pale wanapokuwa wanachezesha.

Unaweza kushangaa ni kwa nini tunaendelea kulalamika kuhusu waamuzi, tunafanya hivi kwani hawa ndio watu muhimu zaidi hasa pale wanaposhindwa kutoa uamuzi wa haki.

Wanaweza kusababisha uvunjifu wa amani na hata vifo, kwani ushabiki wa soka ni kitu ambacho mara nyingi kinasababisha maafa kutokana na baadhi ya mashabiki kuwa na unazi wa kupitiliza.

Mwamuzi anaposhindwa kusimamia vema sheria na kanuni zinazotawala mchezo huo, mbali na kuchangia uvunjifu wa amani, pia anachangia kuzorotesha maendeleo ya mchezo huo.

Katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliamua kuwaondoa kuchezesha Ligi Kuu baadhi ya waamuzi kutokana na kushindwa kumudu michezo waliyopewa waisimamie.

Cha msingi ambacho tunataka kuishauri TFF, yaani ushauri wa bure usiohitaji kulipiwa, ni kwamba wataendelea kuwatimua mno waamuzi wanaochezesha mechi, hasa zile zinazozihusu Simba na Yanga, ila sasa wanatakiwa waitazame kwa jicho la tatu mechi inayokutanisha timu hizo.

Hatutaki kuwatetea hawa waamuzi wanaovurunda mechi kati ya Coastal Union na Ruvu au Simba na KMC, ila tunataka kusema kuhusu mechi kati ya watani hawa wa jadi. Hii ni mechi kubwa kuliko zote hapa nchini.

Ushauri huu usio wa lazima na kama wanataka waufuate au wauache, lakini ni vema katika kuondoa malalamiko wakati wa mechi zinazohusu timu hizo mbili, wakasaka mwamuzi kutoka nje ya nchi.

Wasichukue mwamuzi kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, bali wajaribu kuomba waamuzi kutoka nchi za Kusini mwa Afrika, Afrika Magharibi na hata Kaskazini.

Tunapozungumzia mwamuzi, tuna maana kuanzia yule wa kati mpaka wasaidizi wake. Wabaki na mwamuzi wa akiba na kamishna ambao watakuwa kutoka hapa.

Inawezekana, kwani hata Misri wameliona hili na mechi yoyote ya Al Ahly na Zamalek lazima waamuzi watoke nje ya nchi hiyo. Tunaamini hata kwa TFF kitu hiki kinawezekana.

Kuwabana waamuzi ina maana ni kuleta fedha, kwani ukiitazama La Liga, ililazimu mamlaka ya Hispania kufanyia mabadiliko sheria ya haki za matangazo ya uonyeshaji wa mechi za soka kupitia vituo vya runinga. Ifikapo mwaka 2016, timu zote za Hispania zitakuwa na haki sawa kwenye suala la malipo ya haki za mechi kuonyeshwa na vituo vya runinga.  Ila walianza kushughulika na waamuzi.

Hivi sasa Real Madrid na Barcelona ndizo zina haki ya kujadiliana na wamiliki wa televisheni juu ya malipo ya haki za kuonyeshwa mechi zao. Matokeo yake Barcelona na Real Madrid wameendelea kutajirika huku timu nyingine kama vile Cordoba na Malaga zikibakia katika hali ya umaskini, kwani wanachokipata kama malipo ya haki za mechi zao kuonyeshwa ni kidogo.

England klabu zimefaidika kupitia malipo ya haki za televisheni, hawatumii mfumo wa kinyonyaji kama ule unaotumika nchini Hispania.

Hispania yenye kutupatia starehe ya mechi za El Clasico kila mwaka wanataka kuondokana na mfumo huu wa mwenye kisu kikali ndiye mwenye kustahili kula nyama iliyonona, lakini sisi bado tunataka kuukumbatia mfumo uliopita na wakati. Ila tucheze na waamuzi kwanza.

Kuna maneno mitaani, kwamba Ligi Kuu yetu huwa na ushindani kwenye mechi za mzunguko wa kwanza pekee, unapoanza mzunguko wa pili wale wenye uhakika wa kubakia katika msimu ujao wanaanza kucheza ‘kirafiki’.  Waamuzi wanahusika.

Wachezaji wa timu nyingi za mikoani, wanaonyesha udhaifu tangu wakati timu zinafanya mazoezi ya viungo kabla ya kuingia vyumbani kwa ajili ya kutoka nje na kuanza mechi.

Charles Boniface Mkwasa

“Waamuzi bado ni tatizo na kuna haja ya kupigania hapa, ukiitazama Ligi Daraja la Kwanza unaweza hata kulia, ila cha msingi acha tusonge mbele.”

Luc Eymael

“Ni shida kubwa, unamaliza mbinu zako zote uwanjani, lakini mtu mmoja anakuja kukumaliza bila sababu. Hatutaki kusema sana, ila wanaosimamia soka walione hili.”

Sven van der Broeck

Kuna wakati inabidi ukubali ukweli, ila hauwezi kuwaacha waamuzi kando katika maendeleo ya soka. Wasimamie haki ili tuondoke hapa tulipo.”

Boniface Wambura

Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi anaamini waamuzi wapo sahihi na lazima wapewe nafasi ili kuendelea kujifunza zaidi na hakuna maana ya kumleta mwamuzi mgeni katika mechi kati ya Simba na Yanga. 

668 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!