Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, akizungumza wakati akifungua mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Agosti 25, 2024 mkoani Mara. Wadau hao ni pamoja na Viongozi wa vyama vya siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu, Wanawake na Wazee wa Kimila. (Picha na INEC).

Sehemu ya washiriki wa mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Agosti 25, 2024 mkoani Mara. Wadau hao ni pamoja na Viongozi wa vyama vya siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu, Wanawake na Wazee wa Kimila. (Picha na INEC).

Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, akiteta jambo na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Bw. Kailima Ramadhani wakati wa mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Agosti 25, 2024 mkoani Mara. (Picha na INEC).

………….

Na Waandishi wetu, Mara

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeviasa vyama vya siasa kutoingilia mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika vituo vya kuandikishia wapiga kura.

Wito huo umetolewa leo tarehe 25 Agosti, 2024 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Jacobs Mwambegele, wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika mkoani Mara.

Mhe. Jaji Mwambegele amesema mawakala au viongozi wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuingilia mchakato wa uboreshaji vituoni kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria ya uchaguzi.

Amehimiza viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kuzingatia sheria ya uchaguzi, kanuni za uboreshaji, maelekezo ya tume, na kusimamia miiko na mipaka ya uendeshaji wa zoezi la uboreshaji wa Daftari. 

Pia amevitaka vyama vya siasa kutumia sheria zilizopo kuwasilisha changamoto zinazojitokeza kwa tume, ambapo ameongeza kuwa INEC itazingatia Katiba, sheria ya uchaguzi, na kanuni zilizotungwa chini ya sheria katika zoezi la uboreshaji.

Akiwasilisha mada kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhan Kailima amsema Tume inategemea vyama vyenye usajili kamili kutumia fursa za kisheria zilizotolewa kwao kuhakikisha zoezi la uboreshaji linafanikiwa na kuongeza kuwa endapo kutajitokeza changamoto zozote wakati wa zoezi, Vyama vitumie taratibu zilizoainishwa kwenye sheria kuwasilisha changamoto hizo.

“Viongozi wa vyama hawapaswi kuingilia utekelezaji wa majukumu ya watendaji wa vituo wakati wote wa uandikishaji wa wapiga kura vituoni kama kuomba orodha au idadi ya walioandikishwa au kuboresha au kuhamisha taarifa zao,”

Ameeleza kuwa, Tume inaowajibu wa kuwapatia vyama vya siasa taarifa hizo mara baada ya zoezi kukamilika.

Mkutano kama huo umefanyika pia mkoani Simiyu na Manyara ambapo akifungua mkutano mjini Bariadi, mkoani Simiyu, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk S. Mbarouk, amewataka wadau kuwaelimisha wananchi kujiandikisha mara moja tu ili kuepuka uvunjaji wa sheria.

Naye Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari, ambaye alifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Manyara, amewahimiza watu wenye ulemavu, wazee, wagonjwa, wajawazito, na akina mama wenye watoto wachanga watakaokwenda nao vituoni kujitokeza kwa wingi kwa kuwa watapewa fursa ya kuhudumiwa bila kupanga foleni.

Mikutano hiyo ni maandalizi ya mzunguko wa nne wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao utajumuisha mkoa wa Mara, Simiyu na  baadhi ya halmashauri za Mkoa wa Manyara ambazo ni Halmashauri ya Mji wa Babati na Halmashauri za Wilaya za Babati, Hanang na Mbulu ambapo uboreshaji utaanza tarehe 04 Septemba, 2024 hadi 10 Septemba, 2024 na vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.

Please follow and like us:
Pin Share