Nape NnauyeKatika Tanzania ya leo tumefika mahali ambako maneno ‘ukweli’ na ‘uchochezi’ yanaonekana kama yana maana moja.

Mwandishi wa habari na wa magazeti akiandika ukweli mtupu bila kupindisha anaangaliwa kama mchochezi.

Mwanasiasa, hasa wa kambi ya upinzani, akisema ukweli mtupu bila kupindisha anaonekana mchochezi.

Tusubiri hili Bunge linalokutana sasa. Litakuwa na hoja nzito na nyeti za kujadiliwa. Hapana shaka Wabunge wa Kambi ya Upinzani watatoa mchango wao bila kupindisha kitu.

 Kwa hiyo kunaweza kuwa na zomea zomea. Wabunge wa kambi ya upinzani watazomewa kwa madai kuwa ni wachochezi pale watakapothubutu kuita shoka shoka badala ya kuita shoka jembe.

Ushabiki wa kisiasa umechangia pia kwa kiasi kikubwa watu kuonekana ni wachochezi pale wanaposema ukweli. Kwa jumla ukweli ni uwazi au usahihi wa mambo au hali halisi.

Kwa upande mwingine uchochezi ni kitendo cha kushawishi au kuhamasisha watu wachukue hatua zisizofaa katika jambo Fulani.

Turudi nyuma. Binafsi nimechoka kusikia watu wa UKAWA wakisema kwamba walishinda Uchaguzi Mkuu uliopita huku wanasiasa na mashabiki wa chama tawala wakidai kuwa ni wao walioshinda uchaguzi ule.

Kwa lengo la kusaidia umma wa Watanzania kujua ukweli wa mambo niliwashauri katika gazeti hili watu wa UKAWA waende Mahakama ya Afrika kutafuta haki kwa kuwa sheria za Tanzania zinakataza wananchi kwenda mahakamani kuhoji uchaguzi wa Rais.

Kwa kweli Tanzania ina haki ya kuingizwa katika rekodi ya vitabu vya Guinness kwa kuwa ni nchi pekee duniani inayokataza watu wake kwenda mahakamani kutafuta haki.

Nilitoa sababu zangu za kuwataka wapinzani kwenda Mahakama ya Afrika kutoa ushahidi katika madai yao kwamba walishinda uchaguzi wa mwaka 2015. 

Kwanza, kumaliza ubishi na majigambo. Wananchi wajue nani hasa alishinda uchaguzi huo. Ni uchochezi huo?

 Pili, kukomesha utamaduni wa kuiba kura(kama upo) ambao unahatarisha amani ya nchi pia usalama wa hao wanaoiba kura na washiriki wao. Ni uchochezi huo?

Tatu, niliandika kwa uwazi kwamba tumebahatika kuwa na Edward Lowassa ambaye baada ya kuona kwamba alikuwa ameporwa ushindi hakuhamasisha watu wa kambi yake kwenda kutafuta haki msituni baada ya kuzuiwa kwenda mahakamani kutafuta haki.

Nilisema kuwa katika siku zijazo tunaweza kuwa na mgombea uchaguzi ambaye akiona kwamba ameporwa ushindi hatavumilia. Ataingiza nchi kwenye machafuko. Ni uchochezi huo?.

Nikaongeza kwamba inawezekana kwamba kwa hivi sasa dunia inaamini kwamba Watanzania tunawekana madarakani kwa kuiba kura za washindi wa uchaguzi. Hii si sifa nzuri kwa taifa letu.

Ndiyo maana nikawashauri watu wa UKAWA waende wakatafute haki Mahakama ya Afrika. Ukweli ungemaliza aibu hii ambayo inapata chama tawala kila mwaka wa uchaguzi. Ni uchochezi huo?

Sidhani kwamba mtu mwenye akili timamu angeona kwamba kwa kushauri UKAWA uende Mahakama ya Afrika naleta uchochezi.

Haukupita muda, nikakuta ujumbe mfupi wa maneno (sms) katika gazeti la JAMHURI toleo la Januari 12- 18 mwaka huu ukiwa na kichwa cha habari  ‘Halimoja mchochezi’ ni ujumbe uliotumwa na mtu mwenye namba 0682 978 334.

Kwa faida ya wasomaji ambao hawakusoma gazeti hilo ili wafahamu alichosema mtu huyo nanukuu maneno yake yote. Ujumbe wake ulikuwa hivi; “Mzee Yusuf Halimoja acha uchochezi. Uchaguzi umekwisha, washindi wamepatikana.  Kama huwataki walioshinda andamana na Edward Lowassa wako ‘aliyeshinda’. Hatudanganyiki. Pole sana unalo!”.

Kwamba uchaguzi umekwisha, hakuna asiyejua. Lakini hata kama uchaguzi umekwisha vitendo vya wizi wa kura umeendelea kulalamikiwa kila baada ya uchaguzi.

Tena kuna kesi za Ubunge na Udiwani zimeendelea kusikilizwa baada ya uchaguzi. Kwa hiyo kuna haja ya kuchukua hatua ya kukomesha wizi wa kura kwa kupeleka shauri hili Mahakama ya Afrika ili ukweli ujulikane.

Sitaki ionekane naumia eti kwa sababu Edward Lowassa hakushinda uchaguzi kama inavyodaiwa ingawa yeye mwenyewe ameendelea kudai kwamba alishinda uchaguzi huo.

Nataka nionekane naumia kwa sababu tunakosa uchaguzi huru na wa haki, naona hatari iliyoko mbele yetu kama tutaendekeza wizi wa kura.

Ndiyo maana mashirika ya kimataifa yasiyopungua 1200 yalimchagua kumpa tuzo ya amani Lowassa katikati ya watu 1000 kwa kuepusha maafa.  Bila taifa kuungana kukomesha wizi huu wa kura maafa aliyoepusha Lowassa siku moja yanaweza kutokea akitokea mpinzani atakayekosa uvumilivu. Na huu si uchochezi, ni kulitaka taifa lichukue tahadhari. Ni kulitakia mema taifa langu.

Kwa kweli niliposoma ujumbe ule, kama ningeona kwamba aliyepeleka ujumbe huo ni mjinga ningemwelimisha. Lakini niliona kwamba aliyepeleka ujumbe huo ni mpumbavu ambaye ningekuwa  ninapoteza wakati wangu kuwasiliana naye.

Sasa tuangalie uchochezi wa gazeti la MAWIO. Limefutwa kwa madai ya uchochezi. Gazeti la  MAWIO liliandika  ‘Machafuko yaja Zanzibar’. Kwa vyovyote hii si kauli ya uchochezi. Ni kauli ya kutahadharisha kutokana na hali mbaya ya kisiasa iliyopo Zanzibar. Kwa jumla kuandika ‘Machafuko yaja Zanzibar’ ni sawa na kuandika ‘Machafuko yanukia Zanzibar’. Hapo uchochezi uko  wapi? Si kuzungumzia ukweli tu wa hali halisi  iliyopo Zanzibar?

Na kama MAWIO lilifanya utafiti likapata kura zilivyopigwa kuna ubaya gani kuchapisha? Kama takwimu za MAWIO si sahihi, si zingeletwa tu takwimu sahihi? Uchaguzi wa Zanzibar ulimalizika na ulifanyika kwa uwazi. Kwa nini yafichwe matokeo?

Lazima tuseme kweli. Ukiangalia utawala wa CCM unavyoendeshwa Tanzania utasema kwa haki kabisa kwamba afadhari wakato wa mkoloni. Hebu tuangalie Mwingereza alivyoshughulikia kesi za magazeti mwaka 1958.

Rais wa TANU, Mwalimu Julius Nyerere, aliletwa mahakamani kwa madai ya kukashifu wakuu wawili wa Wilaya ya Kikoloni katika jarida la ‘Sauti ya TANU’ ambalo yeye alikuwa mhariri wake.

Kesi ikasikilizwa mahakamani ingawa kulikuwa na Waziri wa habari wa serikali ya kikoloni. Hakuona haki ya kufuta jarida lile bila shauri kufikishwa mahakamani.

Mwaka huo huo wahariri wa gazeti la Mwafrika, Rashidi Baghelleh na Robert Makange, walifikishwa mahakamani kwa madai ya kuandika uchochezi katika gazeti lao.

Waliandika kwamba Mwingereza  hakuwa Tanganyika kwa lengo la kuwaletea ustaarabu wananchi kama alivyokuwa akidai bali kwa lengo la kuwanyonya.

Kesi yao ikasikilizwa na mahakama na hukumu ikatolewa. Lakini gazeti halikufutwa. Mwingereza alihukumu wahariri. Hakuhukumu gazeti.

Sasa tuna utawala  au serikali ya wananchi. Ni kweli Mwingereza alikuwa mtawala wa kigeni lakini aliheshimu na alifuata utaratibu. Hakuchukua sheria mkononi, alijali mgawanyo wa madaraka. Alijua nafasi ya mahakama katika kushughulikia masuala ya kutoa haki.

Utawala wetu wa leo ambao unadai ni utawala wa sheria umechukua sheria mkononi. Waziri anaamua kufuta gazeti bila kutoa nafasi kwa mahakama kusikiliza shauri lote na kutetea uamuzi.

Na angalia, wakati tayari Waziri amefuta gazeti, Polisi iliwaita wahariri ili wajieleze ikawaweka mahabusu  wakati tayari Waziri amekwishaamua kufuta gazeti? Kwa nini shauri hili halikupewa nafasi kusikilizwa na mahakama kwanza? Kwa nini shauri moja liamuliwe na Waziri kisha na polisi?

Hapa tuna utawala wa mabavu ambao sasa umewatia woga wahariri na waandishi wao. Hawajui waandike nini maana ukweli umegeuka kuwa uchochezi. Ni vyema polisi wakaitisha semina ya wakuu wa vyombo vya habari ambayo itazungumzia kwa uhuru tofauti kati ya ukweli na uchochezi. Magazeti yafanye kazi kwa uhuru na amani.

Lakini pia tunalazimika kujiuliza, hivi Serikali ya CCM si Serikali ya wananchi? Serikali ya wananchi ingetambua kuwa wahariri na waandishi wao ni sehemu ya Serikali na wana haki ya kuzungumzia masuala ya  nchi yao kwa uhuru bila kutishwa na bila kusumbuliwa.

Pengine jambo hili linashangaza. Nape Nnauye anafuta gazeti kwa madai kwamba linaandika uchochezi wakati yeye mwenyewe ni mchochezi nambari wani. Ni majuzi tu Nape alipokitaka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimfukuze kutoka kwenye chama Lowassa eti ni fisadi.

Hivi kwa nini Nape anaendelea kumsakama na kumvunjia heshima Edward Lowassa wakati amewaachia CCM yao? Nape hajui kuwa Lowassa ni mtu wa kimataifa na si saizi yake? Nape ni nani mbele ya Lowassa?

CCM tuliyoijua, ilisisitiza kuwa kiongozi sharti awe mtu anayeheshimu watu. Hapa tuna kiongozi wa CCM asiyeheshimu watu. Hakika CCM imekwisha.

Mwaka 1970 nilipelekwa Iran na Ghana kuchukua mafunzo ya uenezi. Ilisisitizwa kwamba mtu wa uenezi anatakiwa awe mwenye kuheshimu watu na mwenye uhusiano mzuri na watu.

Si huyu Nape. Kwani ndani ya CCM hakuna mafisadi? Wapo mafisadi wa rada, Epa, Escrow na wengine wengi tu, mbona Nape hawafukuzi? Sasa basi, Nape amemsikia Edward Lowassa akishikilia kuwa alishinda uchaguzi wa mwaka jana. Kwa kuwa huyu Nape ni Katibu Mwenezi wa CCM tunataka akanushe madai hayo ya Lowassa.

Nape atuambie kama Lowassa alishinda  urais akaporwa ushindi au hakuporwa. Na huu si uchochezi bali ni kutafuta ukweli. Tunasubiri.

1931 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!