Tunatenda makosa ya elimu tukidhani tuko sahihi

KILIMANJARO

Na Nassoro Kitunda

Mara zote kumekuwapo na mjadala wa elimu hapa nchini hasa katika kupima ubora wake huku kukiwa na makundi tofauti yanayotoa maoni. Wapo wanaosema elimu yetu imeshuka na kuna haja ya kubadili mitaala na wengine wanaona kuwa suala si mitaala bali ni mbinu za kufundishia ndipo kuna shida.

Lakini kila kundi linaona kuna haja ya kuitisha mjadala wa kitaifa juu ya elimu. 

Lakini katika makundi haya, wote wanakubaliana kuipima elimu kama sehemu ya majengo bora, uwepo wa vitabu, walimu na ufaulu wa shule husika. Kwa hiyo, msisitizo mkubwa umewekwa katika ufaulu. Tumekuwa tukilinganisha ubora wa elimu wa kila shule na kila matokeo nani kawa wa kwanza nani kawa mwa mwisho?

Pia tumekuwa tukiona waandishi wa habari wakiwahoji wanafunzi waliofaulu vizuri. 

Kwa matukio haya, ndiyo sehemu ambayo elimu yetu inajadiliwa.  

Katika makala hii, nitajikita zaidi kuonyesha makosa tunayoyafanya na kuyahalalisha na kudhani ndiyo sahihi na elimu yetu inapaswa kwenda hivyo. Lakini pia nitaonyesha nini elimu yetu inapaswa itizamie.

Kupima elimu kwa matokeo/ufaulu

Niligusia hapo juu katika mjadala uliopo namna tunavyopima elimu yetu. Hii ni sehemu ya makosa tunayoyafanya, kupima ubora wa elimu kwa matokeo ya mitihani. 

Na ndiyo jamii na mamlaka husika tunafikiri huko na wakati fulani hata shule ikishindwa kufaulisha mwalimu mkuu unakuta anashushwa cheo au anakuwa na kesi ya kujibu. Kwa shule za serikali na shule binafsi mwalimu unaweza kujikuta hauna kazi. 

Hii imefanya hata wazazi kudhani shule ya elimu bora ni ile inayofaulisha vizuri. Shule zimekuwa zikishindana na kila mmoja kujiona bora kwa kufaulisha.

Zimekuwa zikitumia ufaulu kujitangaza na kusema wao mwaka jana walifaulisha vizuri kuliko shule nyingine na wao ndio bora. 

Kupima elimu kwa majengo

Nadhani hii pia ni sehemu nyingine ambayo kama makosa tunayoyafanya katika elimu yetu ni kufikiri kuwa na majengo mazuri ndiyo ubora wa elimu unapatikana. 

Kwa hiyo tunatumia muda mwingi kujenga shule, madawati na kuzungushia shule ukuta, tukiamini tunafanya elimu yetu kuwa bora zaidi. Au kufanya ukarabati wa miundombinu ya shule mbalimbali. 

Ni sehemu muhimu, lakini tunashindwa kujua  majengo yanapaswa kuwa matokeo ya kile kinachofundishwa na kwa kiasi gani kinaeleza ukweli wa maisha yetu.

Tunadhani elimu pekee inapatikana shuleni au chuoni

Hii pia inaweza kuwa sehemu ya makosa, tunadhani kuwa elimu lazima wote twende shuleni na huko ndiko inakopatikana. Kwa hiyo, tunawaeleza watu na jamii kuwa lazima twende shuleni au ndiko maarifa yanapatikana. 

Mwalimu Julius Nyerere katika kitabu chake cha ‘Tujisahihishe’, alisema tunakuwa tunafanya makosa kudhani elimu ni kwenda shuleni na kila mtu afikie huko. Hoja hii ililenga kusema elimu iwe ni utafute ukweli popote utakapokuwa. 

Lakini nadhani tumetoka huko na tumebaki hapo kuwa ili mtu aelimike ni lazima aende chuoni au shuleni. 

Elimu inapaswa itazame nini?

Katika hoja nilizozieleza hapo juu, kama makosa tunayoyafanya katika elimu yetu na kudhani ndiyo elimu inapaswa kuwa. Sasa ni muhimu kutoa tafsiri ya hoja hizo hapo juu. 

Kwa ujumla tunapaswa tuweke msisitizo juu ya falsafa ya elimu kwanza kabla ya mambo hayo niliyo yaeleza ya kutathmini matokeo, majengo au kudhani elimu ipo shuleni au chuoni tu. 

Kwa muda sasa, hatujaweka wazi juu ya falsafa yetu ya elimu inasukumwa na itikadi gani? Kipindi cha Mwalimu Nyerere, elimu ilikuwa na falsafa ya ujamaa na kujitegemea, ilikuwa inaeleza juu ya kueleza mifumo ya uzalishaji mali, kwanini sisi ni maskini na ilikuwa wazi kueleza kwa kina sababu za mifumo ya uchumi ya kibepari juu ya kutoendelea kwetu na kutoa mwelekeo wa lazima tujitegemee ili kukabiliana na unyonyaji huo. 

Lakini sasa hatuna falsafa na tumekuwa tunadhani suala la matokeo ya ufaulu, majengo na ajira ndiyo elimu yetu tunaipima ubora wake. Mwalimu Nyerere  katika kitabu chake cha ‘Tujisahihishe’ anasema kujielimisha si maana yake kwenda shuleni. Kama hivyo ingekuwa ndivyo, TANU ingekuwa imefanya kosa kubwa kumtaka kila mwanachama ajitahidi kujielimisha na kutumia elimu yake kwa ajili ya wote. 

Kujielimisha ni kutafuta ukweli wa mambo. Kwenda shuleni hutusaidia.  Ni kutafuta ukweli wa hali zetu za jamii, maisha na shida zetu. Lakini pia namna ya kukabiliana na hali zetu. 

Ndiyo maana kulikuwa na elimu ya kujitegemea, kujitegemea si kwa mtu, ni kwa taifa kupambana na ubeberu. Lakini sasa yapo makosa hayo tunaona elimu ni mtoto kufaulu mtihani na kufika chuoni lakini si tena kutafuta ukweli sahihi wa matatizo yetu. Mwalimu anasisitiza mpumbavu ni yule anayeyapa mambo sababu zisizo za kweli na kutoa dawa isiyo ya kweli katika kutafuta sababu za matatizo na kuyaondoa. Sasa lazima tujiulize, je, elimu yetu inazipa sababu za kweli matatizo yetu? 

Kwa hiyo, naweza kusema elimu inayotakiwa ni inayotupa ukweli wa hali zetu kwanini tupo hapa na tunatokaje? Tunapaswa tufikiri zaidi ya majengo (madarasa) na kuongeza idadi ya walimu, sisemi madarasa si muhimu, la hasha! Ni muhimu kwa sababu yanawafanya watoto wasome katika mazingira mazuri au walimu hawahitajiki, tunahitaji walimu sana, wana umuhimu sana katika elimu yetu. 

Lakini la muhimu zaidi ni kufikiri falsafa tuliyonayo katika elimu inatosha kutupa ukweli wa mambo? Ni swali ambalo Mwalimu Nyerere ametuachia. 

Kwa sababu elimu ni zaidi ya madarasa na walimu. Elimu kama nilivyosema awali ni kutafuta ukweli, si lazima tuwe katika darasa au chuo ndipo tutajua ukweli wa mambo, ukweli unatokana na falsafa sahihi ya kuonyesha hali halisi ya shida zetu na matatizo yetu, tuliyokuwa nayo. 

Kwa hiyo si kwenda shuleni tu, si kuwa na majengo tu. Kwa ufupi, msisitizo lazima uwekwe katika kile kinachofundishwa, kinasukumwa na ajenda gani? 

Kimebeba falsafa gani? Falsafa ya ukombozi? Au falsafa ya kupumbaza watu wasione uhalisia wa jamii na maisha yao? Mambo haya lazima yapewe kipaumbele katika mijadala yetu tunayoiibua katika elimu. 

Tusiishie kujadili madarasa, majengo, ukarabati wa miundombinu, kuongeza walimu na ufaulu pekee bali tuipe nafasi hoja ya elimu kuwa sehemu ya kutafuta ukweli wa maisha yetu. 

Rai yangu

Ni kwamba tutumie wakati wetu kujadili falsafa ya elimu, na si falsafa tu, falsafa itakayotueleza ukweli ndani ya elimu yetu. 

Wakati fulani tulikuwa na falsafa ya elimu iliyotueleza ukweli wa maisha yetu, kwanini tupo hapa chini ya Azimio la Arusha?

Lakini naona sasa hatupo nayo tena, tumeacha ukweli, na tumeanza kuhubiri masuala ya ujasiriamali, ajira, uhamasishaji watu kujiajiri na kuacha sehemu kubwa ya elimu ya kutafuta ukweli, kwanini bado umaskini upo?

Si suala la kujiajiri tu, bali tuangalie mifumo tuliyonayo ya kiuchumi, kwa kiasi gani inatubakisha katika umaskini? 

Lakini namna sasa tunavyopima umaskini, tunaupima kwa urahisi, sasa elimu inabidi iseme na kutafuta ukweli juu ya shida hii ya umaskini, si tu kusema tuwe wajasiriamali. 

Hivyo, mimi nachochea mjadala katika jamii kama sehemu ya mwanazuoni na kutoa mchango wangu kwa jamii, tufikiri katika haya, wakati wa ujenzi wa sera na miongozo yetu kwa kuwashirikisha wananchi katika elimu yetu.