Wiki iliyopita Umoja wa Ulaya umetoa tamko lenye kulitahadharisha taifa letu kuepuka matukio yasiyo na siha njema kwa afya ya taifa. EU wamesema wanafuatia ongezeko la matukio ya kisiasa yenye viashiria vya ukatili na vitisho Tanzania. EU kwa ushirikiano na Mabalozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wenye uwakilishi Tanzania na kuungwa mkono na Mwakilishi na Mabalozi wa Norwei, Canada na Uswisi wameasa.

Wamesema wanashuhudia kwa wasiwasi mwendelezo wa matukio ya hivi karibuni yanayotishia nidhamu ya kidemokrasia na haki za Watanzania, katika nchi iliyojizolea umaarufu mkubwa duniani kwa utulivu, amani na uhuru.

Wamemesikitishwa na kifo cha mwanafunzi aliyepigwa risasi Akwilina Akwilini Bafta, aliyeombolezwa nchi nzima. Wakasema wanakaribisha wito wa Rais John Magufuli wa uchunguzi wa haraka katika mauaji hayo. Vilevile, wakatoa wito wa uchunguzi wa kina katika vifo vyote vya wanaharakati wa kisiasa na haki za binadamu. Wakatoa pole za dhati kwa familia zao zote.

Wakasema wana wasiwasi na ongezeko la ripoti za ukatili katika miezi ya hivi karibuni, kama vile: jaribio lililohatarisha maisha ya mbunge Tundu Lissu; kupotea kwa watu kama mwandishi wa habari Azory Gwanda; na mashambulio yaliyopoteza uhai wa viongozi wa serikali, wawakilishi wa vyombo vya usalama na wananchi yaliyotokea Mkoa wa Pwani ndani ya miaka miwili iliyopita.

Wakaungana na Watanzania katika kuwaomba wahusika wote, kutunza amani na usalama wa michakato ya kidemokrasia, nchi, watu wake na kuheshimu utawala wa sheria bila udhalimu.

Sisi tunasema tamko hili limekuja wakati mwafaka. Tumesikia baadhi ya wanasiasa wameanza kulibeza wakisema limetolewa kwa kuwa Tanzania imekata mirija ya unyonyaji uliokuwa unafanywa na kampuni zao. Tunasema inawezekana baadhi ya wanasiasa hawatalipenda tamko hili, ila ukweli ni kwamba watu wanapotea na kuna mauaji yasiyofahamika yanatokana na nini.

Tunaungana na Rais Magufuli kutaka wote waliohusika na mauaji ya Akwilina na watu wengine wakiwamo askari wanane waliouawa eneo la Mpakani Mkuranga wasakwe na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria haraka. Tusipodhibiti mauaji na upoteaji wa watu haraka, mbele ya safari tutajenga taifa la visasi na tutajikuta tunakuwa kama Somalia, Iraq, Syria, Afghanistan, DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati na nyingine zenye mauaji kwani nazo zilianza kidogo kidogo kama taifa letu lilivyo sasa. Chondechonde, tulinde amani yetu. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

By Jamhuri