Rais John Magufuli alipozungumza na viongozi wa dini, kwa chini chini kulionekana tofauti za hapa na pale. Tofauti hizo hazikuzungumzwa kwa mwangwi, na kwa maana hiyo ilisaidia kutoibua hisia za utengano.

Kiongozi mmoja wa Kikristo alitoa maombi yaliyonikumbusha maneno niliyopata kuyaandika miaka kenda iliyopita na kuyarejea mwaka 2013. Katika safu hii niliandika makala iliyokuwa na kichwa cha habari: ‘Wakati mwingine Wakristo wanaanzisha chokochoko.’ Nakumbuka nilipokea simu na sms nyingi kutoka kwa wahafidhina walioniona nimekusudia kuukwaza Ukristo. Hawakuwa sahihi.

Makala yangu ilitokana na mapendekezo ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) ya kutaka kubadilishwa kwa siku ya kupiga kura ya maoni kutoka siku ya ibada – Jumapili. Mapendekezo ya CCT yaliwasilishwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala. Mwakilishi wa CCT, Mchungaji Lazaro Rohho, akasema mabadiliko hayo yanatakiwa kuwekwa kwenye muswada wa kura ya maoni uliokuwa unatarajiwa kuwasilishwa bungeni.

Kwenye mazungumzo ya Rais Magufuli na viongozi wa madhehebu ya dini, jambo hili lilijitokeza tena.

Mjadala huu umekuwa ukijitokeza mara kwa mara. Baadhi ya Wakristo wamekuwa wakitaka Jumapili isiwe siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Hoja yao mara zote imekuwa kwamba kutokana na Jumapili kuwa siku ya ibada, inawawia vigumu kushiriki uchaguzi huo vizuri!

Hili jambo ni muhimu tukalijadili hata kama wapo watakaokwazika. Sharti tulijadili kwa sababu tunataka kuijenga Tanzania yenye utangamano, mshikamano na zaidi ya yote kuwa na Tanzania ya kuvumiliana.

Mara zote Watanzania wema wanaoitakia heri nchi yetu wamesisitiza sana kuvumiliana. Uvumilivu unaozungumzwa hapa unatuhusu sote – Wakristo, Waislamu na wale wasioamini Mungu huyu wa kwenye Kurani na Biblia.

Mara zote nimesema kuwa madai haya ya Wakristo ya kuanza kuhamasisha Jumapili isiguswe yanaweza kuibua madai mazito kutoka kwa Waislamu na watu wa imani nyingine. Waislamu wanaamini kabisa kwamba Ijumaa kwao ni siku takatifu.

Ndiyo siku yao kuu ya ibada. Wakristo si wote wanaoamini Jumapili kuwa ndiyo siku takatifu. Wapo Wasabato wanaoitambua Jumamosi. Lakini yapo madhehebu mengine mengi ya asili yasiyokubaliana na siku hizo tatu – Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.

Waislamu, pamoja na ukweli huo, na bila kujali wingi wao, wameridhia Ijumaa isiwe siku yao maalumu ya mapumziko. Ndiyo maana utawaona wakiwa katika ofisi za umma na ofisi binafsi wakichapa kazi. Hawajawahi kusema Ijumaa isiguswe kwa namna yoyote ile na shughuli za kiserikali au za kijamii. Wamekuwa wakiswali, kisha kuendelea na mambo mengine kadiri inavyowezekana.

Kitendo cha wao kukubali siku yao ya ibada – Ijumaa – itumike kwa shughuli nyingine, ni uvumilivu wao kwa ndugu zao Wakristo. Wakikomaa tunaweza kujikuta tukiwa na siku tatu za mapumziko katika nchi hii, yaani Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.

Kwa desturi tuliyokwishakuwa nayo ya kuifanya Jumapili siku ya Uchaguzi Mkuu, ni kwamba jambo hilo halijaathiri kitu chochote miongoni mwa Wakristo. Sana sana ni uamuzi uliosaidia kujenga mshikamano na uvumilivu miongoni mwa Watanzania wa madhehebu haya makubwa.

Kwa hili la Uchaguzi Mkuu, sioni ubaya wowote kwa miaka mitano Wakristo kutenga siku moja tu ya Jumapili kwa ajili ya kupiga kura.

Miaka mitano ina wastani wa siku 1,825 hivi. Miaka mitano ina Ijumaa 260 hivi. Ndani ya siku hizo 1,825 Waislamu wamekubali siku zao 260 ziingiliwe na mambo mengine ya umma. Kama wao wameweza kuvumilia kwa siku 260, kwanini Wakristo wawake kwa siku moja tu kutumika kufanya jambo ambalo hata maandiko yanalitambua? Kwanini wanataka tuongeze siku nyingine ya mapumziko? Tumekuwa taifa la kuwaza mapumziko tu!

Sina hakika kama kweli mtu anaweza kuhukumiwa kwenda motoni kwa sababu Jumapili moja ndani ya miaka mitano hakuhudhuria ibada kanisani! Kwenye maandiko mamlaka za utawala za kidunia zimetambuliwa. Je, kweli ni kosa kubwa la mtu kuukosa ufalme wa mbinguni kwa sababu tu ya kutokwenda au kuchelewa kwenda kanisani mara moja ndani ya siku zaidi ya 1,800? Kweli hii ni hoja ya kutusumbua vichwa na kuleta hisia za u-sisi?

Wapi kumeandikwa kuwa ibada lazima ifanyike asubuhi? Wapi kunakosema Mungu hapokei sala za jioni? Kama sivyo, kuna ubaya gani kuwahi kupiga kura, kisha waamini wakaenda kwenye ibada? Au kuna ubaya gani kuwahi kwenye ibada, kisha mtu akajielekeza kwenye uchaguzi?

Wakristo wa kweli ni watu weledi. Ni wavumilivu. Kunapoanza kutolewa madai ya aina hii, ni wazi kuwa upande wa pili nao ni kama wanaambiwa waanze kuleta madai yao. Sote tukitaka tutendewe kadiri ya matakwa ya matamanio yetu tutaivuruga nchi.

Mei 30, 2010 katika Gazeti la Mtanzania niliandika makala inayofanana na hii. Mmoja wa viongozi waandamizi katika taifa letu alipoisoma aliniunga mkono. Akaniletea barua pepe. Napenda kunukuu maandishi yake hapa, lakini kwa kuwa hakunipa ridhaa ya kuichapisha, naomba nilihifadhi jina lake. Alisema hivi:

Ndugu Manyerere Jackton, nimeipenda sana makala yako iliyochapishwa katika Gazeti la Mtanzania la leo Jumapili, tarehe 30, Mei 2010, uk. wa 7. Nimeipenda kwa sababu ni makala ambayo ina sifa ya kuwa na “nguvu ya hoja”, kutokana na utafiti ulioufanya katika maandiko matakatifu ili kuimarisha hoja yako.

Kusema kweli, hilo ‘Jukwaa la Maaskofu’ lilitoa kauli ya kukataa uchaguzi usifanyike siku za Jumapili, limefanya kosa la kujielekeza kwenye tatizo ambalo halipo kabisa, kwani si tatizo halisi, bali ni tatizo la kufikirika tu.

Mimi ni Mkristo, na nimekuwa nikipiga kura (pamoja na Wakristo wenzangu wengi tu) katika kila uchaguzi mkuu uliofanyika siku za Jumapili kila miaka mitano tangu mwaka 1965. Vilevile, nimekuwa nikipiga kura pamoja na Wakristo wenzangu wengi tu, katika chaguzi ndogo nyingi sana za ubunge na udiwani, ambazo zimekuwa zikifanyika siku za Jumapili tangu wakati huo hadi leo. Lakini mimi na Wakrito wenzangu hao hatujawahi hata mara moja kushindwa kwenda kanisani kusali katika siku hizo, eti kwa sababu ya kukosa nafasi ya kufanya hivyo kwa kuwa tulikwenda kupiga kura!

Nimetaja mapema hapo juu kwamba makala yako ina nguvu ya hoja. Kinyume cha maneno hayo ‘nguvu ya hoja’, ni ‘hoja ya nguvu.’ Kwa hakika, Jukwaa la Maaskofu limetumia ‘hoja ya nguvu’ katika kuzungumzia jambo hili.

Kama ulivyoeleza wewe katika makala yako, kura zinapigwa kuanzia saa moja asubuhi hadi saa kumi jioni, ambao ni muda wa kutosha kabisa kuwezesha mambo yote mawili kufanyika. Napenda kuongeza kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi inao utaratibu mzuri tu wa kupanga idadi ya wapiga kura katika kila kituo cha kupigia kura wasizidi watu 350. Idadi hiyo inawezesha wahusika kufanya shughuli zao nyingine kabla au baada ya kupiga kura, bila hofu ya kuikosa nafasi hiyo ya kutekeleza wajibu wao wa kiraia.

Siku aliyoingia madarakani kama Waziri Mkuu wa Uingereza, Mhe. Tony Blair, alisema maneno ya busara yafuatayo katika mkutano wake na waandishi wa habari wa nchi hiyo:

“What is good and working well, we will keep.

 What is not, we will change”

Utaratibu wa kupiga kura siku za Jumapili ni mzuri. Na umefanya kazi vizuri tangu mwaka 1965. Yafaa tuendelee nao.

Mwisho wa kunukuu.

Maneno ya kiongozi yule wa dini yanaibua chokochoko. Hayalengi kujenga utangamano miongoni mwetu Watanzania. Yanaibua hisia za kila madhehebu kuanza kudai mambo ambayo mustakabali unaweza kuwa mbaya.

Kalenda inayotumika sasa (Gregorian) inatambulika kama kalenda ya Kimagharibi au kalenda ya Kikristo. Wakati Waislamu wengi wakiwa wamekubali kuutambua mwaka huu kama mwaka 2019, kwenye kalenda yao kama sikosei huu ni mwaka 1438.

Pamoja na ukweli huo, Waislamu hawasikiki wakitaka sasa kalenda yao ndiyo itambulike hapa nchini. Wameamua kuikubali ile ya Kikristo kama sehemu tu ya uvumilivu na staha; wakitambua kuwa hawawezi kupata wanayotaka kwa asilimia 100. Kadhalika, Wakristo nao wanapaswa kuwa na moyo wa aina hiyo. Jumapili moja kwa jambo lenye heri kwa nchi, sidhani kuwa kutamfanya Mkristo aonekane kwa Mungu wake kuwa ni muasi. Tuishi kwa kuvumiliana.

Please follow and like us:
Pin Share