Tutafakari vyema uamuzi wetu Oktoba

 

Unaweza ukajiuliza ni kwanini Ugiriki imeyumba vibaya kiuchumi? Sababu zipi za kiuchumi zilizoifikisha hapo ilipo?

Mwalimu Julius Nyerere alipata kusema kuwa ubepari ni unyama. Na nikiwa kizazi kipya na wala si mhafidhina kwa baadhi ya sera, bado ninaendelea kuuona ubepari mkongwe kuwa ni changamoto kubwa kwa nchi zetu zinazoendelea.

Ninaamini kuwa na dira halisi ya kiuchumi na ule umakini mkuu wa kuyatenda machache yaliyo makubwa miongoni mwa yale mengi ya kuyatenda kwa rasilimali zetu, ndiko hasa kutakakotusukuma mbele kutoka hapa tuliko. Uwepo wa viwanda vingi vya kati kwa malighafi tulizonazo, kunabaki kuwa hitaji lililo mbele litakolotupeleka tunakotaka.

Tukiendelea kuzalisha vilivyo bora na kulinda soko letu la ndani huku tukitengeneza na kubuni njia nyingi za soko la nje, hakika tutauinua uchumi na kukiepuka kikombe walichokipata Ugiriki. Kuyumba uchumi wa Ugiriki kuliusukuma Umoja wa Ulaya (EU) na zile kauli nzito za Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kuwapatia mikopo ya fedha nyingi yenye masharti mahsusi ili kuwakwamua kiuchumi.

Maofisa wa fedha na mawaziri wao na kama kawaida yao walichora suluhisho la tatizo la Ugiriki. Walitoa maagizo ya kufuatwa yakiwamo kupunguza matumizi makubwa yasiyo ya lazima ya serikali, kuziangalia sera zao kwa wafanyakazi wa taasisi za umma na wabia wa biashara huria, kupunguza madeni yao — yote yakiwaelekeza kujifunga na kuukaza mkaja.

Yalipita mengi ya ile mikikimikiki ya maandamano ndani ya nchi yao. Wapo walioliangalia tatizo lao kushabihiana na milengo ya siasa za vyama vyao. Na hapa ndipo hasa ninapotilia mkazo kwani waliibuka wananchi walioona ipo haja ya kuwachagua na kukabidhi nchi iongozwe na vyama vyenye mlengo wa kushoto ulio mkali na si vile vya kulia.

Waliendelea kuiangalia mikopo na masharti waliyopewa kama kitanzi cha waya, walikosoa kutowafikia walengwa — wananchi — na kusema serikali yao inaielekeza kwa zile taasisi kubwa za kibiashara zenye ubepari mwingi usiowasaidia wafanyakazi na wananchi wa hali ya chini.

Katikati ya matatizo yao akatokea mwanasiasa wa chama cha Syriza cha mlengo mkali wa kushoto, Alexis Tsiparas (40). Huyu alikuja na mawazo ya kiuchumi yaliyokinzana na msisitizo waliopatiwa kutoka Brussels, Ubelgiji. Syriza ikapinga na kuendelea kupinga vikali hatua za kimageuzi ya kiuchumi.

Hatimaye wananchi wakaipigia kura na kuichagua na sasa itaunda serikali itakayoongozwa na Alexis Tsiparas. Hapa tunajifundisha kuwa kwa nchi yetu Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM) bado kinatakiwa kuendelea kuaminiwa kuendelea kuiongoza nchi kwa kule kujianika vyema kwa sera zake bora za kiuchumi, sera zinazoendana na uhalisia wa mnyonge wa Tanzania.

CCM ni tofauti na vyama vifuatavyo mlengo wa kulia ama ule wa kati ambavyo wenzetu wa Ugiriki wamekataa kuvikabidhi kuunda serikali ya nchi yao.

Tanbihi inakuja; iweje kwa wananchi wa nchi yetu changa kiuchumi tena yenye rasilimali nyingi zinazohitaji kulindwa vyema dhidi ya ubepari mkongwe kutoipa kura CCM, chama ambacho kisera kinaendelea kutambua uhalisia wa changamoto za ubepari na vyama vyenye mlengo huo?

 

Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kuwa ni msomaji wa gazeti hili. Anapatikana kwa barua pepe: [email protected] au namba ya simu 0714 534 574