Ukraine yaivuruga Urusi

Vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea nchini Ukraine imeelezwa kutanuka na kusambaa nchini Urusi baada ya kiongozi wa upinzani, aliyepata kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Urusi, Boris Nemtsov, kupingwa risasi mwishoni mwa wiki.

Wanaharakati wanasema Nemtsov ameuawa na vyombo vya dola kutokana na msimamo wake wa kupinga Urusi kuwaunga mkono waasi nchini Ukraine na kupinga hatua ya Urusi kuungana na Jimbo la Crimea, mwaka jana.

Inadaiwa kuwa watu wasiofahamika walimpiga risasi nne Nemtsov mgongoni wakati anavuka daraja karibu na makao makuu ya Chama tawala Kremlin nchini hapa.

Kifo chake kimetokea zikiwa ni saa chache kabla ya kufanyika kwa maandamano aliyoitisha jijini Moscow kupinga Serikali ya Rais Vladimir Putin kujiingiza katika vita nchini Ukraine akidai Putin anaunga mkono waasi nchini Ukraine.

“Rais Putin ameamua kusimamia uchunguzi wa kifo hiki mwenyewe,” alisema Msemaji wake, Dmitry Peskov. “Inaonekana ni mauaji ya kupangwa,” anaongeza.

Rais wa Marekani, Barack Obama alilaani mauaji hayo aliyoyaita ya kinyama na kutaka ufanyike uchunguzi wa haraka na wa wazi.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko amemtaja Nemtsov kama daraja lililokatika kati ya Ukraine na Urusi. “Muuaji ameharibu kila kitu. Nadhani si kwa bahati mbaya,” alisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa facebook.

Boris Nemtsov alikuwa mmoja wa wachumi waliofufua uchumi wa Urusi katika miaka ya 1990.

Hivi karibuni, Nestov alitoa kauli kuwa anahofia msimamo wake wa kupinga uvamizi wa Putin nchini Ukraine Rais Putin angeweza kumuua.

Kinachotokea ni mwendelezo wa matukio. Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, zimeiwekea Urusi vikwazo kadhaa, ikiwamo viongozi na wafanyabiashara mbalimbali waliozuiliwa kusafiri katika Bara la Ulaya na Marekani.

Vikwazo hivi vinahusisha uuzaji wa bidhaa na huduma kutoka Urusi kuingia katika nchi za mabara hayo. Baada ya kumwekea vikwazo, Urusi nayo ilipopatiwa kibano hicho ikaamua kuzuia bidhaa kutoka nchi za Ulaya na America ikiwamo Ujerumani na Ufaransa.

Baada ya kuzuia Ujerumani na Ufaransa zikapata maumivu makubwa. Ikabidi viongozi wa juu wa mataifa hayo wasafiri kwenda Urusi kuona jinsi ya kupoza mambo. Hata hivyo, mgogoro unaendelea kufukuta kwa kasi kubwa kwa kiwango ambacho baadhi ya wachambuzi wanadhani mgogoro huu unaweza ukaingiza dunia kwenye vita kuu ya tatu.

Urusi kwa upande wake, wanasema hadi sasa hawana majeshi nchini Ukraine na askari wanaoonekana nchini Ukraine wapo kwa ajili ya kutoa msaada wa kibinadamu.

Urusi inauza asilimia 24 ya gesi inayotumika katika Bara la Ulaya, hivyo leo ikiamua kusitisha biashara moja kwa moja na bara hilo wanaweza kupata tabu kubwa.