Na Mwandishi Wetu, Mwanza
SERIKALI kupitia Waziri wa Maji Jumaa Aweso,imeusimamisha uongozi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), baada ya uzembe uliosababisha adha ya kukosa huduma ya maji kwa zaidi ya wiki mbili kwa wananchi wa maeneo mbalimbali jijini Mwanza.
Aweso alichukua hatua hiyo jana mkoani Mwanza mara baada ya kufanya ukaguzi wa ghafla katika baadhi ya miundombinu ya maji, ambapo alibaini uzembe na kasoro mbalimbali zikiwemo mivujo ya maji na baadhi ya matenki kukosa maji,ikiwa ni utekekalezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu uhaba wa maji uliodumu kwa zaidi ya wiki mbili katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Mwanza.
“Nimefanya maamuzi ya kusimamisha uongozi wote (manejimenti) nzima,idara zote na vitengo vya MWAUWASA na kuvunja idara yote ya ufundi.Tutaanza upya na kuisuka MWAUWASA itakayotoa matokeo ya haraka na kuimarisha hali ya upatikanaji wa maji,”alisema Aweso.
Aweso alisema,walienda kwenye tenki la maji Buswelu lenye ujazo wa lita milioni 3,akiwa ameambatana na Mbunge wa Ilemela,lakini walipofika huko juu walikuta hakuna maji huku akiuliza kwanini maji hakuna lakini hakupata majibu.
Alisema baada ya hapo walienda kwenye tenki jingine lenye uwezo wa lita milioni 13,lakini walikuta maji yanapotea na kuvuja kwa kiwango kikubwa kuliko yanayokwenda kwa wananchi.
“Inakuwaje wananchi wanakosa huduma halafu maji yanavuja kwa kiwango hiki na pale maji yanapotoka mengi wanaweka mawe.Katibu Mkuu akasema maji yanapotea mengi,nikamuuliza kwa nini ,hapa kuna changamoto ya fedha au uzembe akajibu uzembe,”alisema Aweso.
Pia alisema alimuuliza Meneja wa Ufundi ambaye ndiye msimamixi wa mambo yote ya Ufundi kuhusu hali hiyo lakini hakumpa majibu licha ya kumtaka ampatie taarifa ya Hali ya utoaji huduma ya maji kwa Jiji la Mwanza.
“Unaweza kumpenda sana mtoto wako lakini akiumwa,ulienda kwa Daktari anasema ili alone anatakiwa kupiga “cristerpen”ingawa inauma,na hawa lazima tuwapige “cristerpen”.Tulienda Nyegezi hali ni mbaya kwenye matenki,”alisema Aweso.
Sanjari na hayo alisema awali walikuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 90, lakini sasa wanazalisha lita milioni 138 huku kukiwa na miradi ya 8 yenye thamani ya zaidi ya milioni 100,hiyo yote ni kuhakikisha wanamaliza tatizo la maji kabisa.

