Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania TANESCO imepiga hatua nyingine katika kuimarisha miundombinu ya nishati nchini baada ya Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb.), kuzindua rasmi Kituo cha Kubadilishia Njia za Usambazaji Umeme (Switching Station) na Transforma ya Kudhibiti Umeme leo Juni 16, 2026. katika eneo la Mbande, Wilayani Kongwa, Mkoani Dodoma.

Mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 10.5 unalenga kutatua changamoto ya muda mrefu ya kukatika kwa umeme na mabadiliko ya nguvu za umeme (low voltage) kwa wananchi wa Wilaya ya Kongwa na maeneo ya Jirani Kabla ya uwekezaji huu, wananchi wa Kongwa walikuwa wakitegemea njia moja tu ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Dodoma Mjini, hali iliyolemewa na kuathiri shughuli za kiuchumi kutokana na kukua kwa mahitaji.

Katika hotuba yake, Waziri Ndejembi amebainisha kuwa mradi huo umehusisha ujenzi wa miundombinu thabiti ikiwemo njia mpya ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Zuzu hadi Mbande yenye urefu wa kilomita 92, pamoja na kusimika transforma yenye uwezo wa MVA 20.

Waziri amezipongeza kampuni zilizoshirikiana kufanikisha ujenzi huo ambazo ni State Grid Electrical & Technical Works Limited, Central Electricals International Limited, pamoja na Ezeetec Limited kwa kukamilisha kazi hiyo kwa viwango vinavyotakiwa.

Kukamilika kwa miundombinu hiyo sasa kunakwenda kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme katika wilaya nne za kimkakati ambazo ni Kongwa, Gairo, Chamwino, na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Mpwapwa.
“Tunatarajia kuona ongezeko la shughuli za uzalishaji mali, kuimarika kwa biashara, uwekezaji na utoaji wa huduma za kijamii kutokana na uwepo wa huduma ya umeme wenye uhakika zaidi”. Amesema Mhe. Ndejembi huku akiwataka wananchi kulinda miundombinu hiyo dhidi ya uhujumu.

Ujenzi wa kituo hicho cha Mbande ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali kupitia mpango wa Grid Imara vituo vingine kama hiki tayari vimeshajengwa maeneo ya Msigani Dar es Salaam na Mugumu Mara, huku transforma za kudhibiti umeme AVR za uwezo wa 20MVar zikiwa tayari zimeshafungwa mkoani Songwe eneo la Songwe Mkwajuni na mkoani Kagera.