Wiki hii nimewaza na kuwazua. Kwa furaha nimepokea mrejesho kutoka kwenu wasomaji wangu. Hakika nimefurahi jinsi mlivyolikubali gazeti JAMHURI, na jinsi mawazo tunayoyatoa mnavyoyaunga mkono. Nasema asanteni sana na mkihisi tumekosea, msisite kutusahihisha.

Baada ya utangulizi huu, nikukumbushe msomaji wangu kuwa wiki iliyopita nilizungumzia mpango wa kodi ya simu kuwa ilikuwa sawa na kodi ya kichwa. Nimepata mrejesho mkubwa na nafurahi kuwa na sehemu ya watu waliotoa mchango wa mawazo katika hili.

Nikutaarifu msomaji wangu kuwa Serikali imetoa taarifa rasmi kupitia kwa Waziri wa Fedha, William Mgimwa, kuwa kodi hii imesitishwa. Sasa muswada wa kodi hii utapelekwa bungeni mwezi Agosti kwa nia ya kuifuta rasmi. Nasema nimefarijika sana na hatua hii.

Sitanii, wapo walionihoji kwa nini nimepinga kodi hii? Nimejitahidi kuwafafanulia, lakini moja nililisahau katika ufafanuzi huo. Nimekaa na kuwaza, nikabaini kuwa kitendo cha kumlipisha kodi ya Sh 1,000 kila mwezi anayemiliki simu, kilikuwa kinyume na sheria ya kodi inayozuia bidhaa moja kutozwa kodi mara mbili.

Ninachomaanisha ni kwamba ukinunua simu dukani unailipia kodi. Ukinunua muda wa maongezi, unaulipia kodi. Tena tayari kuna kodi ya huduma ya asilimia 14 kwenye muda wa maongezi, hivyo kilichotaka kufanyika hapa ni wizi mtupu!

Sitanii, katika kichwa cha makala haya napendekeza tuwatelekeze wabunge, na tuwawezeshe polisi. Wapo watu wanaoweza kushindwa kuelewa namaanisha nini nisipofafanua. Hapa namaanisha ukweli kuwa wabunge ndiyo chimbuko la umasikini unaotukabili sisi kama Watanzania.


Hawa wameweka maisha yetu rehani kwa kuwa wamekula hadi wakavimbiwa.

Hivi ninavyoandika makala haya ikiwa yupo mbunge ambaye pato lake ni chini ya Sh 500,000 kwa siku kwa maana ya Sh milioni 15 kwa mwezi, anyooshe kidole juu kisha amwambie Mwenyezi Mungu; “Mimi mbunge silipwi kiasi hiki na kama nadanganya niondoshe duniani sasa hivi.”

Wala sitoi siri, posho ya vikao ni Sh 200,000 kwa siku. Mshahara si chini ya 100,000 kwa siku. Posho ya kujikimu nje ya jimbo 80,000 kwa siku. Mafuta ya kutembelea jimbo 83,000 kwa siku. Posho ya dereva (siitaji italeta mgogoro). Mfuko wa Jimbo (usiokaguliwa). Vikao vya mashirika na bodi mbalimbali (wengine wanakimbizana hata na vikao vitatu kwa siku).

Sitanii, hawa hata kama wanatokana na chama kinachounda ‘Serikali Sikivu’, hawawezi kupata nafasi ya kuwaza Maisha Bora kwa Kila Mtanzania. Wameshiba. Wenye njaa wanawasumbua. Si unajua tena shibe ni mwana malevya na njaa ni mwana malegeza? Ukishiba unatamani kupata usingizi kidogo. Hivyo ndivyo walivyo wabunge wetu walio wengi.

Nini kinachotokea? Hawa walioshiba nyamachoma za Dodoma na bia zinazokaribia kuexpire zinazouzwa kwa mbwembwe za ‘promotion’ wakati wa vikao vya Bunge, hata ukumbini wanakuwamo kama hawamo. Ndiyo maana inapitishwa kodi ya simu ya Sh 1,000 kila mwezi bila wao kuiona.

Kodi hii ilipofika uraiani huku kwetu, tukaipinga na kuipigia kelele, nao wakajifanya kuungana na sisi. Eti wanaanza kusema, imepitishwa na Serikali. Ndugu msomaji, Serikali haipitishi muswada wala kutunga sheria bungeni. Wanapitisha wabunge wetu hawa wanaosinzia mchana, na wala usiniulize usiku saa za kulala wanafanya nini?

Serikali yoyote duniani inatafuta mbinu za kupata mapato. Ni kazi ya wabunge kukataa hayo yanayopendekezwa na Serikali. Hiyo ndiyo maana ya kuishauri na kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba. Hivi Serikali ambayo bajeti yake ina nakisi ya zaidi ya asilimia 30 unatarajia isifanye umafia wa aina hiyo?

Baadhi, ama wabunge wengi ni wakware. Wanatumia vijisenti vyetu vinavyotokana na kodi kuharibu miili yao. Wanatelekeza familia. Tena wenyewe wanatwambia ndani ya ukumbi huo mtukufu kuwa wapo wanaopata mimba zisizotarajiwa. Ni bahati tu kuwa wabunge wote wanaungana kupinga mpango wa David Cameron, vinginevyo ingekuwa kihama hapa kwetu!

Sitanii, muda wanaoutumia kusaka senti ni mwingi kuliko muda wa kupitia ‘document’ wanazopewa bungeni na kuibuka na mawazo chanya. Juzi nilibahatika kukaa na kundi la wabunge pale Mlimani City, Dar es Salaam. Kwa masikitiko nasema nilijichanganya katika kundi la wabunge tisa, ila kati yao ni mmoja tu aliyekuwa ameisoma neno kwa neno rasimu ya Katiba mpya.

Hawa ndiyo tunaotarajia watutungie Katiba hivi karibuni. Nasema Watanzania tujiandae kuandamana au kupinga Katiba ikiwa itapitishwa Katiba mbovu. Wala msihofu. Kodi ya simu si wameitunga wenyewe? Si tumewalazimisha kulamba matapishi yao? Agosti wanatunga sheria ya kuifuta rasmi. Wenyewe wanaita marekebisho.

Kimsingi, nasema hawa hawana muda wa kuwaza jinsi gani nchi yetu itaongeza mapato. Na hapa ndipo napendekeza kuwa tuwafutie masilahi manono wanayopata, tuyahamishie kwa polisi. Tena wala tusifanye roho mbaya. Polisi tuwape wastani wa Sh 100,000 kwa siku. Kila polisi aweze kukunja Sh 3,000,000 kwa mwezi. Utaona matokeo.

Sitanii, polisi hawa wanakula rushwa ya mikate barabarani kwa sababu ya njaa. Wanapokea hongo ya Sh 1,000 kutoka kwa madereva wa daladala kutokana na njaa kali. Tena kibaya zaidi siku hizi wamewekewa wale wanaoitwa Polisi Jamii. Polisi Jamii wana nguvu kubwa ajabu. Wanawarekodi hadi polisi na kupeleka kwa mkubwa.

Hawa Polisi Jamii wasiooma ndiyo wenye radio call (simu za upepo za polisi) mkononi. Hawa wasioapa siku hizi wanafanya kazi ya vehicle inspectors (wakaguzi wa magari). Wamekuwa vinara wa rushwa. Hawa ndiyo wanaovujisha SIRI za umahiri wa Jeshi la Polisi, na wakati mwingine ‘kuwatonya’ majambazi polisi doria iko wapi.

Mimi nasema Polisi Jamii wafanye kazi, lakini ni kero. Wamepewa madaraka kuliko uwezo wao halisi. Wengi ni vibaka waliokuwa mitaani, lakini leo ndiyo kwa kuvalishwa hivi vikoti vilivyoandikwa polisi, wana kauli nzito kuliko hata Said Mwema, Mkuu wa Jeshi la Polisi. Ni kawaida, ukitaka kumjua binadamu mpe madaraka.

Sitanii, ebu tulinde heshima ya nchi yetu. Polisi Jamii wafanye kazi kama sungusungu. Wasipewe radio call kama nilivyoshuhudia hivi karibuni eneo la Mwenge, au kukagua magari kama ilivyo eneo la Banana, Dar es Salaam. Pick-up ikipakia hata bati moja, kwa Polisi Jamii ni kosa. Hii ni kero. Magari ya mizigo yakipakia mizigo ni kosa siku hizi.

Mazingira kama hayo yanawafanya polisi kukata tamaa. Taarifa zilizopo ni kuwa Mwema amewaruhusu Polisi Jamii kuwapa amri askari wa kawaida. Hii kama ndivyo ilivyo ni aibu. Haikubaliki. Askari wamesomea jinsi ya kumkamata mhalifu, kuchunguza mashauri na hata kukagua magari, si hawa vibaka wa Polisi Jamii waliokusanywa kutoka vijiweni wakiwa wakwapuzi, leo tunawakabidhi kazi ya kutenda haki. Hapana.

Sitanii, hivi unatarajia polisi akichanganya hasira za mamlaka yake kupokwa na Polisi Jamii, akashuhudia wakubwa serikalini wanasajili kampuni hewa tatu au zaidi zinalipwa hadi milioni 600, wanatembelea mashangingi na yeye buti imechanika hana hadi ‘kiu’, ukiingia kwenye anga zake atakufanyaje? Ukiwa mwanasiasa unakwenda Jangwani kuandamana atakuponyesha kweli? Jibu tu.

Sitanii, polisi wetu wakilipwa Sh 3,000,000 kwa mwezi, magari ya doria yakajazwa hadi lita 100 za mafuta kwa siku badala ya lita tano, wakapewa mamlaka ya kukamata kila aliye na bidhaa isiyo na risiti ya elektroniki, kwa maana ya zile zinazotolewa na TRA moja kwa moja, hakika ndani ya mwaka mmoja tu, tutamwita Rais Barack Obama wa Marekani kuja nchini kumkabidhi msaada akasaidie watu wa taifa lake.

Utajiri wetu unaishia mikononi mwa wachache. Tena kwa ulafi tu maana kama mtu tayari ana kiasi cha Sh bilioni hadi 10 kwenye akaunti, unajiuliza anatafuta fedha za kufanyia nini? Ndiyo maana nyumba zinachipuka kama uyoga Dar es Salaam na ukiwauliza wanaojenga hawadaiwi hata mkopo.

Tunashangaa wimbi la askari kukamatwa na pembe za ndovu, bangi, dawa za kulevya, madini, mbao na magogo, lakini nasema hii isiwashangaze. Polisi wanaokamatwa na bidhaa hizi ni wa Arusha, Dar es Salaam, Kilimanjaro na mikoa mingine iliyochangamka. Kwa vijijini polisi wanasafirisha gongo, mbao, mkaa na kimoro kwa kutumia magari ya polisi! Unacheka?

Hapa kinachotokea ni nini? Hizi ni ishara. Kabla sijazisema ishara hizi, nisema linalowezekana. Inawezekana Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema na, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, wameamua kusimamia sheria bila ubaguzi. Kwamba wameamua kukamata kila awaye, bila kujali ni JWTZ, Polisi, Magereza au Sungusungu. Ikiwa ndivyo, hongera zao.

Sitanii, ninachodhani ni ishara ni mwangwi wa kinachoendelea serikalini. Kama polisi wanamkamata mtu anayeendesha ujangili kisha inapigwa simu kutoka juu anaachiwa kabla hawajamaliza kufungua jalada, unatarajia nini? Kama askari anakamata magogo, wakati anajiandaa kupiga simu kwa mabosi wake kutoa taarifa, anapata simu ya mwanasiasa akimtaka asindikize mzigo huo, unatarajia nini?

Tena simu hiyo haiji kwa upole. Anamwambia “usindikize mzigo huo ‘nitakucheki’ kama hutaki sema nimwambie bosi wako ‘B……’ aje ausindikize mwenyewe.” Na kweli siku anayokuwa lindo akakataa kuusindikiza, kwa mfano, bosi wake anapigiwa simu anafika na kuusindikiza kisha anamlisha yamini. Wiki inayofuata atatoa taarifa huyo?

Sitaki kuamini kuwa kadhia hii ya dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam wakubwa wa pale macho yao yamepigwa upofu. Nafunguka, wakati umefika kulinda heshima ya nchi yetu. Hatuwezi kukusanya kodi kwa kuwa na askari polisi wanaoshindia mahindi na mihogo ya kuchoma, huku wafanyabiashara wakiwazawadia baskeli za kufukuzia majambazi.

Polisi wetu wakilipwa vizuri, watafanya kazi kwa umakini mkubwa kwani wameapa kudhibiti wahalifu. Tukumbuke nao wanataka kusomesha watoto, kujenga nyumba nzuri na hata kusaidia ndugu zao badala ya kuendelea kuishi kwenye nyumba za mabati pale Bunguruni.

Sitanii, nafasi inazidi kuwa finyu. Nahitimisha kwa kusema kwa faida ya Taifa letu, kwamba hebu tuwape polisi kila wanachohitaji kufanya kazi yao vizuri, na tukiishafanya hivyo tuwalaumu wakishindwa.

Tukiwawezesha polisi, ujambazi utatoweka, pembe za ndovu zitapona, magari ya polisi hayatabeba mikaa, wafanyabiashara wahuni hawatakwepa kodi, na muhimu kuliko vyote tutakusanya kodi na kuifanya Tanzania kuwa Taifa tajiri kuliko yote Afrika na hatimaye duniani.


1430 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!