Na Angalieni Mpendu

“Kuondoa uvivu, ugoigoi na woga katika nchi ni kazi ngumu. Mambo haya yanapendwa sana na watu ingawa yana madhara makubwa.”

Pia ni vizuri kutambua dhana kuwa “busara kubwa kichwani haina faida kama moyoni hamna chembe ya wema” ama “waungwana hawasemi  uwongo”.

Nukuu tatu hizo `nimezichota’ kutoka kwa bingwa wa lugha ya Kiswahili, mshairi stadi na mwanafasihi mbobezi hapa nchini, marehemu Sheikh Shaaban Robert, aliyezaliwa na kuzikwa Vibambani Machui mkoani Tanga. Aliishi kuanzia Januari 01, 1909  hadi Juni 22, 1962 alipofariki dunia.

Kwa maana nyingine ni sawa na kusema, alizaliwa katika ardhi ya iliyokuwa Tanganyika. Nimetumia neno Tanganyika makusudi badala ya Tanzania kuweka uzito na upendo wa marehemu na nchi yake.

Sheikh Shaaban Robert alizaliwa, alilelewa, alipata elimu ya madrasa na shule, na alifanya kazi katika Serikali ya Tanganyika (kwa wakati huo).

Alioa na alipata watoto.Alitumia vizuri maisha ya uhai wake wa miaka 53 duniani katika makuzi, kupata elimu, kufanya kazi na kutunza ndoa na watoto wake. Alichukuana vyema na jamii iliyomzunguka popote alipokwenda na kuishi ndani ya nchi yake.

Kauli alizozitoa wakati ule hadi sasa bado zina nuru na zinawasuta baadhi ya Watanzania katika matendo yao ya kupenda uvivu, ugoigoi na woga; na kuchukia kufanya kazi na kupuuzia kutunza na kulinda rasilimali za nchi.

Hadi sasa hekima zake kwetu ni tunu, tamu na muhimu kama zilivyo za marehemu wenzake. Mwenyezi Mungu azidi kumrehemu. Amin!

Ni kweli nchi kuondoa uvivu ugoigoi na woga ni kazi ngumu kwa sababu watu wanapenda na wanashindwa kutambua upofu na uziwi walionao.

Uhuru wa Tanganyika ulipatikana Desemba 9, 1961 ikiwa na idadi ya watu milioni tisa. Sensa ya watu ya mwaka 1967 ilibaini idadi hiyo kuongezeka kufikia milioni 12.3 na ya mwaka 2002 wakafikia milioni 34.6 wakati ile ya mwaka 2012 wakawa watu milioni 45 milioni.

Hivi sasa tunakadiriwa kufikia watu 55 milioni. Nusu ya watu hao ni nguvu kazi ndani ya taifa lililo maskini.

Nguvu kazi hiyo ina baadhi ya watu wavivu, goigoi, waoga na tegemezi kwa watu wachache wenye uthubutu na uwezo wa kufanya kazi.

Makundi hayo yanapenda mno ubwete. Ndio hao waliotajwa na marehemu Sheikh Shaaban Robert. Tunamuelewa?

Rais John Pombe Magufuli anafanya juhudi ya kuondoa uziwi na upofu wa makundi haya katika kutunza na kulinda rasilimali ya Taifa.

Anakemea watu hao wasipewe chakula iwapo hawaendi mashambani na viwandani kufanya kazi ili tuondokane na umaskini.

Cha kushangaza wanachomoka watu wenye busara vichwani mwao wanapinga juhudi hizo na huku wakijinasifu wana wema ndani ya mioyo yao.

Ndipo pale Shaaban Robert aliposema,” busara kichwani haina faida kama moyoni hamna chembe ya wema.”

Moja wapo ya sifa ya uzalendo ni kuwa na uungwana; na muungwana ni mkweli wa kauli na matendo.

Nchi hupata maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni pale watu wake wanapobeba sifa hizo na kutambua maisha ya mtu ni msingi wa maendeleo ya nchi.

Wavivu, goigoi na waoga wameiweka nyuma Tanzania katika maendeleo ya uchumi.

Watanzania hatuna budi kujinasua kutoka katika majira haya, na kubadilika kimawazo na matendo, kuchapa kazi, kulinda na kudhibiti rasilimali za umma.

Daima, busara inatusihi na kutuongoza  Watanzania tuwe wamoja wa kauli na matendo, tupate maendeleo ya kiuchumi. Tukumbuke, “kipawa chochote cha mtu kama hakikuongozwa vyema huweza kuwa hatari na maangamizi kwa wengine.” (Shaaban Robert).

Watu tumejaa tele Tanzania. Ardhi iko ya kutosha kwa mahitaji yetu. Siasa yetu ni ya kujitegemea na uchumi wa viwanda kuelekea uchumi wa kati.

Tunachohitaji ni uongozi bora wa kuelewana, kukubaliana na kushirikiana katika mabadiliko ya kweli ya kujenga Tanzania mpya.

By Jamhuri