Mafanikio yoyote yana sababu (14)

Na Padre Dk. Faustin Kamugisha
 
Kuwa na ndoto na kuzifanyia kazi ni siri ya mafanikio. Watu wanaofanya vitu vikubwa wanaota ndoto kubwa. Watu wanaofanya vitu vingi sana wanaota ndoto nyingi sana.
 
“Unaamini katika ndoto? Ukitaka ndoto zako ziwe ukweli wa mambo usipitilize katika kulala! Usiache ndoto ziwe jinamizi,” alisema Henrietta C. Mears (1890–1963) mwelimishaji.
 
Kuwa na ndoto itakayokufanya uamke asubuhi na mapema, ukiwa mchangamfu na kuifuatilia na kuifanya iwe ukweli wa mambo. Ndoto ni maono.
 
Ndoto hizi si zile ambazo zinatokea wakati umelala fofofo bali ukiwa macho. Ndoto ni jina lingine la kuwa na picha ya kesho uitakayo, picha ya vitu unavyovitaka, picha ya unayetaka kuwa. Ni jina jingine la kupanga na kufikiria.
 
Katika karne ya 19 ndugu wawili walikuwa na wazo ambalo liligeuka kuwa mbegu ya ukweli. Nao ni Wilbur Wright na Orville Wright wa Marekani.
 
Wakiwa vijana walirusha tiara (Kishada kilichofungwa kamba ambacho hurushwa hewani ili kiruke angani). Walifikiria kuwa binadamu anaweza kurushwa angani kwa kanuni za tiara.
 
Walifikiria kutengeneza “meli ya angani,” au chombo cha angani. Walichekwa. Gazeti la New York Times la 1903 lilisema kuwa wanasayansi wasipoteze muda na pesa kwa majaribio ya chombo cha angani.
 
Wiki iliyofuata ndugu hao walifanikiwa kuruka angani. Hawakuwa na shahada yoyote ya Chuo Kikuu ya Elimu ya angani, Uhandisi, Fizikia au Hesabu.
 
Somo tunalojifunza hapa ni kuwa unapokuwa na ndoto unakuwa na mbegu za ukweli. Mfano wa ndoto kuwa kweli ututie motisha ya kuzifanyia kazi ndoto kama ndugu wawili wakina Wrights.
 
Lakini watu wengi wa Brazil wanaamini Alberto Santosa (1873-1932) ndiye mvumbuzi wa ndege wa kwanza. Na wengine wanaamini Ni Richard William Pearse (1877 – 1953) wa New Zealand.
 
Hoja yangu si kuangalia ni nani hasa mvumbuzi wa kwanza, bali ukweli kuwa ndoto iligeuka ukweli wa mambo. Watu wote huota ndoto. Kuna ambao wanaota ndoto wakiwa wamesinzia, lakini kuna ambao wanaota ndoto wakiwa macho.
 
Wengi wanaoota ndoto wakiwa usingizini wakiamka wanakuta ni ubatiri mtupu. Kuna wanaoota ndoto wakitembea bila usingizi, au wakiwa wamekaa bila kusinzia. Wanaziweka ndoto zao katika matendo, wakiwa na macho yaliyofunguliwa.
 
“Wale wanaoota ndoto wakati wa mchana wanatambua mambo mengi ambayo uwaponyoka wanaota tu usiku,” alisema Edgar Allan Poe. Jua si kila jicho ambalo limefumbwa limelala. Na si kila jicho lililofunguliwa linaona.
“Waota ndoto ni wasanifu wa ukubwa. Akili zao zimeleta miujiza yote ya kibinadamu… Nyumba zenu ziko kwenye ardhi ambayo muota ndoto aliitafuta. Picha ukutani ni maono kutoka kwa muotaji… Ni wateuliwa wachache – ni waonyesha njia wanaoweka alama- ambao hawavai bendeji ya mashaka kwenye macho yao,” alisema Herbert Kaufman.
 
Ni maelezo mazuri sana kuhusu waotaji. Lakini lazima kumwingiza Mungu katika ndoto zako asaidie kuleta “miujiza.” Nakubaliana na Conrad Hilton aliyesema: “Mtu na kwa msaada wa Mungu na kujitoa kibinafsi, anaweza kufanya lolote analoliotaka.”
 
Conrad Hilton (1887 – 1979) alianzisha hoteli za Hilton. Alianzisha mfumo wa viwango wa hoteli wa nyota moja hadi tano. Kwa kutazama hoteli za Hilton zilizoenea pande nyingi za dunia tunaweza kusema kuwa waota ndoto ni kama wasanifu wa majengo, wanasanifu ukubwa na mafanikio.
 
Kipimo cha mtu mkubwa ni ndoto zake kubwa anazozifanyia kazi. Ota makubwa. Hakuna kitu kinafanyika bila kukiota. Kama umejenga nyumba uliota kujenga nyumba. Kama umelima shamba la mazao ya chakula au biashara, uliota kulima shamba hilo. Kama umeanzisha biashara fulani uliota kuanzisha biashara hiyo.
 
“Baadhi ya watu huona mambo yalivyo na hujiuliza: ‘Kwa nini?’ Mimi naota ndoto za mambo ambayo hayakuwepo najiuliza: ‘Kwa nini yasiwepo?” alisema George Bernard Shaw (1856 – 1950) mzaliwa wa Ireland na mshindi wa tuzo la Nobel katika Fasihi mwaka 1925.