Na Mwandisho Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Baraza la Michezo la Taifa (National Sports Council Sports Awards 2025) ambazo hutolewa ili kutambua mchango wanamichezo bora nchini mwaka huu zitatolewa Mei 9, 2026 katika ukumbi wa ‘The Super Dome Masaki’ uliopo Jijini Dar es Salaam ikiwa ni msimu wa nne mfululizo tangu zilipoanza kutolewa mwaka 2022.
Hayo yamesemwa leo Aprili 21, 2026 Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo za BMT Prof. Mkumbukwa Mtambo wakati akiongea na waandishi wa habari na kuongeza kuwa mwaka huu tuzo zimeongezeka kutoka makundi 20 hadi kufikia 21.
Prof. Mtambo amesema lengo la tuzo hizo ni kuendelea kuwatambua, kuwapongeza na kuwaenzi wanamichezo na timu za Kitanzania ambazo zimefanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa kwa mwaka 2025 kwani juhudi zao na mafanikio waliyoyapata yamesaidia kuipeperusha vyema bendera ya nchi kimataifa na kuliletea taifa heshima kubwa.
“Tuzo hizi zimekuwa na mafanikio makubwa kwa sababu zimeongeza ari za wanamichezo wetu na kuwafanya kuongeza juhudi kwenye mashindano ya kimataifa na kuufanya umma wa watanzania kutambua mafanikio yanayopatikana katika sekta ya Michezo pamoja na kuonesha mchango wa sekta ya michezo katika kukuza uchumi na kuleta mshikamano miongoni mwa watanzania”, amesisitiza Prof. Mtambo.
Kuhusu vigezo vya jumla vya wanamichezo wanaopendekezwa kupewa Tuzo, amevitaja kuwa ni; mwanamichezo wa kiume au wa kike raia wa Tanzania, awe amependekezwa na chama cha Michezo cha kitaifa kama miongoni mwa mwanamichezo bora katika mchezo wao.
Awe ameonesha ubora na kupata mafanikio mazuri katika mashindano ya kimataifa kwa mwaka 2025 na awe ametoa mchango mkubwa kwa mafanikio na matokeo mazuri ya timu yake katika mashindano ya kitaifa na kimataifa kwa mwaka 2025.
Prof. Mtambo amevitaja vipengele vya Tuzo za mwaka 2025 kuwa ni; mwanamichezo bora wa kiume na kike, mwanamichezo bora kijana wa kiume na kike, mwanamichezo bora wa kiume na kike mwenye ulemavu, timu bora ya taifa wanaume na wanawake, timu bora ya taifa (klabu) mwanamke na mwanaume, kocha bora wa kiume na wa kike, mwanamichezo bora wa kike na kiume kutoka shuleni.
Pia mwamuzi bora wa kiume na wa kike, mwanahabari za michezo bora wa kiume na wa kike, mwanamichezo nguli wa zamani ‘Sports Legend Award’, mwanahabari nguli wa michezo pamoja na tuzo ya mchezaji bora chaguo la watu “People’s Choice Award”.




