Leo tunaumaliza mwaka 2019 na kesho tutaingia mwaka 2020, ambao tunaamini utakuwa ni mwaka utakaotawaliwa na harakati za kisiasa, ikizingatiwa kuwa ni mwaka ambao Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu.

Kwanza, tuwatakie Watanzania wote heri ya mwaka 2020, tukiwaombea kwa Mungu wapate heri na baraka tele katika yote waliyopanga kuyafanya kama mtu mmoja mmoja na kama taifa kwa ujumla.

Lakini maombi kama haya hayapaswi kutufanya tubweteke, tukiamini kuwa Mungu atashusha baraka zake na sisi tutaneemeka. Ni lazima tuinuke kuzitafuta baraka hizo, kwani tukikaa kitako kamwe baraka hazitatufuata tulipo.

Katika muktadha huo huo, tungewasihi Watanzania kuhakikisha kuwa wanafanya kila lililo chini ya uwezo wao kuhakikisha kuwa nchi inavuka mwaka huu salama.

Hatuna shaka kuwa uchaguzi utakwenda vizuri, kwa sababu historia inaonyesha kuwa misuguano ya kisiasa haijawahi kuifanya nchi ikaingia kwenye misukosuko mikubwa. Lakini, mabadiliko ya miaka ya hivi karibuni yanaonyesha kuwa tusipozidisha uangalizi katika masuala ya siasa, tunaweza kujikuta tukiwa mahali ambapo hivi sasa tunawatolea mifano wenzetu.

Tunapoingia kwenye Uchaguzi Mkuu tunapaswa kufahamu kuwa amani ni muhimu na bora zaidi ya kitu chochote kile, yakiwamo madaraka ya kisiasa. Hili ni kwa sababu ukipata unachokihitaji huku amani ikiwa imevurugika, basi uwezekano wa kufaidi na kunufaika na hicho ulichokipata ni mdogo sana.

Tukumbuke kuwa uchaguzi huu utapita kama zilivyopita chaguzi nyingine huko nyuma. Hamu ya wanasiasa kukamata madaraka katika ngazi mbalimbali kamwe isizidi haki ya Watanzania kuwa na nchi yenye amani.

Ingawa Watanzania mbalimbali wanaunga mkono vyama vya siasa na harakati za siasa, lakini tukumbuke kuwa ni watu wachache sana ambao siasa inawaletea mkate wao wa kila siku moja kwa moja. 

Wengi wanaishi wakitegemea shughuli nyingine nyingi nje ya siasa. Hivyo basi, hatupaswi kutumia siasa kuvuruga na kuharibu shughuli nyingine ambazo zinawaletea ustawi mamilioni ya Watanzania na nchi yao.

Lakini haya yatawezekana pale kila mmoja atakapotimiza wajibu wake ipasavyo kulingana na jinsi sheria, kanuni na taratibu zinavyoelekeza. Wakati tukiwaasa wanasiasa kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na taratibu, pia tuwasihi wale waliopewa dhamana ya kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinafuatwa, kuhakikisha kuwa kunakuwa na uwanja sawa wa wanasiasa kuifanya kazi yao. 

Hilo litawarahisishia Watanzania kujua ni yupi anawafaa zaidi kuwa kiongozi wao, hivyo kuwa na kazi nyepesi watakapolikaribia sanduku la kura baadaye mwakani.

9679 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!