Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM

Mafuta mengi kwa sasa yanauzwa bila kulipiwa kodi zote za serikali baada ya kudaiwa kuingizwa kwa njia za panya katika mikoa iliyopo mipakani na maeneo mengine ya nchi.

Habari za uhakika kutoka kwa chanzo cha kuaminika (jina linahifadhiwa) kilichopo ndani ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) zinasema katika siku za hivi karibuni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilipata taarifa kuwa mafuta yanayokwenda nje ya nchi yanauzwa kwa wingi mkoani Kigoma.

Chanzo hicho kilichozungumza na Gazeti la JAMHURI hivi karibuni kimesema baada ya taarifa hiyo, Ewura ikachunguza, na kati ya vituo 30 vilivyokaguliwa, vituo 20 sawa na asilimia 66 ya mafuta yanayouzwa Kigoma yanalipiwa kodi na asilimia 34 sawa na vituo 10 hayajalipiwa kodi. 

Vilevile, kimesema hali hiyo imetokana na kiwango cha utekelezaji wa sheria kushuka kutoka asilimia 96 hadi 84 kabla ya Kampuni ya SICPA SA kuwa na mkataba na TBS wa uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta. 

“Hali hiyo inasababisha upotevu wa mapato ya serikali na lengo lake la kuanzisha mfumo huu halijatimia, maana vitendo vya ‘dumping’ ya petroli vimeongezeka,” kimesema chanzo hicho.

Zabuni ya uwekaji vinasaba yafutwa

Chanzo hicho kimesema kati ya Januari na Februari, 2022, wawakilishi wa Wizara ya Nishati, Wizara ya Viwanda, Ewura, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na TBS walifanya mapitio ya kanuni za uwekaji wa vinasaba (Petroleum Marking and Quality Control Regulations, 2022). 

Kimesema kanuni hiyo inaainisha namna mradi wa uwekaji wa vinasaba katika mafuta inavyotakiwa kufanyika, masharti yake, majukumu ya Ewura, taasisi itakayoviweka na namna ya kupanga gharama za uwekaji wake na wizara ikaitisha kikao cha mwisho cha wataalamu kilichofanyika Mei 26-28, 2022.

Pia kimesema Februari 7, 2022 kupitia barua yenye kumbukumbu namba EA.179/240/44/A/106, Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) ilimwandikia barua Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) ikimuelekeza kuratibu upatikanaji wa mzabuni wa mradi wa uwekaji vinasaba katika mafuta atakayefanya kazi na TBS.

Aidha, kimesema kuwa Februari 14, 2022 kupitia barua yenye kumbukumbu namba CBA.45/166/01, Wizara ya Nishati nayo ilimwandikia barua GPSA ikimuelekeza kuratibu upatikanaji wa mzabuni wa mradi huo wa uwekaji vinasaba katika mafuta.

Katika kutekeleza maelekezo hayo, kimesema GPSA iliandaa makubaliano kati yao, Ewura na TBS ili kupata ushauri wa kitaalamu katika kuandaa nyaraka za zabuni na kutoa ufafanuzi wa kitaalamu kutoka kwa wazabuni pale itakapohitajika na yakasainiwa na pande husika na utekelezaji ukaanza.

Katika hatua nyingine, kimesema Machi 22, 2022, GPSA ilitangaza zabuni ya uwekaji wa vinasaba kwa Tanzania Bara na ikaifungua Aprili 13, 2022 na kampuni tano ziliomba.

Kimetaja kampuni hizo na gharama zao katika mabano kuwa ni Global Fluids International-GFI (Dola 2.12 za Marekani kwa lita 1,000 za ujazo), Aunthentix (Sh 4,528.30 kwa lita 1,000 za ujazo), SICPA SA (Sh 7,056 kwa lita moja ya ujazo), Intertek Testing Services (E.A) PTY Ltd (Dola 1.80 za Marekani kwa lita 1,000 za ujazo) na Tracerco Limited (Sh 53,149,110).

Kimesema GPSA ikateua kamati ya tathmini kwa mujibu wa kifungu cha 40 (1), (2), (3), (4), (5), (6) na (7) iliyofanya kazi yake kuanzia Aprili 19 hadi 21, 2022 na kuwasilisha taarifa yake katika Bodi ya Zabuni kwa mujibu wa sheria.

Baada ya taratibu za ndani kukamilika, kimesema Mei 2, 2022, GPSA ilitoa notisi ya nia ya kutoa zabuni kwa GFI kwa mujibu wa kifungu cha 60(3) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410, aliyeonekana kukidhi vigezo vya kisheria na zabuni na wazabuni wengine walipewa taarifa hiyo.

Kimesema ilitarajiwa kwamba baada ya muda wa barua hiyo  Mei 10, 2022, GFI angepatiwa mkataba kwa ajili ya kutoa huduma ya uwekaji wa vinasaba katika mafuta huku Bara, lakini Mei 14, 2022, GPSA ilitoa tangazo la kufuta zabuni husika kwa mujibu wa kanuni ya 16(2)(d) na (5) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma, 2013. 

“Tangazo la kufuta zabuni husika lilieleza kuwa zabuni imefutwa kutokana na changamoto walizokutana nazo wakati wa zabuni hiyo kwa mujibu wa kanuni 16(2)(d),” kimesema.

Baada ya tangazo la GPSA la kufuta zabuni husika, kimesema ilibainika kulikuwa na barua ya maelekezo kutoka kwa kiongozi mwandamizi serikalini (jina linahifadhiwa) kwenda PPRA na GPSA, ikielekeza kusimamisha mchakato wa zabuni na kuielekeza TBS kuongeza muda wa mkataba wake na SICPA SA kwa kipindi cha miezi sita ikiwa na bei iliyopunguzwa. 

Pia kimesema kiongozi huyo alielekeza majadiliano yafanyike ili bei itakayotumika katika mkataba iwe ya fedha za Tanzania na katika barua hiyo nakala zilipelekwa TBS, Wizara ya Nishati na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara lakini Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) haikupewa nakala ya barua.

Mbali na hayo, kimesema kanuni ya 16(2)(d) na (5) iliyotumika katika tangazo la kufuta zabuni inahusu kukataa zabuni na si kufuta. 

Kimesema kanuni ya 16(5) iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 na kwa sasa inasomeka kama kanuni 16(3) kwamba endapo GPSA ilimaanisha kukataa zabuni ilipaswa iridhie sababu za kusitisha mchakato kama ilivyoainishwa kwenye kanuni ya 16(1) na kufuta mchakato wa zabuni unatakiwa kufanyika baada ya kuomba ridhaa na kukubaliwa na PPRA kwa mujibu wa kifungu cha 19(1)(a) na (b),(2) na (3) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410. 

“Suala hili halikufanyika kama inavyotakiwa kisheria kwa kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ndiye mshauri mkuu wa masuala ya kisheria katika serikali hakushirikishwa katika mchakato wa kufuta zabuni ya uwekaji wa vinasaba.

“Kwa mazingira haya, kitendo cha kutomshirikisha AG kitaleta changamoto katika kuishauri na kuiwakilisha serikali mahakamani endapo suala hili litafikishwa huko,” kimesema.

Aidha, kimesema taarifa ya kufuta mchakato wa zabuni ilitolewa nje ya muda wa siku saba baada ya notisi ya nia ya kutoa zabuni kutolewa Mei 2, 2022 kwa mujibu wa kanuni ya 16(2)(d) na (3) kama ilivyorejewa mwaka 2016 na bila kukidhi sababu zilizoainishwa katika vifungu vya 4A(2) na 59 vya Sheria ya Ununuzi ya Umma, Sura 410. 

Kimesema kifungu cha 59(2)(e) cha sheria kinaafiki kukataa zabuni endapo mkataba ukitolewa hautaweza kutekelezwa. 

Vilevile kifungu cha 59(1), (2),(3)(4) na (5) cha sheria kimetoa sababu za kukataa au kusitisha zabuni na kifungu cha 19(1)(2) na (3) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410 kinachohusu kufutwa kwa mchakato wa zabuni kinahitaji kufanyiwa uchunguzi na PPRA na wazabuni wote watakaoathirika na uamuzi wanatakiwa kupewa nafasi ya kujieleza.

Kasoro za mkataba kati ya TBS, SICPA SA

Pamoja na mambo mengine, chanzo hicho kimesema utekelezaji wa mkataba wa muda kati ya TBS na SICPA SA una kasoro nyingi.

Kimesema kasoro hizo zimesababisha TBS kushindwa kutekeleza hadidu za rejea na ikiwamo kumsimamia SICPA SA kutekeleza mkataba ili kuboresha huduma kwa serikali. 

Kimetaja kasoro zilizopo katika utekelezaji wa mkataba wa sasa kuwa SICPA SA imeshindwa kuwasilisha vifaa tisa vya kutambua ubora wa mafuta kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma na imeshindwa kuanzisha vituo sita vya upimaji wa hiyari vilivyoainishwa katika hadidu za rejea ili kuwapa fursa watumiaji kupima kiwango cha vinasaba kama vimewekwa kwa usahihi.

Kasoro nyingine kimetaja kuwa ni SICPA SA kushindwa kuweka mfumo wa kisasa wa kuweka vinasaba katika mafuta ili kupunguza makosa ya kibinadamu, kushindwa kuweka mfumo wa Tehama utakaotoa taarifa halisi za matumizi ya mafuta hayo yanayowekwa kila sekunde na kusababisha serikali na vyombo vyake kukosa taarifa sahihi ya huduma hiyo.

Pia kimesema SICPA SA imeshindwa kuweka kamera za usalama za CCTV katika maghala ya mafuta na maeneo ya kuhifadhi vinasaba, hivyo kuathiri usalama wake.

TBS yajibu

Juni 17, 2022, JAMHURI limefanya mahojiano na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Athuman Ngenya, kuhusu kasoro za utendaji wa SICPA SA na wao kukiuka hadidu za rejea za makubaliano lakini amesema wanaotakiwa kutoa majibu ya zabuni hiyo ni serikali, kwa sababu ndio waliosimamisha mchakato wote.

“Kwa sasa kampuni iliyopo ni ile ile SICPA SA iliyokuwapo awali na inaendelea kutuuzia vinasaba kwa mkataba na serikali ndiyo yenye jukumu hilo la kujibu,” amesema Dk. Ngenya.

Pia Juni 17, 2022, Ofisa wa SICPA SA, Marwa Mwita, ameliambia JAMHURI kwa kifupi kwamba mambo yote kuhusiana na mkataba wao wa kazi ya kuweka vinasaba katika mafuta waulizwe TBS, si wao.

By Jamhuri