DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Hali ya hoteli ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano inayomilikiwa na Serikali ya Libya, Bahari Beach Ledger Plaza, ni mbaya kiasi cha kuibua migogoro ya mara kwa mara kati ya uongozi na wafanyakazi.

JAMHURI linafahamu kwamba kwa miezi mitano sasa wafanyakazi, hasa wasimamizi wa idara, hawajalipwa mishahara huku wafanyakazi wa kawaida wenye mishahara midogo wakilipwa kwa kusuasua.

Na sasa wafanyakazi wanamtaka Meneja Mkuu wa Hoteli, Wisam Najem, kuwalipa stahiki zao zote au kuifunga.

“Tunanyanyasika bila sababu, meneja anatuambia halipi mishahara kwa kuwa hana fedha, lakini tunajiuliza, kama hali ni mbaya kiasi hicho, kwa nini hataki kuifunga?” amehoji mmoja wa wafanyakazi, akisema Najem anaishi maisha ya kifahari Masaki wakati wao wakishindwa hata kulipa kodi za nyumba wanakoishi na ada za shule za watoto.

Najem ameletwa nchini mwaka 2020 na Kampuni ya Libyan African Investment (LAICO) kuwa msimamizi baada ya kuondolewa kwa hila uongozi wa awali ukidaiwa kuvamia na kujimilikisha hoteli kinyemela.

Mtoa taarifa wetu anadai kuwapo udanganyifu wa fedha za mapato na kwamba meneja huzitumia kwa manufaa binafsi.

“Tunafanya kazi katika mazingira magumu. Haki zetu hazizingatiwi, michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii haipelekwi.

“Mikataba ya kazi ikiisha tunaondolewa bila kupewa mipya wala nafasi ya kujieleza,” amesema mfanyakazi mwingine ambaye mkataba wake unakaribia ukingoni.

Watumishi zaidi ya 60 tayari wamekwisha kufukuzwa kazi tangu Najem aingie madarakani mwaka 2020, hali inayosababisha ugumu wa kazi kwa watumishi takriban 30 tu waliosalia.

“Ni kweli biashara ya hoteli inapita kipindi kigumu kwa sasa, lakini kwa nini Najem atunyanyase kwa kigezo kwamba hoteli si ya Watanzania?” amehoji.

Siku za nyuma, Bahari Beach Ledger Plaza, mali ya Serikali ya Libya, ilikuwa ikifanya vizuri migogoro iliyopo imesababisha uchakavu wa kutisha na mdororo wa biashara.

Kwa sasa inakumbwa na upungufu wa vitanda, viti, majokofu ya kuhifadhi vyakula na mashine za kufulia na kukausha nguo.

Pia ina miundombinu mibovu ya wateja kufanyia mazoezi, baadhi ya vitanda vimevunjika na vingine kuongezewa mbao kuvishukilia visiporomoke.

“Kuna matumizi mabaya ya fedha zinazopatikana. Badala ya kutumika kuboresha uwekezaji, zinatumika kwa masuala binafsi ya watu,” amesema mtumishi mwingine wa hoteli hiyo.

Amesema ili hoteli irudi kwenye ubora wake kama ilivyokuwa zamani, inatakiwa ifanyiwe ukarabati mkubwa pamoja na utawala kubadilishwa.

“Ni shida. Februari mwaka huu tulikumbwa na uhaba wa mashuka. Tukamweleza meneja; akasema hakuna fedha. Baadaye akaenda Kenya, akaleta mashuka yaliyokuwa yakitumika huko ili tuyatumie hapa! Hili halikuwa sahihi,” amesema.

Mfanyakazi huyo ana hofu kwamba huenda hoteli inaendeshwa bila kuwa na bodi ya wakurugenzi inayotambulika nchini.

Akizungumza na JAMHURI, Meneja Mkuu wa Hoteli, Najem, ameonyesha kukasirishwa na kuvuja kwa taarifa za kuporomoka kwa ubora wa Bahari Beach Hoteli.

“Kama waliokupa taarifa ni wafanyakazi wa hapa, nitajie majina au unionyeshe vitambulisho vyao. Kama huwezi kuwataja, siko tayari kujibu chochote utakachoniuliza,” amesema kwa kufoka Najem.

Pasipo kutoa ufafanuzi wa kina wa maswali aliyofikishiwa mezani kuhusu tuhuma za kufuja fedha na hali ya hoteli kuwa mbaya, Najem ameyakanusha malalamiko ya wafanyakazi kutolipwa mishahara, akidai hulipwa kwa wakati.

Bahari Beach Ledger Plaza ni hoteli kongwe na kubwa iliyopo ufukweni mwa Bahari ya Hindi, ambayo awali ilisifika kwa kutoa huduma bora, zenye hadhi ya nyota tano.

Please follow and like us:
Pin Share