DAR ES SALAAM

Na Andrew Peter

Pamoja na ukame wa mabao na kusota benchi katika klabu zao washambuliaji Mbwana Samatta na Simon Msuva bado wanabeba matumaini ya Taifa Stars dhidi ya Niger katika kusaka kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika 2023 nchini Ivory Coast.

Taifa Stars imepangwa Kundi F pamoja na Uganda, Algeria na Niger. Itaanza kampeni ya kusaka kufuzu kwa fainali hizo ugenini Juni 4 dhidi ya Niger kwenye Uwanja wa L’Amitie jijini Cotonou, Benin na siku nne baadaye Juni 8, itarejea Dar es Salaam kuivaa Algeria kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Stars inakwenda katika michezo hiyo miwili ya mwanzo huku safu yake ya ushambuliaji ikiwa na pigo kutokana na washambuliaji wake nyota wawili; Samatta na Msuva, wamekuwa na wakati mgumu katika klabu zao msimu huu.

Wawili hao ndio vinara wa ufungaji mabao kwa Taifa Stars, wakiwa wamefunga jumla ya mabao 37, kwa pamoja huku

Samatta akiwa amefunga mabao 20 na Msuva (17) hadi sasa, huku Mrisho Ngassa akishikiria rekodi ya kuwa kinara wa ufungaji wa muda wote wa Stars kwa mabao yake 25.

Pamoja na rekodi hiyo, mshambuliaji wa Royal Antwerp FC, Samatta ‘Samagoal’, amekuwa na wakati mgumu msimu huu akicheza mechi 32, sawa na dakika 1,437, akifunga mabao matano tu katika Ligi Kuu ya Ubelgiji.

Wakati hali ya ‘Samagoal’ ikiwa hivyo, pacha wake, Msuva, maisha yake ndani ya Klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco hayakuwa mazuri kabisa, akicheza dakika 44 tu msimu mzima na kufunga bao moja katika mchezo wa kirafiki.

Hali hiyo ilimfanya Msuva kukimbia Morocco na kurejea nyumbani. Muda mwingi amekuwa akifanya mazoezi peke

Yake, jambo lililozua maneno alipojumuishwa katika kikosi hiki cha Stars kwa ajili ya mechi hizi mbili.

Hata hivyo, taarifa za hivi karibuni zinasema Msuva amejiunga na Klabu ya FK Auda inayoshiriki Ligi Kuu nchini Latvia, barani Ulaya atakayoitumikia kuanzia msimu ujao.

Samatta na Msuva pamoja na upungufu wao katika klabu zao msimu huu, bado ndio wamebeba matumaini ya Watanzania katika kuiona Stars inapata matokeo mazuri katika mechi yake dhidi ya Niger.

Katika michezo miwili ya kirafiki ya Taifa Stars iliyochezwa Machi dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Samatta alifunga

bao moja katika ushindi wa 3-1 huku magoli mengine yakifungwa na kiungo chipukizi, Novatus Dismas, wa Klabu

ya Beitar Tel Aviv Bat Yam ya Israel na nyota wa Geita Gold, Geogre Mpole, wakati Msuva yeye alifunga katika

mchezo uliomalizika kwa sare 1-1 dhidi ya Sudan.

Kinara wa ufungaji wa Ligi Kuu, mshambuliaji wa Geita Gold, Mpole, mwenye mabao 14 katika ligi, alifunga bao lake la kwanza Stars akiingia akitokea benchi katika ushindi 3-1 dhidi ya Jamhuri ya Afrika Kati katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliochezwa Machi, lakini kukosa kwake uzoefu hakuna shaka kwamba Kocha, Kim Poulsen, ataanza na Samagoal na Msuva katika mchezo huo wa ugenini.

Naye mshambuliaji chipukizi, Kelvin John, wa KRC Genk bado hajaweza kuchukua mikoba ya Samatta kwa kuhamishia makali yake yale ya Serengeti Boys kwa Taifa Stars.

Kocha Kim atalazimika kumpa nafasi Kelvin ili kuendelea kumjenga chipukizi huyo kuja kurithi mikoba ya Samatta 

siku za usoni.

Kiungo mkongwe, Himid Mao, wa Klabu ya Grazi El Mahalla ya Misri amerejea katika kikosi cha Stars. Katika mechi hii atakuwa na jukumu moja kubwa la kuimarisha safu ya ulinzi pamoja na chipukizi Novatus wakiwa viungo wakabaji.

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kukutana na Niger katika mashindano haya, hivyo kunategemewa kuwa na ushindani mkubwa.

Kocha Poulsen amesema katika kundi letu Niger haifahamu, ila Uganda na Algeria anazifahamu vizuri kwa sababu tulikwisha kucheza nazo huko nyuma.

“Naamini timu zote zimejiandaa vizuri, na sisi tunapaswa kujipanga kwa kujiandaa vizuri kuhakikisha tunazitumia vizuri mechi hizi mbili za awali,” amesema Kim na kuongeza kwamba kwa mujibu wa viwango vya Fifa sisi ni wa mwisho, tukifuatiwa na Niger, Uganda na Algeria. Kwa hiyo tunategemea ushindani mkubwa kutoka kwa wapinzani wetu.

“Katika makundi timu zote zilizokuwa juu kwa viwango vya Fifa ndizo zinazopewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi

moja kati ya mbili, tunajua hilo,” amesema Mdenmark huyo na kusisitiza: “Hakuna ubishi, lengo letu ni moja, kuhakikisha tunafuzu kwa AFCON 2023. Ni matumaini yangu kwamba tutapata moja ya nafasi mbili.”

Tanzania inasaka kufuzu kwa mara ya tatu kwa fainali za Afrika baada ya kufanya hivyo mwaka 1980 nchini Nigeria

na 2019 nchini Misri.

By Jamhuri