Bao la Fei Toto lafufua rekodi Yanga

Dar es Salaam

Na Andrew Peter

Bao la shuti la umbali wa mita 25 la kiungo Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ limefufua ndoto ya Yanga ya kusaka rekodi kuwa timu ya kwanza kutwaa mataji mawili; Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi Kuu Tanzania Bara bila kufungwa.

Fei Toto alifunga bao pekee kutokana na pasi ya Khalid Aucho akiwa katikati ya uwanja na kukokota mpira kwa kasi kabla ya kupiga shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni na kumwacha kipa wa Simba, Beno Kakolanya, akiruka bila mafanikio; bao lililodumu hadi mwisho wa mchezo.

Ushindi wa Yanga unawafanya Yanga kuwa katika nafasi nzuri ya kuweka rekodi ya kutofungwa hata mchezo mmoja kwenye mashindano mawili makubwa kwa klabu nchini, hivyo kuivunja rekodi iliyowekwa na Simba msimu wa 2009/10, na Azam (2012/13); ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu bila kufungwa.

Pia ushindi huo uliopatikana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika mchezo wa nusu fainali ya ASFC ni mwendelezo wa ushindi wa Yanga mkoani Mwanza. 

Yanga wameshinda mechi ya tano miongoni mwa saba walizocheza dhidi ya Simba mkoani Mwanza tangu walipocheza kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Nyamagana mwaka 1974.

Tangu mwanzo wa msimu huu vijana wa Jangwani walidhamiria kumaliza ufalme wa miaka minne wa Simba kwa kuanza na Ngao ya Jamii na sasa wamewavua ubingwa wa ASFC,  huku wakihitaji pointi tatu tu kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Mara ya mwisho Yanga kutwaa mataji yote mawili ndani ya msimu mmoja ilikuwa ni msimu wa 2016, na wakishinda fainali ya ASFC, watarejea rekodi hiyo; na wakishinda mchezo mmoja tu miongoni mwa mitano iliyobaki ligi itakaporejea baada ya mapumziko kupisha michezo ya kimataifa, watatawazwa kuwa mabingwa.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Simba, Kocha Mohamed Nabi wa Yanga alikataa kutangaza ubingwa sasa akisema bado wana mechi ngumu mbele.

“Ubingwa bado, tunahitaji kushinda mechi zetu zilizobaki, ila kwa sasa mashabiki wetu wafurahi kwa ushindi huu dhidi ya Simba na kufuzu kwa fainali,” amesema Nabi.

Katika mchezo huo Nabi akiwa kwenye benchi tofauti na mechi iliyopita ya Ligi Kuu alikuwa akitumikia adhabu, Mtunisia huyo aliamua kuanza na washambuliaji wawili – Harriet Makambo na Fiston Mayele, mbinu iliyofanikiwa kwa Yanga. 

Mbali ya kuanza na washambuliaji wawili, pia hakuwachezesha wale mawinga wake katika mfumo wake 3-5-2 huku mpinzani wake Pablo Martin wa Simba akitumia 4-3-3, jambo lililofanya Yanga kuwa na viungo wengi katikati ya uwanja.

Kipigo hicho cha Simba kinafanya siku za Mhispania Pablo ndani ya Simba kuanza kuhesabika baada ya kushindwa kufikia malengo yake aliyopewa ya kuiwezesha timu hiyo kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa au Kombe la Shirikisho Afrika na sasa amepoteza ubingwa wa Kombe la ASFC pamoja na Ligi Kuu.

Matokeo ya Mwanza: Yanga vs Simba 

AGOSTI 10, 1974: Yanga 2-1 Simba (Kombe la Hedex)

JUNI 30, 1996: Yanga 2-0 Simba 

SEPTEMBA 30, 2001: Simba 1-1 Yanga

APRILI 20, 2003: Yanga 3-0 Simba 

JULAI 2, 2005: Simba 2-0 Yanga

OKTOBA 16, 2010: Yanga 1-0 Simba

MEI 28, 2022: Yanga 1-0 Simba