Na Nizar K Visram

Shireen Abu Aqleh alikuwa mwanahabari wa Kipalestina aliyeajiriwa na Shirika la Utangazaji la Al Jazeera hadi Mei 11, 2022 alipopigwa risasi na kuuawa na wanajeshi wa Israel. 

Aliuawa akiwa kazini akiripoti habari za wanajeshi hao kuvamia kambi ya Wapalestina iliyopo Jenin nchini Palestina.

Baada ya kumpiga risasi Shireen, waliendelea kuwalenga wanahabari wenzake waliojaribu kumsaidia. Ali al Samoudi, mwandishi wa Gazeti la al Quds naye alipigwa risasi mgongoni na akajeruhiwa. Mwandishi mwingine, Shatha Hanaysha, alikoswa mara kadhaa.

Asasi ya Kipalestina ya kutetea haki za binadamu, Al-Haq ilifanya uchunguzi kwa kuwahoji mashahidi na kuangalia ripoti ya madaktari. Ikaamua kuwa Shireen aliuawa kwa risasi iliyofyatuliwa na askari wa Israel. Risasi hiyo iliingia kichwani ingawa alikuwa amevaa kofia ngumu na kizibao kilichoandikwa ‘Press’ ili kumtambulisha kuwa yeye ni mwanahabari. 

Al-Haq iligundua kuwa askari wa Israel waliwalenga wanahabari hao makusudi na risasi iliyomuua Shireen ni ile inayotumiwa na askari wa Israel.  

Ali Samoudi akiwa amelazwa hospitalini alisema askari wa Israel walimlenga yeye na wenzake makusudi, wala haikuwa bahati mbaya. 

Akaongeza: “Tulijitayarisha kuwapiga picha askari hao ambao ghafla walitufyatulia risasi.”   

Maneno ya Samoudi yaliungwa mkono na mwandishi mwingine, Shatha Hanaysha, aliyesema walikuwa waandishi wanne na wote walivaa vizibao vya waandishi pamoja na kofia ngumu. Huku akibubujikwa machozi, Hanaysha alisema baada ya Shireen kuanguka alijaribu kumsaidia lakini alishindwa kwa vile Waisraeli waliendelea kufyatua risasi. 

Si tu Shireen aliuawa na askari wa Israel, bali hata mazishi yake waliyashambulia. Mazishi hayo yalihudhuriwa na maelfu ya Wapalestina waliosindikiza jeneza kupitia miji ya Jenin, Nablus na Ramallah hadi Jerusalem kwenye makaburi ya Wakatoliki maeneo ya Mlima wa Zion. 

Halaiki ya Wapalestina wa Kiislamu na Kikristo walimiminika Jerusalem kumzika Shireen. Inasemekana hata mazishi ya Rais Yassir Arafat mwaka 2004 hayakuhudhuriwa na halaiki kama hiyo. 

Waombolezaji hao walipigwa marungu na askari. Waliobeba jeneza walipigwa hadi jeneza almanusra lidondoke. Wakawanyang’anya bendera ya Palestina huku wakiwapiga. 

Waombolezaji waliokusanyika nyumbani kwa Shireen, Jerusalem mashariki, nao walishambuliwa na askari wa Israel. Waliwataka kuacha kuimba nyimbo za kizalendo na kuteremsha bendera ya Palestina.  

Kama kawaida, Israel ilikanusha kuwa askari wake walimuua Shireen, wakidai kuwa aliuawa na Wapalestina.   

Haya yalisemwa na Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa Israel, wizara yake ya mambo ya nje na balozi wake nchini Marekani. Wakaeneza video katika mtandao ikionyesha Mpalestina akimfyatulia risasi askari wa Israel. 

Lakini asasi ya kutetea haki za binadamu iliyopo Israel, B’Tselem, ilichunguza video hiyo na kugundua kuwa wakati Shireen anapigwa risasi mahali hapo hapakuwa na Wapalestina ila tu askari wa Israel waliokuwa wakipiga risasi. Wakagundua pia video iliyosambazwa na Israel imepigwa mahali ambako ni mbali na alipouawa Shireen.

Mwanahabari wa Shirika la Agence France-Presse aliyeshuhudia mauaji ya Shireen naye alikubaliana na B’Tselem. Shahidi mwingine ni Lina Alsaafin, mwandishi wa Al Jazeera (Kiingereza) ambaye alisema video inaonyesha waziwazi kuwa askari wa Israel waliwalenga wenzake Shireen waliojaribu kumsaidia. Hii inaonyesha kuwa Shireen na wenzake walikuwa wakilengwa na askari hao. 

Mashirika mawili ya utangazaji nchini Marekani yamefanya uchunguzi wao na wakathibitisha kuwa Shireen aliuawa na Israel kwa kukusudia. Shirika la CNN lilisikiliza ushahidi kutoka kwa mashahidi wanane pamoja na wataalamu wa silaha, kisha wakaamua kuwa ni askari wa Israel ndio waliomuua Shireen. Associated Press nayo ilisema kuwa risasi iliyomuua Shireen imetokana na silaha ya Israel. 

Kwa hiyo mashirika haya yamekubaliana na taarifa iliyotolewa na mamlaka ya Palestina (PA) na ushahidi wa wenzake Shireen. Mamlaka hiyo tayari imesema inatayarisha ripoti ya uchunguzi ambayo wataifikisha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC). 

Israel mwanzoni ilisema Shireen aliuawa na Wapalestina wenzake. Baada ya kuthibitika kuwa huo ni uongo, wakasema uchunguzi ufanywe ili kuthibitisha nani aliyemuua. 

Ni vizuri kujiuliza ni nani atakayechunguza na baada ya hapo ni hatua gani zitakazochukuliwa. Mamlaka ya Palestina imesema haina imani na uchunguzi utakaofanywa na Israel kwa sababu: “Mhalifu hawezi kujichunguza.” Badala yake mamlaka hiyo inataka uchunguzi ufanywe na ICC.

Msomi wa Kipalestinaa nchini Marekani, Profesa Rashid Khalid, amesema kama mwanahabari wa Kimarekani angeuawa na askari wa Urusi nchini Ukraine, tungesikia nchi za Magharibi zikipiga mayowe. Lakini mwandishi Mpalestina anauawa na askari wa Israel na hatusikii hatua zikichukuliwa dhidi ya Israel.

Ingawa Mpalestina huyo ni raia pacha wa Marekani, bado Marekani inanyamaza kimya na inaendelea kuipa Israel misaada ya kijeshi ya dola bilioni 3.5 kila mwaka. Profesa Khalid anakumbusha kuwa huyu ni Mpalestina-Mmarekani wa pili kuuawa na Israel katika muda wa miezi mitatu, na hakuna uchunguzi.

Kuuawa kwa Shireen halikuwa tukio la pekee, kwani katika Palestina inayokaliwa na Israel wanahabari wengi wamewahi kuuawa kwa sababu tu wamekuwa wakitumia weledi wao kuueleza ulimwengu kinachotokea katika maeneo hayo.

Asasi ya kimataifa ya wanahabari (Reporters Without Borders) imesema tangu mwaka 2018 wanahabari wasiopungua 144 wameshambuliwa na kujeruhiwa na askari wa Israel. 

Mwaka 2018/19 wanahabari wawili waliuawa; nao ni Yasser Murtaja na Ahmed Abu Hussein. Walikuwa wakichukua filamu ya maandamano katika Ukanda wa Gaza. Aidha, mashambulizi ya angani yalilenga nyumba alimokuwa mwandishi Yousif Abu Hussein aliyekuwa mtangazaji wa Redio ya Al-Aqsa.

Novemba 2018 askari wa Israel walimpiga risasi na kumjeruhi mwandishi wa AP, Rashed Rashid, aliyekuwa amesimama mita 600 kutoka kwenye maandamano ya Ghaza akiwa amevaa mavazi ya waandishi wa habari.

Mwaka jana polisi wa Israel walimkamata mwandishi wa Al Jazeera, Givara Budeiri, na wakamvunja mkono, alipokuwa anafuatilia maandamano ya Jerusalem. 

Na Chama cha Wanahabari wa Kipalestina (Palestinian Journalists Syndicate), kinasema kati ya mwaka 2000 na 2020 waandishi zaidi ya 46 wameuawa. Aidha, kikaongeza kuwa Aprili mwaka huu kumekuwako na matukio 57 ya Israel kuwadhalilisha waandishi.

Chama hiki kikishirikiana na wenzao wa kimataifa (International Federation of Journalists na International Center for Justice for Palestinians) wameamua kuifikisha Israel katika Mahakama ya Kimataifa (International Court of Justice).

Waandishi wengine wengi wamefungwa gerezani bila ya kufikishwa mahakamani, akiwamo Bushra al-Tawil.

Mwaka jana majeshi ya Israel yalishambulia Gaza kwa makombora kwa muda wa siku 11. Wakabomoa jengo la ghorofa 12 ambamo mlikuwamo ofisi za Associated Press na Al Jazeera. Israel ilidai eti jengo hilo lilikuwa likitumiwa na wapiganaji wa Hamas, ingawa hawakutoa ushahidi. Katika mashambulizi haya waliwaua Wapalestina 260, wakiwamo watoto 66.

Mtawala wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani ameutaka Umoja wa Mataifa (UN) uchukue hatua thabiti kumaliza suala la Palestina sawa na wanavyofanya katika vita ya Ukraine. Alisema tangu kuundwa kwa UN Wapalestina wameporwa ardhi yao lakini hakuna hatua inayochukuliwa.    

Mfalme huyo akasema wanahabari saba waliouawa Ukraine wanapewa umuhimu wakati tunasahau kuuawa kwa Shireen pamoja na waandishi wengine 18 waliouawa nchini Palestina tangu mwaka 2000 na wengine waliouawa huko Iraq, Syria na Yemen.

Naye kiongozi wa Palestina Dk. Hanan Ashrawi alisema askari wa Israel kuwashambulia waombolezaji waliobeba jeneza la Shireen, bendera na mabango ya Palestina ni ishara kuwa “wakoloni wa Israel wameingiwa woga na wasiwasi mkubwa.” 

Nchini Marekani mjumbe wa Baraza la Seneti, Bernie Sanders, alilaani mauaji ya Shireen na mashambulizi ya waombolezaji. Akasema ni lazima Marekani iilaani Israel na kutaka uchunguzi ufanyike.

Na mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Bi Rashida Tlaib, alisema mauaji haya ni kazi ya ukaburu wa Israel dhidi ya Wapalestina. Akasema yanahuzunisha hasa kwa vile yanawezeshwa na msaada wa kijeshi wa dola bilioni 3.8 unaotolewa na Marekani kwa Israel bila ya masharti.  

Wengine walioilaani Israel ni wawakilishi Ro Khanna na Ilhan Omar ambao walitaka uchunguzi huru ufanyike.

Wawakilishi André Carson na Lou Correa wameandika barua kwa Serikali yao ya Marekani wakitaka uchunguzi ufanywe na Shirika la uchunguzi la FBI kwa vile Shireen ni raia wa Marekani na ana haki ya kulindwa na Serikali ya Marekani. Barua hiyo imezungushwa kwa wawakilishi wengine ili waisaini.

Wabunge wengine walilaani mauaji bila ya kutaja Israel kama inahusika. Na wengine walikaa kimya bila ya kusema chochote. Wachambuzi wanasema hiyo ndiyo tofauti ya mauaji ya Wapalestina na yale ya Ukraine. 

Habari za hivi karibuni zinasema Mamlaka ya Palestina imetayarisha mashtaka na kuyafikisha ICC. Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina, Dak Riyad al-Maliki, amesema kesi hiyo amekabidhiwa mwendesha mashtaka wa ICC, pamoja na mashtaka mengine yaliyowasilishwa mapema. 

Hata hivyo, Dak Mustafa Barghouti, mwanaharakati wa Palestina anasema ICC ni ndumila kuwili kuhusu suala la Palestina. Anasema: “Palestina imekuwa ikiwasilisha kesi katika mahakama hiyo kwa muda wa miaka 13 lakini hakuna uchunguzi uliofanyika. Kwa upande wa pili huko Ukraine haikuchukua hata miezi miwili tayari ICC imetuma huko watafiti 42. Huu ni unafiki.”

[email protected]

+1 343 204 8996

By Jamhuri