MOROGORO

Na Everest Mnyele

Tuzo ya Mo Ibrahim ilianzishwa mwaka 2007 na bilionea wa Sudan, Mohamed ‘Mo’ Ibrahim, kupitia taasisi yake kwa madhumuni ya kuwatuza viongozi wa Afrika, hasa marais na wakuu wa serikali walioonyesha uongozi uliotukuka katika nchi zao. 

Hadi sasa tuzo hiyo ya dola za Marekani milioni 5 imetolewa kwa marais saba tu; Joachim Chisano wa Msumbiji, Festus Mogae wa Botwana, Patros wa Cabo Verde, Pohamba wa Namibia, Ellen Johnson wa Liberia, Mahamadou Issiofou wa Niger na Nelson Mandela aliyepewa tuzo za heshima. 

Hawa walipewa tuzo kutokana na waliyoyafanya kwa wananchi wao kuanzia utawala bora mpaka maendeleo endelevu katika nchi husika; yaani uongozi uliotukuka.
Tuzo hii yenye thamani kubwa kuishinda ile ya Nobel yenye thamani ya dola milioni 1.5 tu, ilianzishwa kwa malengo ya kuhamasisha uongozi uliotukuka Afrika, bara lenye migogoro mingi ya uongozi. 

Marais wanahamasishwa kufanya vema katika nyanja za utawala bora, utawala wa demokrasia, ukomo wa vipindi vya madaraka, kuheshimu utawala wa sheria na kuwaletea wananchi maendeleo endelevu. 

Haya ndiyo mambo makubwa yaliyoangaliwa ili kiongozi ashinde tuzo hii, tuzo ngumu kuipata kwa viongozi wa Afrika ndiyo maana kwa miaka 17, ni marais saba tu wameipata. 

Ili kuipata, kiongozi anapaswa kuwa na nia ya kweli kutoka moyoni ya kutaka kuleta mabadiliko chanya nchini mwake. Si kuzungumza tu, bali aonekane ana dhamira ya dhati ya kuleta mageuzi.
Tanzania imejaliwa amani, hivyo si ngumu sana kwa kiongozi wa nchi kuleta mageuzi ya utawala bora, demokrasia, maendeleo endelevu na utawala wa sheria. 

Cha msingi ni kujiwekea malengo kwa kuangalia kinachokwamisha utawala bora, je, ni rushwa? Ni uvunjaji wa haki au kukosa uwazi katika utendaji serikalini?

Kwenye demokrasia ni kuangalia misingi gani iliyo sahihi, mfano uchaguzi huru au tume huru ya uchaguzi.

Katika maendeleo endelevu; je, pato la mtu mmoja mmoja linaongezeka? Watu wanapata huduma za kijamii? Wanazifurahia na kuzipenda ili wawe wenye furaha ya kweli?
Haya ni baadhi ya mambo ya kujipima. Kuyafikia haya, kiongozi anapaswa kuzungukwa na wasaidizi wenye uwezo, wanaotambua dhamira na umuhimu wa dhamana waliyopewa na wananchi. 

Pia kunapaswa kuwapo uongozi wa pamoja wa kuleta mabadiliko chanya. Hii si kazi ya lelemama.

Ninamheshimu sana Profesa Ibrahim Lipumba kwani ni mmoja wa wachumi wabobezi nchini. Nilimsikia akizungumza kwa sauti ya chini lakini ya uhakika wakati Rais alipokuwa Tabora.
Tusidanganyane, Profesa Lipumba hajaibuka tu. Lazima ameona dalili zinazoweza kumfanya Rais Samia kushinda tuzo hii. 

Ninaungana na Prof. Lipumba kwani baada ya Samia kuingia madarakani tu, katika hotuba yake ya kwanza alitoboa kuonyesha kuwa mambo hayakuwa sawa, akasema wazi kuwa tunahitaji maridhiano ili tuijenge nchi yetu. 

Akashughulikia corona, uhusiano wa kimataifa na baadaye akaanzisha mjadala wa maridhiano ya kisiasa. Nadhani haya ni baadhi ya aliyoyaona Prof. Lipumba, akaona umuhimu wa kuisukuma ajenda ya tuzo ya Mo Ibrahim. Nyota njema huonekana asubuhi.
Dola milioni 5 si haba. Ni vema tukaungana na Lipumba kuanzisha kampeni kumfanya Mama Samia kuibuka kidedea kama ilivyokuwa kwa Rais Ellen Johnson wa Liberia. 

Hatulazimishi, bali tunaiona dhamira ya dhati ya Mama Samia kwenye mageuzi chanya ya demokrasia, utawala bora, utawala wa sheria na maendeleo endelevu. 

Kauli yake ya mara kwa mara kuwa ‘nchi hii ni yetu sote, tushirikiane kuijenga’, ni nzito kutoka kwa kiongozi wa nchi. Ninaamini anaisema kutoka moyoni na anaifanyia kazi.
Ndugu zangu tusidanganyane, wanaoweza kusababisha Rais Samia kupata tuzo hii ni viongozi na watumishi wa umma ambao ndio wanaotekeleza mipango na malengo ya serikali. 

Kwa upande wake ameanza vema. Amewapandisha madaraja na mishahara kwa kiasi ambacho hakijawahi kutokea. Amerekebisha kikokotoo kwa wastaafu.

Watumishi mfahamu kwamba Rais anawajali, hivyo ni wajibu wenu kufanya kazi na kutoa huduma ili kukidhi matamanio ya wananchi. 

Kuhusu utawala bora, ni viongozi na watumishi ndio wanapaswa kutekeleza haya na mengine mengi. Ninayaona matamanio ya mama kwa taifa hili.

Rushwa na matumizi mabaya ya fedha za serikali vinawahusu watumishi wa umma na ni vema Rais awe mkali sana katika hili.

Kwa kuyadhibiti haya serikali itatekeleza miradi mingi ya maendeleo na taifa kupata maendeleo endelevu; kigezo muhimu kushinda tuzo ya Mo Ibrahim. 

Jambo jingine ni utawala wa demokrasia. Tuwe wakweli, hapa tuna tatizo na ninashukuru Rais analijua.

Ni vigumu kutoka hapa kama hatutakuwa na uchaguzi huru na wa haki. Hii itaonekana kwa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na uhuru wa kufanya mikutano ya kisiasa. 

Muhimu zaidi ni kuheshimu utawala wa sheria. Kufika huko tunahitaji mageuzi makubwa ya sheria, tukianza na katiba ambayo ndiyo chimbuko la malalamiko yahusuyo kukosekana utawala wa sheria na mambo mengine mengi. 

Suala hili lipo mikononi mwa kikosi kazi kilichoundwa na Rais. Mimi kama Lipumba, naona mwanga unaongezeka.
Hivyo namna anavyokwenda na kwa utii wa Watanzania, Rais Samia anaweza kufanikiwa kuleta utawala bora, demokrasia ya kweli, utawala wa sheria, kuondoa umaskini na kuleta maendeleo endelevu. 

Samia ni miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi duniani, hivyo anaweza kutusimamia tuache matumizi mabaya ya madaraka, rushwa, matumizi mabaya ya fedha na mali za umma, utawala wa sheria na usimamizi wa demokrasia ya kweli, hivyo kuondoa umaskini, kuleta maendeleo endelevu, ustawi na furaha kwa Watanzania.
Inawezekana, tuungane na Profesa Lipumba kumsaidia Rais ‘kufanikisha jambo letu’. Nchi hii ni yetu sote, hakuna mwenye hatimiliki.

By Jamhuri