Polisi wanatumia vibaya kosa la kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu

Na Bashir Yakub

Yapo mambo ambayo kwa mujibu wa sheria si kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu. Hata hivyo polisi kwenye vituo vyao wamekuwa wakilazimisha mambo hayo kuwa kosa hilo la kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu kwa sababu wanazozijua wao, mojawapo ikiwa ni mchongo kutoka kwa mlalamikaji.

Masuala ya watu kudaiana fedha ama migogoro ya ardhi kama mtu mmoja kuwauzia watu tofauti ardhi moja si masuala ya polisi, wala si makosa ya kujipatia fedha ama mali kwa njia ya udanganyifu.

Tumesema mara nyingi kuwa mamlaka ya polisi ni  kushughulikia masuala ya jinai tu. Masuala ya kudaiana fedha ni masuala ya madai, si jinai. 

Kwa msingi huu yapo nje kabisa ya mamlaka yao. Masuala ya kudaiana fedha yanaongozwa na sheria ya mikataba Sura ya 345, pamoja na sheria nyingine za fedha na rehani, wakati masuala ya migogoro ya ardhi yanaongozwa na Sheria namba 4 na 5 za ardhi, Sheria ya Usajili wa ardhi na nyinginezo mtambuka.

Kwa hiyo makosa haya na mengine yanayofanana na haya hayawezi kuitwa ya kujipatia mali ama fedha kwa njia ya udanganyifu. Mara nyingi makosa haya yamekuwa yakipelekwa huko kwenye kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu kwa makusudi ili kumkomoa mtu ili awekwe ndani nk.

Vifungu vya 301, na  302, vya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, vinaelezea kosa la kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu kumaanisha ujinai. 

Mfano wa makosa ya kujipatia mali ama fedha kwa njia ya udanganyifu ni wale wanaotuma SMS au kupiga simu na kusema umejishindia kitu fulani, hivyo utume fedha ili upate kitu hicho, na fedha kweli zikatumwa kwake, huku jambo hilo si kweli. Fedha hizo zitakuwa zimepatikana kwa njia ya udanganyifu.

Au mtu anakwambia lete fedha nikuletee mali fulani au nakuagizia Japan huku akijua si kweli. Fedha hizo akizipokea na asilete alichoahidi zitakuwa zimepatikana kwa njia ya udanganyifu. Mifano kama hiyo ndiyo ya kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu.

Aidha, tunasisitiza tena kuwa masuala ya kudaiana fedha, au ugomvi wa ardhi hayaingii kwenye jinai ya kujipatia fedha/mali kwa njia ya udanganyifu, bali ni madai. 

Hivyo, ni kosa kabisa askari yeyote katika kituo chochote kujihusisha na masuala ya madai, labda iwe kwa ushauri. Kama askari atachukua masuala haya ili awashauri au awapatanishe, hiyo itakuwa ni sawa. Ila kama atayachukua ili afungue jalada la kesi hilo ni kosa.

Mahakama Kuu ya Tanzania imekwisha kutoa uamuzi mwingi kuelezea jambo hili na moja ya uamuzi wa hivi karibuni ni katika Madai ya Rufaa Namba 23/2017 kati ya RIBENT RWECHUNGURA vs PONSIAN MUTAYABARWA ambapo Jaji  KAIRO alisema ni makosa mgogoro  wa ardhi kufunguliwa polisi.

Sehemu husika ambapo yafaa upeleke masuala hayo ni mahakamani moja kwa moja. Ukiulizia mahakamani au ukampata wakili utaelekezwa utaratibu mzima wa hapo mahakamani.