*Wadau wadai sekta ya uvuvi nchini imeoza

*Wasema kuna mtandao wa mapapa unaofadhili uvuvi haramu

*Wamwomba Waziri Mashimba Ndaki kuifumua sekta nzima

*Mwenyewe atangaza vita, operesheni maalumu yaanza

Dar es Salaam

Na Alex Kazenga

Wadau wa uvuvi nchini wameiomba serikali kuuvunja mtandao wa uvuvi haramu kwa kuifanyia mabadiliko makubwa sekta ya uvuvi.

Hayo yamekuja ikiwa ni mwezi mmoja tu baada ya Gazeti la JAMHURI kuandika taarifa kuhusu kukithiri kwa uvuvi haramu katika Ziwa Victoria ndani ya mwaka mmoja, hali inayotishia kuyumba kwa uchumi wa wananchi wa Kanda ya Ziwa.

Uvuvi ndiyo shughuli kubwa ya kiuchumi kwa wananchi wengi wa Kanda ya Ziwa, lakini kwa sasa inakabiliwa na hali mbaya kutokana na uhaba mkubwa wa samaki kuwahi kutokea ndani ya Ziwa Victoria; ziwa kubwa zaidi barani Afrika, likishika nafasi ya tatu duniani nyuma ya maziwa Caspian na Superior ya Marekani.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti baada ya kikao na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, kilichofanyika wiki iliyopita kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, wadau wa uvuvi wamedai kuwapo kwa maofisa uvuvi wanaoshirikiana na wavuvi wasio waaminifu kuendesha uvuvi haramu, wakinufaika kwa fedha za rushwa.

“Hii sekta imeoza na ili kukomesha uvuvi haramu na kuliokoa Ziwa Victoria, yanatakiwa kufanyika mabadiliko makubwa ndani ya wizara. Tumezungumza na Waziri Ndaki, lakini kuna mengine hatujamwambia,” amesema mdau mmoja aliyeshiriki katika kikao na waziri akiomba kutoandikwa jina gazetini.

Kikao hicho kimewahusisha wadau kutoka maeneo ya Musoma, Mwanza, Geita, Bukoba na Ukerewe.

Amesema bila kuwaondoa maofisa ‘wachafu’ wa uvuvi, juhudi zote za serikali kudhibiti uvuvi haramu hazitakuwa na maana.

“Lazima waziri na serikali wafanye uamuzi mgumu. Wawaondoe watendaji wote wa sekta ya uvuvi kuanzia wizarani hadi wilayani. Wasiwaonee aibu hata kidogo. Hawa wanafanya kazi kwa mazoea na kuididimiza sekta hii muhimu.

“Wamedumu kwa miaka mingi lakini hawaisaidii serikali wala hawatusaidii wavuvi na wafanyabiashara wenye viwanda. Sekta inaporomoka, wao wapo tu! Hawa ndio wanaokwamisha juhudi za serikali,” amesema, akiongeza kuwa upo mtandao unaowahusisha watendaji ndani ya wizara na wavuvi kufanya uvuvi haramu.

Mapendekezo ya kikao

Wakati hayo yakisemwa, kikao cha waziri na wadau kimepitisha mapendekezo kudhibiti zana haramu zinazotumiwa kwenye uvuvi pamoja na kuwadhibiti wavuvi, hasa wa dagaa.

JAMHURI linafahamu kwamba kwa mwaka mmoja uliopita wavuvi wa dagaa wamekuwa wakitumia taa za nguvu ya jua (solar power) zenye mwanga mkali usioruhusiwa kisheria katika shughuli zao za uvuvi, wakivua dagaa na sangara kwa wakati mmoja, wakitumia nyavu za dagaa; kitendo ambacho pia ni kinyume cha sheria.

Ni taa hizo za ‘solar’ ndizo zimechangia kwa kiasi kikubwa kupukutika kwa samaki ndani ya Ziwa Victoria.

Katika mapendekezo ya kikao cha waziri, imeazimiwa kwamba sasa taa hizo zidhibitiwe huku Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) ikitakiwa kuchunguza nyavu zinazofaa kwa uvuvi.

Mapendekezo mengine ni kufanyika kwa doria za mara kwa mara kulinda ziwa na wavuvi wa dagaa sasa wanatakiwa kufanya uvuvi nyakati za giza tu kama ilivyokuwa awali.

“Siku hizi uvuvi wa dagaa unafanyika hata nyakati za mbalamwezi kwa kutumia taa za ‘solar’. Hizi zina mwanga mkali kushinda mwezi na hata karabai,” anasema mdau mwingine.

Maoni ya wavuvi, Mkuu wa Mkoa wa Geita

Pamoja na maazimio hayo, wadau wanasema sekta ya uvuvi imekuwa ikiishauri vibaya serikali kuchukua hatua zisizofaa katika kudhibiti uvuvi haramu.

Moja ya ushauri mbovu unatajwa kuwa ni wa serikali kuendesha kamata kamata ya wavuvi na kuchoma moto nyavu haramu, mbinu ambayo haiwezi kutokomeza tatizo zaidi ya kuwatia hasara wavuvi na kuangamiza mitaji.

“Mimi sipingi operesheni kamata kamata, lakini inapofanyika wakati haina tija, inawanufaisha watendaji wa serikali na kuwakandamiza wavuvi ambao hukamuliwa fedha kwa nguvu,” amesema mdau mwingine.

Kwa upande mwingine, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule, ameliambia JAMHURI kuwa mkoa wake unaangalia namna ya kuboresha operesheni kamata kamata ili iwe na tija kwa kila upande.

RC Rosemary amesema kupitia operesheni aliyoiendesha yeye mwenyewe baada ya Gazeti la JAMHURI kumpa taarifa za kukithiri kwa uvuvi haramu mkoani kwake, amefanikiwa kuwakamata wavuvi haramu 29 wilayani Chato, nyavu haramu aina ya timba 17 zinazotumika kuvua sato na sangara wadogo na kokoro moja.

“Tumeweka watu wetu kwenye mialo inayosadikiwa kuwa na wavuvi haramu na zana ambazo hazitakiwi. Hao ndio wanaotupatia taarifa za wahusika wote,” amesema Rosemary.

JAMHURI lina taarifa za kukithiri kwa uvuvi wa makokoro na timba katika mialo ya Mwelani na Katete iliyopo Chato mkoani Geita, hasa katika Kisiwa cha Mwaisome karibu na Hifadhi ya Taifa ya Rubondo.

Samaki wanaopita katika mialo hiyo hupakiwa kwenye ndoo na kusafirishwa kwenda kwenye masoko ya Katoro, Geita, Runzewe na Sengerema.

Samaki wanaovuliwa katika Kisiwa cha Mwaisome karibu na Rubondo hupelekwa Nkome na kusafirishwa kwa pikipiki kwenda kwenye masoko mbalimbali. 

Mdau wa uvuvi wa muda mrefu, Medard Mushobozi, anaipongeza serikali kwa juhudi inazochukua, akiiomba iongeze mbinu zaidi katika kupambana na uvuvi haramu katika Ziwa Victoria.

Amesema kuna tabia za wavuvi za muda mrefu zinahatarisha usalama wa ziwa ambazo serikali haijazifanyia utafiti wa kutosha.

“Uvuvi haramu unasababishwa na mambo makuu matatu; ulegevu wa sera ya serikali kuhusu uvuvi na mazao yake, matumizi mabaya yanayofanywa na nchi zinazogawana maji ya Ziwa Victoria na serikali kushindwa kudhibiti zana haramu kuingia Tanzania,” amesema Mshobozi.

Mshobozi ambaye amefanya kazi ya uvuvi kwa zaidi ya miaka 30, amesema endapo hayo matatu yatafanyiwa kazi inavyotakiwa, ziwa litakuwa na manufaa makubwa kwa uchumi wa taifa.

Amesema ni aibu kwa Tanzania inayomiliki asilimia 51 ya maji ya Ziwa Victoria kunufaika kwa kiasi kidogo; huku Kenya yenye asilimia sita tu na Uganda asilimia 43 zikiongoza kwa kunufaika na samaki wanaovuliwa ziwani humo.

“Tanzania tuna visiwa vikubwa na vidogo takriban 162 na mialo ya kufanyia shughuli za uvuvi 250, tunashindwaje kulitumia vizuri ziwa letu wakati tuna uwanda mpana wa kufanya shughuli za uvuvi zenye tija?” amehoji Mshobozi.

Inadaiwa kuwa Uganda ndiyo kinara wa kusafirisha nje ya nchi minofu ya samaki, ikiwa na viwanda 11 vinavyofanya kazi kwa saa 24 dhidi ya viwanda saba tu vya Tanzania ambavyo havina uwezo wa kufanya kazi kwa saa 24 kutokana na uhaba wa samaki.

JAMHURI linafahamu kwamba wavuvi kadhaa kutoka Tanzania hupeleka samaki Uganda ambako huuza kwa faida zaidi.

Mshobozi anailaumu serikali kwa kushindwa kuimarisha ulinzi wa mipaka ya maji yake hasa maeneo yenye visiwa ndani ya Ziwa Victoria, akidai kwamba maeneo hayo ndiyo huwaingiza wavuvi kutoka Uganda na Kenya kuingiza nyavu haramu pamoja na kuvua samaki katika maji ya Tanzania.

Anashauri kuwekwa kwa alama za mpaka majini ili kila nchi ijue mwisho wa eneo lake.

Hata hivyo, hoja ya wavuvi kutoka nchi jirani kuingia Tanzania inapingwa na Katibu wa Chama cha Wavuvi Tanzania (TAFU), Jephta Machandalo, akisema uhaba wa samaki ziwani ni tatizo kubwa kuliko wageni wanaodaiwa kufanya uvuvi nchini.

“Samaki wamekwisha Ukerewe, kwani ni Wakenya au Waganda wanaokuja kuvua huku? Tatizo ni uvuvi haramu ndiyo maana samaki wanaopatikana Ukerewe ni wadogo kweli kweli,” amesema Machandalo.

Amesema kinachovushwa mipakani ni nyavu zisizofaa na wanaofanya hivyo ni wafanyabiashara wa Tanzania wasio waaminifu.

“Mipaka hailindwi, huko ndiko zinakopita zana haramu na kuingizwa nchini. Tunachopaswa kujiuliza ni kwa nini zisidhibitiwe?” amehoji Machandalo.

Ameitaja njia mojawapo ya kudhibiti uvuvi haramu kuwa ni kuwakamata wahusika wanaouza sokoni samaki ambao hawajafikia kiwango cha kuvuliwa.

Anataja matumizi ya nyavu zenye ukubwa wa sentimeta tatu hadi 10, ukubwa usiotakiwa, kuwa sababu nyingine inayoangamiza samaki, kwa kuwa nyavu hizo hukamata hadi samaki wadogo kabisa wenye ukubwa wa inchi mbili hadi tatu.

Samaki wanaotakiwa kuvuliwa na kupelekwa kiwandani au sokoni ni wenye ukubwa wa kuanzia sentimeta 45.

“Kudhibiti uvuvi haramu si kazi nyepesi kama watu wanavyodhani. Fikiria wavuvi wamefikia hatua ya kupika mitego kwenye maji ili kuipunguza matundu kabla ya kuipeleka ziwani,” amesema.

Machandalo anasema mitego ya inchi sita inayokubalika kwenye uvuvi wa sangara hupikwa na kupungua ukubwa hadi kufikia kati ya inchi nne na tano.

Anasema baada ya kikao cha Waziri Ndaki na wadau wa uvuvi, serikali huenda imezinduka baada ya kuelezwa kuwa sangara wanalo zao muhimu linaloitwa ‘bondo’, ambalo ni muhimu kuliko minofu yake.

“Sangara anapokuwa na kilo tano na kuendelea, bondo lake huwa na thamani kubwa. Soko la bondo liko Ulaya na Asia.

“Ni rasilimali iliyofichika kwenye ukuzaji wa uchumi wa taifa, sasa tukiruhusu ziwa lichezewe na sangara kuvuliwa wakingali wadogo maana yake tunateketeza pato la taifa na viwanda vya kuchakata minofu ya samaki hao,” amesema.

Kauli ya Waziri Ndaki

Akizungumza na JAMHURI kuhusu kikao chake na wadau, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, amekiri kuwapo kwa ugumu katika kudhibiti uvuvi haramu kutokana na kuwapo kwa vigogo wanaojihusisha na shughuli hiyo.

“Vita ni kubwa, tutachukua kila hatua inayowezekana kulinda Ziwa Victoria. Tayari kuna boti zipo ziwani kwa ajili ya kufanya doria. Na ikilazimika tutawaomba wenzetu wa vyombo vya usalama kutusaidia,” amesema Ndaki.

JAMHURI lina taarifa ya kuwapo kwa askari wa moja ya majeshi ya Tanzania ambao tayari wameanza kazi hiyo.

Amesema wakati mbinu bora zaidi zikitafutwa kulilinda Ziwa Victoria, kwa sasa wizara inalazimika kutumia nguvu kulilinda.

By Jamhuri