*Fedha za gari la Katibu Mkuu

zilitosha kununua jipya 

  lakini likanunuliwa la mtumba

*Lakutwa lina kadi mbili zikionyesha   

 limetengenezwa mwaka 2015

 na kusajiliwa mwaka 2014

*Katibu Mkuu asema hakumbuki 

mchakato wa ununuzi ulivyofanyika 

*Asema wananunua magari ya

 mtumba kwa sababu wao si serikali

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Mchakato wa ununuzi wa magari ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) likiwamo la Katibu Mkuu wake Taifa, Rashid Mtima, umegubikwa na utata.

Gari hilo la Mtima ambalo ni mtumba (used) limenunuliwa na Talgwu kwa Sh milioni 180 kutoka kwa muuzaji, Dar es Salaam Motors and Commission Agent Ltd, aliyepo makutano ya Mtaa wa Swahili na Barabara ya Morogoro eneo la Fire bila kufuata taratibu za zabuni.

Zabuni kutotangazwa

Kwa mujibu wa kanuni mbalimbali za Talgwu toleo la mwaka 2018, ni kwamba huduma au kitu chochote kitakachonunuliwa na gharama yake ikazidi Sh milioni 80 inatakiwa itangazwe zabuni ya wazi kwa umma ili kila mtu aweze kuomba.

Licha ya kanuni hizo kusema hivyo lakini ununuzi wa gari hilo haukutangazwa kwa umma kama inavyotakiwa na muuzaji akawauzia Talgwu bila kupitia mchakato wa ushindani wa zabuni.

Taarifa ambazo Gazeti la JAMHURI limezipata hivi karibuni kutoka chanzo chake cha kuaminika kilichopo ndani ya Talgwu kimesema kati ya mwaka 2017 na 2018, Mtima, alipeleka maombi kwa Baraza Kuu la Talgwu ya kununua gari jipya lililoanza kutengenezwa kuanzia mwaka 2015 kwa ajili ya matumizi ya ofisi yake na akaidhinishiwa Sh milioni 100.

Chanzo hicho kimesema kuwa baada ya kutafuta gari na kulikosa kutokana na cheo chake, Mtima, akaliomba baraza hilo limuongezee Sh milioni 80 zaidi ili anunue gari lenye thamani ya Sh milioni 180 na akapewa kibali cha kufanya hivyo.

Baada ya kupata kibali hicho, chanzo hicho kimesema Ofisa Ugavi na Ununuzi wa Talgwu, Brigither Emmanuel, akamshauri Mtima kuhusu ununuzi wa gari lenye thamani hiyo kupitia barua yake aliyomwandikia Desemba 17, 2019.

“Kwa mujibu wa taratibu na miiko ya taaluma ya ununuzi wa vyombo vya moto kama magari kwa matumizi ya taasisi na viongozi inashauriwa kununua vipya kabisa, isipokuwa ununuzi wa ndege, meli na treni inaruhusiwa kununuliwa mtumba kwa kibali maalumu cha wizara husika,” amesema Brigither na kuongeza:

 “Hata hivyo, kanuni za ununuzi za chama zipo kimya juu ya utaratibu wa ununuzi wa vyombo vya moto kwa viongozi wa taasisi. Nashauri kuwa gari la katibu mkuu likanunuliwe jipya katika Kampuni ya Toyota Tanzania Ltd kwa kuwa ndio waagizaji wa magari hayo yakiwa mapya.

“Kwa kuwa fedha hizo ni za umma na zinatokana na makato ya mishahara ya wafanyakazi wa serikali za mitaa hapa nchini ni wazi kwamba Sh milioni 180 zinatosha kupata gari jipya kwa ajili ya kiongozi wa taasisi.”

Aidha, chanzo hicho kimesema ofisa ununuzi na maofisa wengine wa Talgwu walikwenda ofisi za Kampuni ya Toyota Tanzania Ltd na kukuta gari aina ya Land Cruiser linalouzwa Sh milioni 180 linapatikana kama bajeti yao walivyotengewa. 

Chanzo hicho kimesema licha ya Mtima kupewa ushauri huo wa kitaalamu lakini hakuufuata na inadaiwa mwaka 2018 akaamuru gari hilo linunuliwe kwa kuwa limeshapatikana kutoka kwa muuzaji huyo ambaye hakupatikana kutokana na zabuni kutotangazwa kama kanuni zao zinavyotaka.

Bali chanzo hicho kimesema amepatikana kienyeji kwa kuwa baada ya fedha hizo kuidhinishwa kilipita kipindi cha muda mrefu bila mchakato huo kuendelea ndipo kwa wakati huo muuzaji huyo akiwa ndiye aliyewapangisha Talgwu jengo la ofisi zao zilizokuwapo Mtaa wa Tanga na Utete, Ilala jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 10 kabla hawajahamia Temeke karibu na Uwanja wa Benjamin Mkapa akawauzia gari hilo.       

Baada ya makubaliano hayo kufanyika, chanzo hicho kimesema Talgwu wakafanya malipo ya gari hilo kwa awamu tano (Gazeti la JAMHURI lina kivuli cha nakala za mkataba wa malipo); Desemba 24, 2018 wamelipa Sh milioni 40, Januari 30, 2019 wamelipa Sh milioni 35, Februari 28, 2019 wamelipa Sh milioni 35, Machi 29, 2019 wamelipa Sh milioni 35 na Aprili 30, 2019 wamelipa Sh milioni 35.   

Kasoro za gari zabainika

Baada ya malipo hayo kuanza ndipo utata na kasoro zikaibuka kutokana na gari hilo kuwa na kadi mbili (Gazeti la JAMHURI lina nakala za vivuli vya kadi) kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilizotolewa na ofisa wake mmoja mwenye namba 20000269 ya kitambulisho chake wakati wa mchakato wa usajili wake.

Kadi ya kwanza ya gari hilo iliyotolewa na TRA katika ofisi zake zilizopo Mtaa wa Samora, Dar es Salaam na kuthibitishwa Januari 3, 2019 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive inaonyesha gari hilo lenye namba za usajili T 327 DPP aina ya Toyota Land Cruiser V8 lilitengenezwa mwaka 2015 ikiwa na maana kwamba limeingizwa hapa nchini miaka minne kabla hawajalinunua rasmi mwaka 2018, huku mmiliki wake akiwa ni Talgwu.

Vilevile chanzo hicho kimesema gari hilo likasajiliwa hapa nchini kwa mara ya kwanza Oktoba 6, 2014 na hiyo pia ikiwa na maana kwamba lilisajiliwa kabla halijaanza kutengenezwa.

Januari 23, 2019, Ofisa Utumishi wa Talgwu, Cassian Mbunda, akamwandikia barua muuzaji baada ya kubaini kasoro za gari hilo.

Kupitia barua hiyo (Gazeti la JAMHURI lina kivuli cha nakala) ambayo nakala yake Mtima alipelekewa, Mbunda, amesema baada ya kupokea gari hilo Januari 2, 2019 na kukaguliwa wamebaini kuna kasoro katika kadi ya usajili iliyotoka TRA.   

“Kadi inaonyesha gari limetengenezwa mwaka 2015 na limesajiliwa kwa mara ya kwanza Oktoba 6, 2014 hapa Tanzania, hivyo limeshatumika kwa miaka mitano hapa nchini Tanzania na haionyeshi ni Land Cruiser la aina gani.

“Mikanda ya viti vya gari haionyeshi tarehe ya lini gari limetengenezwa kama ilivyo kawaida, pia tunaomba kupatiwa nyaraka zilizotumika katika uagizwaji, upokeaji na usajili wa gari husika,” amesema Mbunda kupitia barua hiyo.

Chanzo chetu kimezidi kusema kuwa baada ya muuzaji huyo kuipokea barua hiyo Machi 8, 2019 akapeleka kadi nyingine ya pili ya gari hilo lenye rangi ya fedha iliyotolewa na ofisa huyo wa TRA katika ofisi zake zilizopo Mtaa wa Samora mwenye namba 20000269 ya kitambulisho.

Januari 23, 2019, Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive iliithibitisha kadi ya gari hilo ikiwa inaonyesha lilitengenezwa mwaka 2013 na kusajiliwa kwa mara ya kwanza hapa nchini Oktoba 6, 2014 huku mmiliki wake ni Talgwu.

Pia chanzo hicho kimesema baada ya muuzaji kupeleka kadi ya pili ya usajili ikabainika lilibadilishwa muundo (upgrade) wa gari hilo kutoka kutengenezwa mwaka 2013 na kuonekana kuwa limetengenezwa mwaka 2015 kisha likang’olewa mikanda ya viti na kuwekwa mipya isiyoonyesha mwaka wa matengenezo kama inavyokuwa kwa magari mengine.

Matengenezo yenye shaka baada ya gari kupata ajali

Katika hatua nyingine, chanzo hicho kimesema baada ya gari hilo kununuliwa inadaiwa halikuwa na utaratibu mzuri wa matumizi ya shughuli za Talgwu na Oktoba, 2019 Mtima akiwa safarini kuelekea Newala mkoani Mtwara katika shughuli zake binafsi lilipata ajali na kuharibika na baadaye likarejeshwa Dar es Salaam kwa matengenezo.

Chanzo hicho kimesema baada ya kurudishwa Dar es Salaam lilipelekwa kwa siri katika Gereji ya Bamba Auto Works ya Tabata bila ya utaratibu wa kiofisi.

Aidha, chanzo hicho kimesema baada ya gari hilo kupelekwa katika gereji hiyo inayodaiwa ni bubu, kwa kuwa inadaiwa kutumia gereji nyingine kufanya shughuli zake maeneo ya Magomeni, lilianza kutengenezwa bila kufuata taratibu, bila Brigither ambaye ni ofisa ununuzi kufahamu.

Baada ya taarifa ya ajali hiyo kufika ofisini kwao, chanzo hicho kimesema Brigither akapewa kazi ya kushughulikia matengenezo hayo na akaona ni busara gari hilo likatengenezwa katika Gereji ya Toyota Tanzania Ltd kwa kuwa wao ndio waagizaji wa magari hayo na vipuri vyake.

Chanzo hicho kimesema Oktoba 25, 2019, Brigither, akamuandikia barua (Gazeti la JAMHURI lina kivuli cha nakala) Mtima akisisitiza gari hilo kwenda kuengenezwa katika Gereji ya Toyota Tanzania Ltd.

“Nimepokea dokezo la Oktoba 22, 2019 folio namba 160 likiomba idhini ya matengenezo ya gari lenye namba za usajili T 327 DPP. Utaratibu wa kawaida kabla ya bima hawajatoa fidia Talgwu ilitakiwa kufanya nukuu ya bei ili kujua gharama halisi za bei na kuziwasilisha bima,” amesema Brigither kupitia barua hiyo na kuongeza:  

“Kiwango cha fidia kinatokana na gharama halisi ambayo ofisi itapata katika kurejesha gari kwenye hali yake ya awali. Kwa kuwa bima wameshatoa kiasi cha fedha, nashauri gari hili lifanyiwe matengenezo katika Gereji ya Toyota chini ya usimamizi wa ofisa usafirishaji na dereva mkuu.” 

Vilevile chanzo hicho kimesema ofisa ununuzi huyo akiwa katika mchakato huo kupitia Toyota Tanzania Ltd, walikubaliana na mafundi kwenda kukagua gari hilo ili watoe hesabu ya matengenezo hayo na alipouliza gari lilipo akaongozana nao.

“Alipofika eneo gari lilipo alikuta limeshatengenezwa na bado kupigwa rangi tu na baada ya kushuhudia hatua hiyo ndipo aliwarudisha mafundi wa Toyota ofisini kwao Barabara ya Nyerere,” kimesema chanzo hicho.

Pia chanzo hicho kimesema baada ya wiki moja Bamba Auto Works iliwasilisha hati ya madai ya malipo ya matengenezo ya Sh milioni 47.

Chanzo hicho kimesema baada ya uongozi wa Talgwu kuona ankara ya matengenezo hayo ni makubwa wakati Mtima alisharuhusu yafanyike Bamba Auto Works, wakaamua kuwasilisha madai hayo kwa Kampuni ya Bima ya Zanzibar Insurance iliyopo makutano ya Barabara ya Morogoro na Lumumba.

Aidha, kimesema wakaguzi wa kampuni hiyo ya bima walikwenda kulikagua na baada ya ukaguzi walibaini taarifa katika kadi ya usajili zinatofautiana na taarifa halisi za gari.

Chanzo hicho kimesema baada ya majadiliano ya muda mrefu, kampuni hiyo ya bima ikaamua kulipa Sh milioni 30 kupitia akaunti yao na baada ya hapo mchakato wa malipo ya matengenezo ulishughulikiwa kati ya Mtima na Mhasibu Mkuu wa Talgwu kisha Bamba Auto Works ikalipwa kiasi hicho cha fedha.

Ununuzi wa magari 14 ya makatibu wa mikoa

Pia chanzo hicho kimesema mwaka 2019, Talgwu, imefanya ununuzi wa magari 14 ambayo ni mitumba kwa makatibu wake wa mikoa yenye thamani ya Sh milioni 540 kwa pamoja bila kufuata taratibu na kanuni zinazosema zabuni inayozidi Sh milioni 80 itangazwe kwa umma.

Chanzo hicho kimesema ununuzi wa magari hayo aina ya Toyota Land Cruiser Prado yaliyotengenezwa kati ya mwaka 1996 na 1999 yaliidhinishwa na Mtima akiwa kama ndiye ofisa masuhuli wa Talgwu na kupelekwa mikoani.

Pamoja na mambo mengine, chanzo hicho kimetaja namba za usajili za magari hayo katika mabano na mikoa yalikokwenda kuwa ni Dar es Salaam (T 321 DVE), Morogoro (T 432 DVB), Mtwara (T 318 DVE), Dodoma (T 338 DVE), Katavi (T 397 DVB), Rukwa (T 379 DUS), Mara (T 584 DUN), Tabora (T 126 DUK), Shinyanga (T 583 DUN), Pwani (T 684 DVD), Lindi (T 395 DVB) na makao makuu (T 582 DUN).

Kimesema magari hayo ni chakavu kwa sababu yametengenezwa na kutumika zaidi ya miaka 25 iliyopita na yamenunuliwa kati ya Sh milioni 38 hadi Sh milioni 40.

Pia kimesema magari hayo yameshatembea zaidi ya kilomita 260,000 hadi 300,000 na hiyo ni hatari kwa watumiaji wake ambao ni watumishi wa Talgwu mikoani na wanachama wake kwa ujumla.

Mtima ajibu

Mei 14, 2022, Gazeti la JAMHURI lilizungumza na Mtima kwa njia ya simu yake ya mkononi na kumtaka mwandishi wa habari hii kwenda ofisini kwake kwa ajili ya kupata majibu yote.

Akizungumza kwa jazba amesema amepambana na mambo mengi Talgwu hadi kufika alipo leo.

“Kama una dhamira njema, kama hauna dhamira ya kunimaliza mimi. Kwamba wewe ni mwanadamu, hunijui kwa misimamo yangu. 

“Unajua maneno si kitu, bali ni vitendo, niko katika utumishi huu wa kuwatumikia kwa muda mrefu, najulikana, kuna mambo ukisema nimeyasema kuna watu watashangaa kwa jinsi wanavyonijua, lakini suala la fulana (Gazeti la JAMHURI liliripoti hivi karibuni kuhusu upigwaji wa fedha za sare za Mei Mosi) ulivyoandika kila mtu amenipigia simu,” amesema. 

Mtima amesema anajua msingi wa taarifa zote na hadi zinapotokea na ndiyo maana mwandishi wa habari hii anapata barua zake za mawasiliano ya kikazi ndani ya Talgwu.

“Najua hizo taarifa unazipata wapi? Huyo mtu tulishamfukuza hapa kazini kwa mambo yake ya wizi, kwa mambo yake ya ajabu, hawezi kuja kwako kwa lengo la kunijenga mimi bali atakuja kwa ajili ya kunibomoa tu,” amesema.

Akamtaka mwandishi wa habari hii awe na mawasiliano rasmi na aende ofisini kwake wazungumze kisha amuonyeshe kadi za gari analolitumia. 

“Haiko hivyo, huwezi kunipigia simu muda wowote unaotaka wewe, njoo ofisini kwangu nitakupa taarifa zote na hata hizo kadi za gari nitakuonyesha zote,” amesema na kuongeza:

“Leo (Jumamosi) ni weekend nafanya shughuli zangu, njoo muda wa kazi ofisini utapata taarifa zote, huwezi kufanya mawasiliano ya kirafiki halafu kumbe mtu anakumaliza.

“Mimi ni Katibu Mkuu, njoo ofisini utapata taarifa zote hata hizo kadi utaonyeshwa. Nitakupa usahihi wa hizo kadi, mbona hizo kadi walifuatilia mwaka jana, kadi mbili za nini, za kutoka wapi? 

“Gari limenunuliwa tangu mwaka 2019 hadi leo hayo mambo ya kadi yanatoka wapi? Ionekane lina kadi mbili? Wewe njoo ofisini nitakupa majibu, siwezi kuongea mambo ya kirafiki halafu unanimaliza, sina muda huo.

“Sasa hivi niko njiani naelekea Mtwara halafu unanisumbua sumbua, njoo Jumatatu ofisini uje kupata taarifa na nitakuonyesha hizo kadi.”               

Mei 16, 2022 Gazeti la JAMHURI lilifika ofisi za Talgwu na kuzungumza na Mtima, pamoja na mambo mengine amesema amefanya kazi katika utumishi wa umma kwa miaka 16 hadi ukurugenzi wa halmashauri na ndiyo maana yuko makini na kila kitu anachokifanya Talgwu.

“Nimeamua kuja huku, ni watu wachache sana, unajua mtu anajipima uadilifu hata na wengine, ni watu wachache wanaonigusa, wala sina shida kwa sababu najua ninachokifanya.

“Njoo hapa angalia vitu nilivyovifanya, nimekuja katika hiki chama walikuwa hawana hili jengo, lilikuwa halijaisha, lakini sasa hivi tupo hapa katika jengo la makao makuu. Jengo hili limeanza kujengwa mwaka 2014 lakini halikumalizika hadi nilipokuja na kuanza kazi,” amesema.

Vilevile amesema mwaka 2020 aliingia katika kinyang’anyiro cha ubunge na akasumbuliwa na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) lakini akawaambia siku watakapomchukua kwa sababu wametumwa kumwaribia, kumdhuru na kumpeleka Mahakama ya Kisutu jamii yote itawashangaa. 

Amesema kwa sababu Takukuru imeundwa ili kurekebisha jamii na kuna siku itaonyesha kwamba wako kwa ajili ya kuonea watu.

“Watasema Mtima ni mwizi, ameiba au amejipatia mali kinyume cha taratibu. Unajua mwanadamu anaonekana tu, mimi kwa tabia ninaonekana tu, japo kuna mwingine atasema Mtima ameiba Sh milioni mbili halafu mimi na yeye tukiwa wawili nikamuonyesha misimamo yangu.

“Halafu atasema Mtima huyo ambaye kuna siku nilikaa naye namshauri akakataa leo anaiba Sh milioni mbili!” amesema.

Kuhusu magari amesema ameanza kazi Talgwu Septemba, 2016 kisha akapokea magari manne yaliyonunuliwa kwa Sh milioni 45 kila moja. 

Amesema anachoshangaa baada ya kuanza kazi amenunua magari ya aina hiyo hiyo kwa Sh milioni 40 lakini yanapigiwa kelele za rushwa.

“Watanzania wana shida kweli, tena si Sh milioni 40 bali ni Sh milioni 35, yaani sijui tukoje? Tatizo huu ndio mwenendo wa ofisi na taasisi hii, nimekuja hapa ofisini nimekataa,” amesema. 

Mbali ya hayo, amesema Talgwu ina vitendo vya rushwa mno, japo si vizuri kwake kukizungumzia hivyo chama hicho.

Amesema hata Takukuru wanajua kwamba alimfukuza mhasibu na kesi hiyo ya wizi wa Sh bilioni 9.2 za Talgwu iko kwao.

Amesema kwa sasa wanamtafuta hadi kwa kuwatuma majambazi wanataka kumuua lakini Talgwu imeamua kumpa ulinzi.

“Nilikuja nikamkuta mhasibu anaiba Sh milioni 30 kila mwezi, nikamwambia hapana, hadi nikamfukuza na bila shaka yeye ndiye anayetoa taarifa hizi kwako,” amesema na kuongeza:

“Inafikia hatua unamfukuza mhasibu, mtu wako wa fedha anayeweza kutumia mbinu zozote kuhakikisha unatulia lakini unasema hapana, kwa msimamo huu braza siwezi kufanya kazi na mtu wa namna hiyo.

“Nilivyokuja tu nikagundua anaiba fedha kila mwezi, nikamwambia braza kabla sijaja umeiba, kuanzia sasa nipe Sh milioni 20 halafu yeye angebaki na Sh milioni 10 na maisha yangeendelea lakini nikasema hapana.”

Kuhusu magari 14 ya makatibu wa mikoa, amesema yamefuata taratibu zote kwa kuwa wana kamati ya ununuzi.

Amesema ununuzi wa magari hayo umefuata taratibu na hayana shida yoyote kwa sababu wao si serikali kwamba lazima wanunue magari mapya. 

“Sisi si serikali, kwa hiyo si lazima kununua magari mapya, lakini wewe Prado gani mpya unanunua kwa Sh milioni 40?” amehoji. 

Amesema utaratibu huo ameukuta hivyo na Talgwu haijawahi kununua magari mapya na yeye ameurithi na kanuni zao haziwalazimishi kufanya hivyo ndiyo maana yeye anaendelea nao. 

“Kwa hiyo mtu akikaa akisema Mtima anakwenda kinyume cha taratibu, hakuna, na hizo gari zimenunuliwa kupitia bodi ya zabuni kwa bei hiyo hiyo, haijaongezeka wala haijapungua, eti nimenunua kwa bei ghali ndiyo maana nasema kwamba mwaka 2016 yamenunuliwa kwa Sh milioni 45 ila sasa hivi yamenunuliwa kwa Sh milioni 40, mnasema kuna rushwa. 

“Braza katika maisha nimejifunza vitu vingi, unaweza kuamua hii Talgwu iwe na rushwa, lakini hiyo ni silka ya mtu, ni tabia ya mtu, siwezi kwenda huko,” amesema.

Pia amesema ili anunue magari ya Talgwu ni lazima aweke katika bajeti, kwa bei maalumu na baraza kuu likapitisha wakayanunua.

Amesema baada ya baraza kupitisha zabuni inatangazwa, ataita kamati ya zabuni kupitisha na kama itaandika zaidi ya Sh milioni 40 na taratibu hazikufuatwa, maana yake inawezekana ni kwa sababu mkataba haujapata soko hilo.

“Kama haumjampata mtu mwenye soko hilo na kama haujapata sokoni kile kilichoandikwa katika bajeti, nina utaratibu wa kurudi katika mfumo wangu ili niombe fedha za ziada,” amesema na kuongeza:

“Kwa hiyo tuliweka katika bajeti na ikapitishwa katika baraza kuu, ikaja tukafuata mchakato wote na gari zikanunuliwa na tukazipekeka mikoani au labda tuseme kinyume cha taratibu zipi? 

“Hizo gari zilinunuliwa bila kufuata utaratibu je, hazikuwapo katika bajeti au hakuna muhtasari wa kikao, bodi ya zabuni kwamba haijapitisha?”

Aidha, amesema amewaambia wenzake kuwa yeye hayuko hivyo kwa sababu Talgwu si mwisho kwake, kwa kuwa mwaka 2020 amekwenda kugombea ubunge katika Jimbo la Newala akawa mtu wa pili ndani ya mchakato wa kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Amesema mwaka 2025 anaweza akawa mbunge Mungu akimjalia na mwaka 2026 ataacha majukumu ya Talgwu kwa kuwa hawezi kuendelea na huo ndio msimamo wake.

Amesema anaweza akawa mbunge kisha akawa waziri na ndoto yake kuwa ni kiongozi mkuu wa nchi.

“Lakini kwa msimamo wangu na wakati mwingine unaweza ukazungumza lakini nenda kaangalie nilikopita, nimeacha nini, watu wananionaje? 

“Kuna watu wana dhamira ya kunichafua na nimepambana na watu hapa Talgwu na wameondoka, lazima watakuwa wanalia na kuugulia huko pembeni,” amesema. 

Aidha, amesema kuna watu wengine wanalia huko pembeni kwa sababu wamefanya uzembe wakatimuliwa na wanamtumia meseji wanamwambia kama amewafukuza na yeye atafukuzwa.

“Siwezi kumfukuza mtu kwa hila, niligombea ukatibu mkuu lakini hata kuandika faili hawezi, nimemfundisha lakini nilimwambia mhasibu niliyemfukuza kwamba una nafasi ya kuwa katibu mkuu kama nikitoka, sasa kwa nini utafute ukatibu mkuu wakati mimi bado nipo mezani?

“Nikamwambia sawa na alipojichanganya nikamshikia hapo hapo na sijamuonea bali alijichanganya badala ya kufanya subira kutokana na mazingira ya kuishi kindugu, yaani anataka kugombea nafasi yangu halafu kajichanganya eti nimwache?” amehoji.

Kuhusu gari analolitumia kuwa na kadi mbili na licha ya kumhakikishia mwandishi wa habari hii kwamba akienda ofisini kwake atamuonyesha lakini naye akahoji kuhusu hizo kadi. 

“Sasa kadi mbili kivipi? Kwamba kuna kadi ya kwangu halafu kuna kadi ya Talgwu?” amehoji.

Amekiri kwamba gari hilo wamelinunua kwa Sh milioni 180 baada ya kwanza kutenga Sh milioni 100 na kutotosha kutokana na bei za sokoni.

“Tulilikosa kwa bei hiyo tukarudisha katika vikao tukaongezewa fedha kisha tukaenda kununua hilo gari,” amesema na kuongeza:

“Labda nikwambie kitu kimoja kwamba kuna mtu mmoja alikwenda na hayo yalikuwa ni mambo ya siasa tu, hili nalitumia mimi muda wote wakati ule nagombea nikaenda nalo kule jimboni wakafikiri kama natumia gari langu wakasema nimenunua gari kwa fedha za Talgwu.

“Lakini analitumia kama gari lake. Wakaja Takukuru hapa nikawapa kadi na hadi sasa hivi hizo kadi ziko Takukuru hawajazirudisha, siku naondoka hapa sina hili gari,” amesema.

Amehoji kuhusu kadi mbili kwamba moja ikoje na nyingine ya aina gani?

Amesema hakumbuki kuhusu suala la kadi kuwa hivyo kwa kuwa hata mchakato wote wa ununuzi wa gari hilo hajausimamia yeye bali alisimamia msaidizi wake kwa sababu wakati huo alikuwa anasafiri mara kwa mara.

“Kwamba sijui kadi ilikuja na ikaondoka na ninachojua kadi ni moja tu na wamechukua Takukuru. Kwa hiyo kama kuna kadi mbili sikumbuki kabisa na kama ni kweli basi hata TRA nao wana vitendo vya rushwa,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Talgwu Mkoa (jina linahifadhiwa), akizungumza na Gazeti la JAMHURI hivi karibuni amemshangaa Mtima kusema wao si serikali kwa hiyo anahalalisha matumizi yao ya fedha yasifuate taratibu.

 “Nadhani Mtima hajui anachokisema. Kwa sababu unavyosema wewe si serikali haina maana kuwe na matumizi mabovu ya fedha.

“Ajiulize anasema yeye si serikali je, hizo fedha anazotumia zinatoka wapi? Jeuri yake yote ya matumizi ya fedha hizo ni kwamba zinatokana na michango ya wafanyakazi wa serikali za mitaa wanaokatwa asilimia mbili ya mishahara yao kila mwezi,” amesema. 

Pia amesema Talgwu kutokuwa taasisi ya serikali haina maana kwamba awe na uhuru wa matumizi mabaya kwa sababu zao la fedha hizo zinatoka katika mshahara wa watumishi wa umma.

“Sisi si serikali kama anavyosema na uhuru wetu tulio nao ni kuwatetea wafanyakazi hasa masilahi yao, lakini hatuna uhuru wa kuchezea fedha zao wanazokatwa kila mwezi.

“Hata kanuni zetu za ununuzi kama ziko kimya hazisemi kuhusu kununua magari mapya lakini tujiulize, serikali inanunua magari mitumba, je, kanuni na sheria za serikali katika ununuzi zipi ni kubwa na tunapaswa kuzifuata zipi?” amehoji.

By Jamhuri