Simba wameshatua Dubai kwa ajili ya maandalizi mafupi ya kujiandaa na mechi za ligi, FA na Klabu Bingwa Afrika. Inavutia kwa namna ambavyo Simba inaishi kisasa zaidi. Simba wanakwenda nje ya nchi kwa mara ya tatu msimu huu katika nia ya kuwapa wachezaji wa timu nafasi ya kujiandaa na mazoezi. 

Kocha mpya wa Simba, Roberto Oliviera, atapata muda mzuri wa kuandaa wachezaji wake katika mfumo anaoutaka yeye ingawa muda hautoshi sana lakini walau atakuwa katika mazingira sahihi na utulivu. Ni ukurasa mpya kwa wachezaji na kocha mpya.

Safari hii inatokea mara tu baada ya ujio wa kocha mpya ambaye ni mgeni toka Brazil. Kabla yake alikuwepo kocha mzawa Juma Mgunda ambaye alitwaa mikoba toka kwa kocha wa kigeni Zoran Maki. Chini ya Zoran Maki Simba walikwenda Misri na baadae Sudan kwa ajili ya kuiandaa timu. Chini ya Mgunda timu ilifanya maandalizi yake nchini. 

Wachezaji wameshatambua kwamba route za nje zinapatikana chini ya makocha wa kigeni sio wazawa. Katika mazingira kama hayo wachezaji wetu wa kigeni na wazawa wataendelea kufanya vizuri sana chini ya makocha wa kigeni kuliko makocha wazawa.

Wengi tunaamini makocha wa kigeni ni bora kuliko wazawa lakini ukweli ni kwamba makocha wa kigeni wanapotua kwenye timu zetu kila kitu kinabadilika kuanzia kambi ya mazoezi, vifaa vya mazoezi, ulipaji wa posho na mishahara huwa katika ubora mkubwa.

 

Mchezaji yeyote kama binadamu anapenda mambo mazuri na kwa kuwa hayo yanapatikana kupitia makocha wa kigeni basi wachezaji wataendelea kufanya vizuri chini ya makocha wa kigeni kwa sababu makocha wazawa huwa wanatumia katika kuganga njaa na kubana matumizi jambo ambalo haliwavutii wachezaji wazawa na wa kigeni. 

Makocha wa kigeni hawapo tayari kufanya kazi ikiwa wachezaji hawalipwi posho Kwa wakati na wala hawataki kuona changamoto za wachezaji hazitatuliwi na viongozi wao na huu ndio uchawi unaotumika kuwasaidia makocha wa kigeni kufanya vizuri. 

Sitashangaa kumuona Kibu Denis akizaliwq upya na kuifanyia makubwa Simba. Habibu Kyombo anaweza akaimbwa sana na mashabiki wa Simba na kejeli zote anazopewa sasa zikatupwa kwa Mgunda kwamba hakuwa anajua namna sahihi ya kumtumia.