UDA-RT sikio la kufa

DAR ES SALAAM

Na Waandishi Wetu

Kinachoendelea ndani ya taasisi zinazohusika na Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam ni giza nene licha ya maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kutaka mabadiliko ya haraka ya mfumo wa utendaji.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kwamba ubia uliokuwapo baina ya serikali na sekta binafsi ni kama haupo tena, na sasa mradi huo unaendeshwa na serikali pekee.

Ubia wa serikali na sekta binafsi (PPP) ulihusisha Kampuni ya UDA Rapid Transit (UDA-RT) pamoja na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), wakala unasimamia miundombinu huku mwekezaji akishughulika na kutoa huduma ya usafiri.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kwamba ‘ndoa’ ya wabia hao ‘ilikufa’ tangu mwaka 2019 kwa serikali kuchukua asilimia 85 ya hisa na mwekezaji kubaki na hisa za asilimia 15 tu.

Aprili 19, mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alitembelea mradi huo maarufu kama ‘mwendokasi’ na kuonyesha kusikitishwa na hali mbaya aliyoikuta, akihofia kufa kwa mradi huo.

Akizungumza na JAMHURI, aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya UDA Rapid Transit (UDA-RT), Robert Kisena, anasema hafahamu kinachoendelea kwa sasa ndani ya mradi huo.

“Kwamba huduma imedorora au la, siwezi kusema lolote. Sifahamu. Mimi simo kwenye operation (uendeshaji) za UDA-RT. Nimebaki kama mwanahisa tu.

“Mwaka 2019 mambo yakabadilika, menejimenti iliyokuwa chini yangu ikaondolewa. Serikali ikabadili muundo wa hisa za UDA-RT, ikachukua asilimia 85 ya hisa hizo na kuacha asilimia 15 kwa Simon Group Limited (SGL). Hili (UDA-RT) sasa ni shirika la umma, lililoko chini ya Msajili wa Hazina (TR) kama yalivyo mashirika mengine ya umma.

“Awali wakati mradi unaanza, Simon Group ilikuwa ndiyo majority shareholder (mwanahisa mkuu). Kwa hiyo tangu wakati huo operesheni zipo chini ya serikali na ninaamini serikali haikuwa na wala haina nia mbaya! Siku zote serikali huwa na nia nzuri kwa wananchi wake,” anasema Kisena.

Akizungumzia kuhusu nani hasa kwa sasa mwenye jukumu la kulipa madeni ya UDA-RT, Kisena anasema: “Ni serikali. Mimi madeni yanayoniumiza kichwa ni ya Simon Group. Hisa za Jiji la Dar es Salaam.

“UDA-RT ilikopeshwa na Benki ya NMB kwa kupitia ‘cross company guarantee’. Sina shaka NMB wanayafahamu mabadiliko ya UDA-RT, kwa hiyo hawawezi kuja kunidai mimi.”

Muundo wa hisa uliopendekezwa na kutekelezwa na serikali wa hisa 85/15, unaacha maswali magumu, na JAMHURI likataka kufahamu kutoka kwa Kisena sababu ya kukubaliana na muundo huo na ni nani aliyelipa kodi ya uhamishwaji wa hisa hizo kama sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) capital gain tax inavyotaka.

“Wakati wa mabadiliko ya hisa hizo, mimi nilikuwa jela (mahabusu). Mambo yote walifanya serikali na mimi nikapewa taarifa tu, hivyo nilikubali kila kitu. Kwa kweli, hata kama wangesema wanachukua hisa zote, nilikuwa tayari.  

“Kodi ya uhamishwaji wa hisa nadhani ilikaribia Sh bilioni 1.6 hivi. Ukienda BRELA (Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni) utajua. Baada ya TRA kunifuata wakitaka kodi iliyotokana na eti mimi kuuza hisa zangu, niliwaambia sijapata hata senti tano na wala hapakuwa na mauziano yoyote,” anasema Kisena.

Ingawa hakuwa tayari kuzungumzia taarifa za kudorora kwa huduma ya Mwendokasi zilizothibitishwa na Majaliwa na kushuhudiwa na JAMHURI, Kisena anasema ubunifu uliokuwapo wakati UDA-RT ilipoanza kutoa huduma Mei 2016, uliashiria mustakabali mwema.

“Operesheni zetu hazikutoa kipaumbele kwa nauli za abiria. Tulifahamu kwamba ile ni huduma kwa umma. Hakuna sababu ya kuwaumiza wananchi kwa kuwatoza nauli kubwa.

“Sasa ili kuendelea kutoa huduma bora, tukawa wabunifu kwa kutafuta vyanzo mbadala vya mapato. Tulianzisha branding ya mabasi na billboards,” anasema.

Hata hivyo JAMHURI lilitaka kufahamu kutoka kwa Robert Kisena kuhusu masharti ya kimkataba kuhusu operesheni zao pamoja na muda ambao kwa hakika ulikuwa miaka miwili tu ya majaribio (kipindi cha mpito), huku wakitakiwa kutumia tiketi za kawaida (za karatasi) na badala yake, UDA-RT wakaenda mbali zaidi kwa kutumia kadi za kielektroniki, wakidaiwa kukiuka mkataba.

“Mkataba wa mtoa huduma kipindi cha mpito unaelekeza matumizi ya simple electronic ticketing system. Mamlaka (Serikali) zikatuagiza kuleta Electronic Fare System (EFS), yaani kadi za kielektroniki.

“Ikabidi twende benki kuomba mkopo. (Benki) Wakatuambia tunapaswa kuwa na comfort letter kutoka Hazina. Tukaipata na tukaleta kadi za kielektroniki za kwanza kutumika kwa usafiri nchini (ambazo sasa hazitumiki).

“Kwa kweli tulikuwa tunakwenda vizuri kabisa. Hadi ninakwenda mahabusu, mabasi yote 140 yalikuwa barabarani.

“Tulikuwa tunaingiza kwenye operesheni asilimia 90 ya mabasi kama mkataba unavyotaka. Malengo yetu yalikuwa ni kuufanya mradi uvutie,” anasema Kisena.

Kwa sasa, UDA-RT huingiza kwenye operesheni chini ya asilimia 50 ya mabasi (kwa mujibu wa Majaliwa), huku juhudi zikifanyika serikali isaidie kuingiza barabarani mabasi 70 yaliyopo bandarini, ingawa wananchi wanahofu kuwa iwapo mabasi hayo nayo yatakufa, huenda mradi mzima nao ukafa.

JAMHURI limezungumza na Msajili wa Hazina, Athuman Mbutuka, kufahamu namna ambavyo serikali ilijitwalia hisa kwa asilimia 85.

“Sasa hapa kuna vitu viwili, moja ni suala la hisa zilivyouzwa, hilo naomba uwasiliane na BRELA wakwambie mchakato ulivyokwenda.

“Jambo jingine naomba uwasiliane na aliyeuza hisa zake, Simon Group Limited, maana yeye ndiye alizungumza na serikali kuhusu mauzo ya hisa hizo.

“Simon Group Limited alizungumza na serikali, hakuzungumza na Msajili wa Hazina. Yeye atakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kulizungumzia hilo. Naomba nisitoe maoni zaidi ya hapo,” anasema Mbutuka.

JAMHURI limemtafuta Ofisa Mtendaji Mkuu wa DART, Dk. Edwin Mhede, ili kufahamu kinachoendelea ndani ya wakala huyo baada ya maelekezo ya waziri mkuu.

“Nitakupatia ofisa mmoja hapa akusikilize halafu atanishauri,” anasema Dk. Mhede.

Hata hivyo baadaye kidogo, JAMHURI lilipigiwa simu na mmoja wa maofisa wa DART akisema alikuwa ameelekezwa na wakubwa wake kuwasiliana na kuona namna miadi itakavyowekwa ili kuzungumza na Dk. Mhede.

Baadaye mtu aliyejitambulisha kama Dk. Eliphas Mollel na kusema yeye ni Mkurugenzi wa Utawala kutoka DART, akasema kuwa baada ya majadiliano wamegundua maswali ya JAMHURI yanashabihiana na hoja za waziri mkuu.

“Ninaomba msubiri hadi pale majibu tuliyopeleka kwa waziri mkuu atakapoyapata, pengine tuwasiliane baada ya wiki kama mbili hivi. Hatuwezi kutoa kwenu majibu tuliyoyapeleka kwa waziri mkuu,” anasema Dk. Mollel.

Kwa kuwa DART iko chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), JAMHURI limemtafuta Katibu Mkuu, Profesa Riziki Shemdoe, ambaye alielekeza jambo hilo lipelekwe kwa Dk. Mhede wa DART.

Watumiaji mabasi wazungumza

Maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam wanaoishi maeneo ambayo mradi wa BRT awamu ya kwanza unapita, wamekuwa na matarajio makubwa ya kupata ahueni ya usafiri ndani ya Jiji la Dar es Salaam baada ya mradi huo kuzinduliwa miaka mitano iliyopita.

Miongoni mwa wakazi hao ni akina mama wajasiriamali wanaouza samaki, wakitokea maeneo ya Mbezi na Kimara. Kutokana na aina ya biashara yao, hulazimika kuamka alfajiri kwenda Kivukoni (Feri) kwenye soko la samaki.

JAMHURI limezungumza na mmoja wa wajasiriamali hao, Mwanahamisi Mitawa, anasema usafiri wa mwendokasi umepunguza adha ya msongamano barabarani.

“Hilo kila mmoja analiona na kulishuhudia. Zamani (wakati wa daladala) haikuwa hivi. Lakini sasa uchache wa mabasi ya mwendokasi unaleta usumbufu mkubwa na kutufanya tufikirie kuurudia usafiri wa daladala,” anasema Mwanahamisi, mkazi wa Mbezi kwa Musuguri.

Mwanahamisi huamka alfajiri saa 11 kwenda kununua samaki Soko Kuu la Samaki la Kivukoni (Feri) na kwa miaka mitano amekuwa mtumiaji ‘mtiifu’ wa mradi wa BRT.

“Ni lazima kuamka saa 11 alfajiri kwa kuwa ukiamka saa 12, ujue hilo limeshakuwa tatizo. Utasubiri usafiri huo kituoni kwa dakika hadi 40, hakuna gari linalotokea. Hapo tayari umeshachelewa na biashara ya Feri hufanyika asubuhi,” anasema.

Anasema kero ya usafiri imeongezeka maradufu baada ya serikali kuhamishia kituo kikuu cha mabasi Mbezi Luis kutoka Ubungo, hali hiyo imegeuka kadhia kwa wakazi wa maeneo hayo maana sasa watumiaji wa usafiri wa mwendokasi wanakuwa wengi kuliko uwezo wa mabasi.

“Mabasi ni ya kugombania kutokana na kuwa machache, ukiwa na ndoo za samaki huwezi kukimbilia kama wengine, inakubidi ukae kituoni muda mrefu hadi atakapokuja dereva atakayejisikia kuwabeba,” anasema Mwanahamisi.

Anaitaja Jumapili kama siku ngumu zaidi kwa wasafiri wanaotoka Kivukoni kwenda Mbezi moja kwa moja akiwaomba UDA-RT kuongeza mabasi siku za Jumapili.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mkazi wa Kimara Korogwe, Agnes Richard, akiongeza kuwa mbali na Jumapili, hata siku za kazi adha ya uhaba wa mabasi husababisha usumbufu kwa wanaotegemea usafiri huo.

“Kuna madereva wa mabasi hayo wenye tabia ya kusimamisha mabasi kituoni muda mrefu huku abiria nao wakilazimika kuwasubiri.

“Unasubiri kwa muda mrefu, mabasi yamesimama tu. Sisi wauza samaki hali hiyo huwa inatishia mitaji na biashara zetu, kwa kuwa tunachelewa kuwafikisha samaki sokoni,” anasema Agnes.

Kwa upande mwingine, ujio wa mwendokasi unatajwa kuwa kichocheo cha ongezeko la wafanyabiashara wa samaki katika soko la samaki Feri katika kipindi cha miaka mitano ya uwepo wa mradi huo.

“Mwendokasi imerahisisha usafiri na kufanya usafirishaji wa samaki kuwa rahisi. Zamani ni akina mama tu ndio tulikuwa tunafanya biashara hii, lakini kwa sasa hata vijana wa kike na wa kiume wameingia kutokana na urahisi wa usafiri uliokuwapo mwanzo,” anasema Habiba Mussa, mkazi wa Kibamba.

Aprili mwaka huu, Waziri Mkuu, Majaliwa, baada ya kutembelea BRT alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha wa DART, Suzana Chaula, baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.

Pia akaahidi kufikisha suala la aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa DART, Mhandisi Ronald Rwakatale, kwenye mamlaka za uteuzi.

Hata hivyo, mtendaji huyo aliondolewa na nafasi yake ikajazwa na Dk. Mhede.

“Tangu Mtendaji Mkuu ameingia DART ana miaka mitano, hakuna hata basi moja alilonunua, na anasema hana fedha, kwani abiria hawasafiri, wakati kila siku wanapigania kule Kimara na wote wanalipa? Unasemaje hakuna fedha za kununulia mabasi?” anahoji Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema kuwa tangu mradi huo ulipoanza mabasi yamekuwa yakipungua kutoka 140 hadi 85: “Watendaji wapo tu wamekaa ofisini wanapigwa na AC (viyoyozi) wananchi wanaumia. Hatuna sababu ya kumbakiza mtu kama hafanyi kazi.”

DART ilianzishwa na serikali kwa ajili ya kuondoa adha ya usafiri kwa wananchi lakini viongozi hao wameshindwa kusimamia vizuri, hivyo kusababisha mradi huo kudorora.

“Kwa nini ukatishaji wa tiketi haufanyiki kwa njia ya kielektroniki kwa asilimia 100? Tiketi zinauzwa kwa vifurushi.

“Haiwezekani. Watu wanafanya ujanja ujanja tu. Wanakuja na tiketi zao mfukoni halafu wakimaliza, anauza za POS (Mashine ya Kielektroniki ya Kukusanyia Mapato) na wasimamizi wapo tu. Mkurugenzi wa Fedha yupo tu, ameshindwa kusimamia hili na limo mikononi mwake.

“Kwa nini mnauza tiketi kwa vifurushi hamtumii mashine kukata tiketi? Mnaua wakala huu kwa sababu wauzaji wa tiketi wanakuja na tiketi zao na nyingine mnazileta nyinyi. Hamuwezi kusimamia mradi huu wa kimkakati,” anasema Majaliwa.

Usuli

Wakati serikali inakopa zaidi ya Sh bilioni 300 kutoka Benki ya Dunia ili kujenga BRT, ilikusudia kumaliza adha ya usafiri jijini Dar es Salaam.

Kuukamilisha mradi huo wenye kilomita 20.9 kutoka Kimara mpaka Kivukoni, Sh bilioni 403 zimetumika, zikiwamo Sh bilioni 307 (Dola za Marekani milioni 290) ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia na kiasi kilichobaki kilitolewa na serikali.
Lakini kwa siku za karibuni, tofauti na malengo yaliyokuwapo kipindi cha uasisi wake, abiria wanaoutegemea mradi huo wanapata kero zilizotarajiwa kumalizwa.
Usafiri wa mabasi ya mwendokasi Dar es Salaam, ni mfumo ulioanza kazi jijini Dar es Salaam Mei 2016. 

Mfumo huo unajumuisha awamu sita na awamu ya kwanza ilianza kujengwa Aprili 2012 na kukamilika mwishoni mwa mwaka 2015.