Wiki iliyopita, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Mrisho Gambo, alishuhudia namna Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (Profesa Maji Marefu), anavyopigwa vita ya kikabila na baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali jimboni humo.

Gambo alikuta vifaa vya ujenzi vilivyotolewa na Maji Marefu vikiwa vimefungiwa ofisini. Vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na mifuko 40 ya saruji, makopo ya rangi na nondo 20 na Sh. milioni 1.5 vilitolewa na mbunge huyo ili vitumike kukarabati kituo cha polisi cha Tarafa ya Bungu.

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya nifanye nini sasa? Nimetoa vifaa hivi tangu mwaka 2010, lakini hadi leo havijatumika. Haya ni mambo ya kisiasa. Tunajitahidi kuleta maendeleo kwa wananchi, lakini wengine kwa sababu zao wanaacha vifaa hivi vinaharibika na hawa ndiyo watendaji wetu wa halmashauri ya wilaya,” alilalamika mbunge huyo.

Pamoja na vifaa hivyo kutosheleza mahitaji yaliyokuwa yakitakiwa, lakini fundi alikarabati sehemu ya kuhifadhia silaha peke yake, kisha vilivyobaki vikaachwa utadhani alivipeleka ili vihifadhiwe mahali hapo. Baada ya kumaliza ukaguzi na kujiridhisha na hali halisi, Gambo aliwaamuru polisi wawakamate Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Bungu, Mohammed Kalaghe; na Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mzee Mambo wanaotuhumiwa kufanya hivyo.

Simtetei Maji Marefu katika hali yoyote ile, hata hivyo, bado namfahamu vizuri kwa sababu tumekutana mara kadhaa katika shughuli za kisiasa za Chama Cha Mapinduzi (CCM) nje ya Tanga, na pia nimezuru jimbo lake kwa zaidi ya mara tatu kati ya Aprili 2011 na Julai mwaka huu.

Ndiyo maana nasema bila shaka yoyote kwamba Profesa Maji Marefu ni mmoja kati ya wabunge wanaofanya kazi nzuri. Anajitahidi kwa juhudi na maarifa yake yote kuwatumikia wapiga kura. Anafuatilia matatizo na kero walizonazo wananchi, anazungumza nao mikutanoni ili kujua shida zao, mahitaji yao na kutekeleza ahadi alizotoa mwaka 2010.

Hata hivyo, jambo linalosikitisha ni kuwapo harakati za kutaka kumkwamisha asitekeleze ahadi hizo, jambo linalofanywa si na viongozi wa ngazi za chini peke yake, bali hadi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Vijijini kwa sababu tu ana asili ya Mkoa wa Ruvuma.

Wakati wa vikao vya bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/2013 vilivyomalizika wiki mbili zilizopita, kiongozi mmoja wa juu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, aliwazuia madiwani walioalikwa na Profesa Maji Marefu kwenda Dodoma ili pamoja na mambo mengine, kujifunza namna Bunge linavyofanya kazi. Alifanya hivyo huku akisema mbunge huyo si lolote na kutaka apuuzwe huku akitamba kwamba hawezi kumfanya chochote, kauli ambayo sikutarajia kama inaweza kutolewa na kiongozi mwandamizi wa umma.

Nawapongeza baadhi ya madiwani waliopuuza agizo hilo na kuitikia mwaliko. Nawapongeza kwa vile walifanya jambo zuri kwa kukataa chembe chembe hatari za ukabila; janga ambalo Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo hazina ugonjwa huo. Harakati zinazofanywa dhidi ya mbunge huyo za kugomea hadi misaada ya maendeleo anayoitoa ni hatari. Ni ujinga ambao mtu yeyote mwenye akili timamu anajua kwamba kamwe haumkomoi Profesa Maji Marefu, bali wananchi wa jimbo hilo.

Wanajicheleweshea maendeleo yao wenyewe kwa kuyapiga vita kwa misingi ya ukabila. Wanajikomoa kwa kumchukia mbunge huyo eti kwa sababu tu asili yake si ya Mkoa wa Tanga. Wapo wenye mawazo mafupi wanaoweza kuuliza kuwa kituo cha polisi na maendeleo vina uhusiano wa namna gani, swali ambalo halina hoja maana msingi wa maendeleo yoyote duniani ni amani, kisha ndipo shughuli nyingine zinafuata.

Kama hakuna amani wananchi hawawezi kuishi mahali popote hata pawe na rasilimali za maendeleo kuanzia ardhi yenye rutuba, madini, bahari, maziwa, mabwawa au mito yenye samaki wa aina zote, misitu minene yenye miti ya mbao, mbuga zenye wanyamapori, ndege wa kuvutia na kadhalika.

Hakuna anayeishi au kuweka shughuli yoyote ya kudumu ya maendeleo katika eneo hatari kwa maisha yake kwa mfano lenye vita vya mara kwa mara, wanyama hatari kama tembo, simba, mamba, chui, viboko, faru, nyoka wenye sumu kali na hata vinginevyo. Ndiyo maana kituo cha polisi ni sehemu muhimu kwa maendeleo. Hii ni kwa vile kazi yake kubwa na pekee ni kuimarisha usalama wa wananchi dhidi ya wahalifu.

Hapo ndipo ninapowashangaa wote wanaompiga vita Profesa Maji Marefu; wale ambao kuna wengine ni viongozi waandamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Vijijni. Nawashangaa kwa sababu wanafanya harakati za kuzuia maendeleo ya jimbo hilo.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220, 0762 633 244 na 0782 133 996

 

By Jamhuri