Toleo lililopita tuliishia aya isemayo: “Mahakama ilikubali hoja hii ya Wakili Erick na kumpa ushindi kwa hoja hii. Kumbuka huyu Erick ndiye anayetajwa kuongoza mchakato wa kuzuiwa kwa Airbus Afrika Kusini.” Sasa endelea…

Kukamatwa ndege

Baada ya maombi ya serikali kutupwa kama tulivyoona hapo juu, kumlipa Mzungu kukakoma. Mzungu alikosa namna ya kukaza hukumu hapa Tanzania kwa kuwa Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Serikali, 1967 inakataza kukamata mali za serikali kama njia ya kukazia hukumu.

Lakini pia haitoi muda wa ukomo wa  lini mtu aliyeishinda serikali awe amelipwa. Unasubiri mpaka iamue yenyewe kulipa na kwa muda inaotaka.

Baada ya kuyaona hayo, Mzungu akakimbilia Afrika Kusini kwenye Mahakama ya Gauteng na kufungua shauri namba 28994/2019 la kukazia hukumu, akijua huko mali za serikali ruksa kukamatwa katika kukazia hukumu.

Kumbuka kuna hukumu mbili. Ya kwanza, ni ile iliyokufa, ile ya taasisi ya usuluhishi, na ya pili ni hii iliyotokana na makubaliano kati ya Mzungu na serikali, ambayo iko hai. Swali kwa Mzungu na timu yake lilikuwa ni hukumu ipi ikaziwe hapo Afrika Kusini kati ya hizi mbili?

Hii iliyotokana na makubaliano ambayo sasa ndiyo iko hai ilikuwa haiwezekani kukaziwa  Afrika Kusini, kwa kuwa mahakama ya huko haitakuwa na mamlaka kutokana na kuwa tukio au makubaliano yaliyofanyika Tanzania, hivyo mahakama za Tanzania pekee ndizo zenye mamlaka.

Mzungu na timu yake kwa kulijua hilo, wakaamua waachane na hiyo hukumu iliyo hai na kuamua kuomba kukazia hii iliyotokana na taasisi ya usuluhishi ambayo mahakama ya Afrika Kusini inaweza kuikazia, kwa kuwa ni ya kimataifa.

Lakini kumbuka hukumu hii si hai tena, kwa kuwa iliuliwa na ile hukumu iliyotokana na makubaliano, na zaidi Wakili Erick na Mzungu walishasema kuwa hukumu hiyo ilishakufa wakati wanapinga maombi ya serikali kama tulivyoona awali na kwa hoja hiyo hiyo wakashinda.

Kwa hiyo wakaamua kuomba kukazia hukumu ambayo wanajua kabisa kuwa ilishakufa na hawakuthubutu kulisema hilo mahakamani ili wafanikiwe, na hakika walifanikiwa kwa kuizuia AIRBUS  5H-TCH.

Kuachiwa ndege

Mawakili wa Serikali walipoungana na wale wa Afrika Kusini waliwasilisha hoja nyingi lakini mojawapo ni ile ya kwamba ndege imekamatwa kwa kutumia hukumu iliyokwishakufa.

Kwa kuzingatia hoja hiyo na kwa ushahidi, Jaji Twala M.L akaridhika na akaona haja ya kuiachia ndege, kwa kuwa ilikamatwa kimakosa kwa kutumia hukumu ambayo haipo.

Mambo mawili muhimu

Kwanza, je, deni la Mzungu limekufa? Jibu ni hapana, deni bado lipo mpaka hapo serikali itakapoweza kufanikisha utaratibu wa kisheria wa kuliondoa, au kuamua kumlipa, au Mzungu atumie taratibu za ndani kupata fedha hizo, au asamehe.

Pili, je, serikali inaweza kupata chochote kwa Mzungu? Jibu ni ndiyo, inaweza kupata chochote kama ifuatavyo: Mosi, imeamriwa serikali ilipwe gharama zake zote za kuendeshea kesi, ikifuatilia italipwa. Pili, inaweza kumfungulia Mzungu mashitaka na kumdai fidia ya hasara zote alizosababisha.

Hili linawezekana kwa sababu mchakato mzima wa kuzuia ndege ulijawa uongo/udanganyifu, kwa kuwa hawa walijua kabisa hukumu wanayokazia imekufa lakini kwa makusudi wakaendelea kufanya hivyo (abuse of court process). Yote kwa yote hivyo ndivyo ilivyokuwa.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.

By Jamhuri