Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amefariki akiwa na umri wa miaka 95. Alisemwa na atasemwa sana, si kwa mema ila kwa mabaya.

Nianze na mabaya yake. Aliongoza Zimbabwe kuanzia mwaka 1980 baada ya uhuru wa nchi hiyo akiwa amerithi uchumi imara, lakini miaka 37 ya uongozi wake ikazorotesha sana uchumi wa Zimbabwe.

Inakadiriwa kuwa kwenye mapigano yaliyoongozwa na jeshi la Zimbabwe ya kuzima upinzani dhidi ya serikali yake kwenye jimbo la Matebeleland kati ya 1982 hadi 1984 watu 10,000 waliuawa.

Anasemwa kwa kuhimiza uporaji wa mashamba ya raia wazungu wa Zimbabwe baada ya mpango wa ugawaji ardhi kwa hiari kusuasua kwa sababu wamiliki hawakuwa tayari kuuza ardhi zao.

Ingawa alishinda uchaguzi katika vipindi vitatu tofauti uchaguzi huo uligubikwa na machafuko na umwagaji damu, na kuna tuhuma kuwa alishinda kwa hila na kupokonya ushindi kutoka kwa mgombea wa chama kikuu cha upinzani.

Alijiongezea maadui, hasa kutoka kwenye serikali na taasisi za nchi za magharibi, kwa kupinga na kuandama raia wake ambao walionekana kuegemea kwenye mapenzi ya jinsia moja.

Niongeze tathmini yangu. Kosa kubwa alilofanya ni kubaki madarakani kwa muda mrefu na kujiongezea upinzani kutoka kwenye makundi mengi ndani ya jamii. Hulka ya binadamu ni kutaka mabadiliko kila mara. Kiongozi anayebaki madarakani kwa muda mrefu hupambana na kiu hii ya mabadiliko.

Kosa hilo likazaa lingine; hakuwa na mkakati maalumu wa kurithisha madaraka ya uongozi ndani ya chama chake cha siasa. Kosa hilo likaleta migongano mikubwa na mgawanyiko ndani ya chama chake na kuibua makundi yaliyowania kurithi uongozi wake.

Mgawanyiko ukasababisha hata jeshi kuhusishwa na likachagua upande mmoja. Matokeo yake likaomuondoa madarakani kwa taratibu zinazoonekana kukiuka misingi ya kikatiba. Lakini kwa sababu yalimtokea Mugabe, kiongozi aliyejitokeza kugombana na wakubwa, sauti za kupinga hatua zile za jeshi hazikusikika sana.

Kuheshimu katiba ni muhimu sana, lakini si rahisi sana kulishutumu jeshi kwa hatua hiyo. Inawezekana kabisa kuwa hali ile ya mvutano baina ya makundi hasimu ndani ya chama cha Zanu-PF ingeachwa iendelee leo hii Zimbabwe ingekuwa kwenye mpasuko na machafuko makubwa.

La muhimu ni kusisitiza kuwa muendelezo wa historia ya Zimbabwe utaje mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa Rais Mugabe, lakini bila kusahau kufanya tathmini juu ya uwezekano kuwa ni jeshi hilo hilo ndilo limelinda amani na usalama wa nchi hiyo.

Nigeukie mazuri yake kwa kusema hakuna kiongozi mzuri asiye na dosari. Aidha, viongozi wenye sifa mbaya ambao hatuwezi kuwasifia kwa lolote ni wachache.

Kwa kawaida, historia za viongozi zina ukweli, zina chumvi; zinaweza kuwa na sifa ya kupitiliza, lakini zinaweza pia kuwa na uongo dhidi yao usiyo na mipaka.

Kundi moja la watu linalosifiwa sana kuweka misingi imara ya serikali ya kidemokrasia nchini Marekani ni waasisi wake. Wanaojulikana zaidi ni George Washington, James Monroe, John Adams, Benjamin Franklin, James Madison, Alexander Hamilton, na Thomas Jefferson. Washington, Jefferson, na Madison walimiliki watumwa, lakini hayo hutayasikia sana juu yao leo kwa sababu wanaosimamia mifumo ya taarifa hawayasemi.

Viongozi kama Mugabe tunawahusisha sana na ubaya kwa sababu tunajazwa ubaya huo kila kukicha na baada ya muda tunasahau mazuri waliyofanya. Hutaambiwa kuwa moja ya sababu ya kuzorota kwa uchumi wa Zimbabwe ni vikwazo vya uchumi vilivyowekwa dhidi yake.

Lakini tukikubali kuwa viongozi hawana sura moja tu ni rahisi kuzungumzia mazuri ya Robert Mugabe. Rais Ali Hassan Mwinyi ametukumbusha kuwa wakati Tanzania ilipoandamwa na hali mbaya ya kiuchumi katika miaka ya 1980 ni serikali ya Rais Robert Mugabe iliyotoa msaada kwa Tanzania.

Rais Mugabe alikuwa kiongozi muhimu wa mapambano yaliyoleta uhuru nchini Zimbabwe. Chini ya uongozi wake, Zimbabwe ilikuwa kiungo muhimu ikiwa mwanachama wa Nchi za Mstari wa Mbele na baadaye wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) zilizounganisha nguvu za kidiplomasia na kijeshi kupinga utawala wa kibaguzi nchini Namibia na Afrika Kusini.

Alikuwa muumini mkubwa wa kuimarisha nafasi ya Bara la Afrika na watu wake kunufaika na rasilimali ya bara hilo na kukata mirija ya ukoloni na ukoloni mamboleo ndani ya mfumo wa uchumi ulimwenguni.

Tukumbuke kuwa katika mapambano hayo hayo kuna nchi kama Malawi, chini ya uongozi wa Dk. Hastings Kamuzu Banda, ambazo zilishirikiana na utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini na kudhoofisha jitihada za kuleta haki na usawa kwa raia wote wa Afrika Kusini.

Julius Malema, mwanasiasa machachari wa Afrika Kusini, ameweka msimamo mzuri juu ya historia ya Robert Mugabe. Amesema kila mtu amkumbuke Mugabe anavyotaka, lakini si sawa kumlazimisha mtu kukubali na kusisitiza sura moja tu ya historia yake.

Huo ni msimamo wa kuunga mkono. Rais Mugabe akumbukwe kama kiongozi muhimu wa ukombozi wa Zimbabwe na dhidi ya utawala wa wachache nchini Namibia na Afrika Kusini.

Maoni: [email protected]

By Jamhuri