Vitendo vya ulawiti kwa watoto wadogo, ubakaji na mimba katika umri mdogo vimeongezeka sana katika Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, JAMHURI limethibitishiwa.





Wafanyakazi wa Shirika la Kivulini wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watoto wanaolelewa katika kituo hicho wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike.

Takriban matukio 35 ya visa hivyo yameripotiwa kutokea ndani ya siku 60, kuanzia Januari Mosi hadi Februari 25, mwaka huu. Miongoni mwa matukio hayo, ni kuingiliwa kinyume cha maumbile kwa watoto wawili wadogo, akiwemo mwenye umri wa miaka mitatu.

Mamlaka za kiuchunguzi wilayani hapa zinasema chanzo cha matukio hayo ni kuporomoka kwa maaadili katika jamii na wazazi kutotimiza majukumu yao ya malezi ipasavyo. Kwa ujumla jamii inapaswa kutoa msaada mkubwa kwa kuripoti mikasa hiyo katika vyombo vya dola ili hatua madhubuti zichukuliwe dhidi ya ahusika.

Uchunguzi unasema kuwa kati ya matukio hayo 35, ni tukio moja tu ambalo kesi yake imeshatolewa uamuzi katika mahakama, huku hukumu ya kesi ya ulawiti wa mtoto mwenye umri wa miaka mitatu ikitarajiwa kutolewa siku yoyote.

Mkuu wa Dawati la Jinsia katika Jeshi la Polisi Wilaya ya Misungwi, Anna Sarimo, amethibitisha kuwapo kwa matukio hayo, akisema kwamba kati ya matukio 35 yaliyoripotiwa tayari kesi nane zimekwisha kufikishwa mahakamani na zipo katika hatua mbalimbali.

“Lengo hapa ni kuhakikisha kuwa sheria inachukua mkondo wake dhidi ya wanaotuhumiwa kufanya vitendo hivi,” anaeleza.

Kwa mujibu wa Sarimo, kesi saba bado zinaendelea kusikilizwa mahakamani, huku polisi wakiendelea na upelelezi wa matukio mengine 23. 

“Uplelezi ukikamilika wale wote ambao wataonekana kuhusika na matukio haya watafikishwa mahakamani,” anasisitiza na kubainisha kuwa watakaopatikana na hatia mahakamani watakabiliwa na kifungo cha miaka 30 gerezani.

“Tayari mtuhumiwa mmoja ameshahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela. Hebu fikiria wewe, mtu mzima anamlawiti mtoto wa miaka mitatu, unyama gani huu?” anahoji Mkuu huyo wa Dawati la Jinsia, Polisi wilayani Misungwi na kuongeza:

“Kuna mtoto mwingine mmoja naye amelawitiwa. Mbaya zaidi matukio haya mabaya unakuta mzazi anaogopa kwenda mahakamani kutoa ushahidi.

“Msiogope… mnaogopa nini wakati wanaoathirika ni watoto wenu?”

Mbali na vitendo vya ulawiti, ubakaji na mimba katika umri mdogo nalo ni tatizo kubwa. Mimba katika umri mdogo ni moja ya tatizo linalosabaisha wasichana wengi wadogo kukatisha masomo yao.

Katika kikao kazi cha kupanga mikakati ya utekelezaji wa kampeni ya kukabiliana na matatizo hayo, ilielezwa kuwa kesi nyingi zinakwama mahakamani kwa kukosa ushahidi thabiti.

“Tunawaomba sana watu wajitokeze kutoa ushahidi mahakamani. Hatuwezi kuwatia watu hatiani iwapo hakutakuwa na ushahidi mzuri,” Sarimo anatoa wito.

Ripoti ya Polisi Wilaya ya Misungwi inasema mwaka 2019, yaliripotiwa matukio 123 ya ukatili wa aina hiyo na kesi 67 zilifikishwa mahakamani, huku watuhumiwa 34 wakihukumiwa kulipa faini.

Katika kesi 25 watuhumiwa walikutwa na hatia na kesi nane zinaendela kusikilizwa. Polisi wanaendelea na upelelezi wa matukio 30,” anasema Mkuu huyo wa Dawati la Jinsia.

Ofisa mwingine wa Polisi wilayani Misungwi aliyefahamika kwa jina moja la Edger, wakati akiwasilisha mpango kazi katika kikao hicho, anasema mtu aliyebakwa anapaswa aripoti tukio hilo si zaidi ya saa 72 (siku 3) baada ya tukio.

“Ukichelewa ni vigumu sana kupata ushahidi wa kutosha, kwani hata daktari akipima hawezi kuona ushahidi wa kubakwa moja kwa moja,” anasema Edger.

Mkakati

Kutokana na matukio hayo ya ukatili, Shirika la Kivulini, linalojihusisha na kupiga vita ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana, likishirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, wameasisi kampeni maalumu ya ujenzi wa nyumba bora.

Kampeni hiyo inatajwa kulenga udhibiti wa vitendo hivyo, kuchochea maendeleo na kupunguza gharama za matibabu. Imeanzia kata za Koromije, Mondo, Mwanigo na Isenengeja.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Kivulini, Yassin Ali, anasema mpango huo si tu unachochea maendeleo, bali unaondoa ukatili na mserereko wa mawazo.

“Hali hii itaondoa hata masimango na unyanyapaa kwa wanafunzi wanaotoka familia zenye nyumba za miti na nyasi. Itaongeza pia mahudhurio darasani na kuongeza ufaulu,” anasema Yassin.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Kivulini, tafiti zinaonyesha kuwa hadi sasa nyumba bora 45 zimeshajengwa kupitia vikundi vijulikanavyo kwa jina la Kisukuma ‘Waponyamaswa’, yaani watupa nyasi.

Amesema rasilimali za mazao na nyinginezo wanazopata raia wa wilaya hiyo, lazima zitumike kuleta maendeleo, kwani hali hiyo itapunguza pia utoro shuleni.

“Tunataka mwaka huu 2020 tupunguze ukatili wa kijinsia kwa asilimia 50 na asilimia 27 ya mimba,” anaeleza huku akitoa wito kwa jamii kujitokeza mahakamani kutoa ushahidi katika kesi dhidi ya wanaotuhumiwa kufanya vitendo hivyo.

Miaka miwili iliyopita kuliripotiwa kuwapo magenge ya makahaba katika Wilaya ya Misungwi, ambapo iliarifiwa wanaume wengi walikuwa wakihonga magunia ya mahindi na mpunga, ili kufanya ngono na wanawake hao.

Taarifa zinabainisha kuwa makahaba hao waliweka masharti ya mwanamume anapotaka kupapasa mapaja au kunyonya matiti lazima atoe debe la nafaka, na waliotaka kushiriki ngono walilipa kuanzia gunia moja.

“Hawa wanawake waliokuwa wanauza miili yao walikuwa wakiitwa ‘nzige.’ Walisababisha mdororo wa chakula na kulegalega kwa baadhi ya ndoa.

“Wanaume wengi walitelekeza familia zao, baada ya kusombwa na upepo huo wa kisulisuli,” anasema Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Kivulini.

Maeneo yaliyotajwa kuathiriwa zaidi na magenge hayo ya makahaba ni Mbarika, Nhunduru, Kidarajani na Misasi. Baadhi ya wanafunzi walipachikwa ujauzito katika wimbi la matukio hayo.

Kulingana na kampeni ya wiki sita iliyoendeshwa na Shirika la Kivulini, likishirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, hali hiyo ilikoma baada ya wanawake hao kuanza kukamatwa na kuswekwa ndani.

“Kwa sasa kuna maendeleo hadi ufaulu wa wanafunzi umekuwa bora. Familia zimejenga nyumba bora. Tumepunguza ukatili wa kisaikolojia, kiuchumi, kingono na vipigo,” anaeleza Yassin.

Hakimu

Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Fela, Wilaya ya Misungwi, Isaac Mbolile, anasema ili kukomesha matukio ya ukatili na mengine yanayovunja sheria, lazima jamii ibadilike kifikra na kujitokeza kutoa ushahidi mahakamani katika kesi za aina hiyo.

Hakimu Mbolile anasema ushahidi imara ndiyo nguzo ya kesi yoyote mahakamani.

“Bila ushahidi usioacha shaka, mahakama haiwezi kufanya jambo lolote.

Ikimuachia huru hapo ndiyo utasikia amepewa sijui nini,” Mbolile anawaeleza wajumbe wa kikao kazi hicho cha kampeni ya nyumba bora.

Akitolea mfano, Hakimu Mbolile anasema aliwahi kupata kesi ya mama mmoja amepigwa na binti yake wa kumzaa, ambapo mama alimfikisha mwanaye mahakamani na kuamuru apewe adhabu.

Mbolile anasema kwa mujibu wa sheria, alimwamuru binti huyo kwenda gerezani, lakini kesho yake alifuatwa na mama wa binti huyo akitaka mwanaye atolewe gerezani.

“Sasa unaona jamii ilivyo. Ukimtoa utasikia aah! Hakimu kapewa kitu kidogo,” anaeleza Hakimu Mbolile.

Ofisa Elimu wilayani hapa, Dianah Kuboja, ameueleza umma kuwa asilimia 43 ya wanafunzi wanapotea (watoro), hivyo jitihada za pamoja zinahitajika kuboresha mazingira ya shule.

Anabainisha kuwa mwanafunzi kutopata chakula shuleni nao ni ukatili unaopaswa kuelekezewa nguvu, kwa kuhakikisha upatikanaji wa chakula, ili kuongeza ufaulu na mahudhurio darasani.

“Tunataka tuwe na ufaulu asilimia 90,” anasema.

By Jamhuri