MOROGORO

Na Everest Mnyele

Mfumo wa siasa wa demokrasia ya vyama vingi ni mfumo uliozoeleka kwa nchi za Magharibi hata kabla ya kuja kututawala.

Kwetu Waafrika, mfumo huu ulikuwapo tangu siku nyingi ukijulikana kama koo, makabila n.k. kwa kila moja kuwa na namna yake ya kujitawala.

Wakoloni walipokuja waliamua kutukusanya makundi makundi, hasa yale yaliyoshabihiana kimila na desturi na kutuweka pamoja na kutuita nchi, ambazo baadaye walizigawana huko Berlin, Ujerumani mwaka 1884.

Kimsingi, wakoloni walipokuja huku walikuja wakiamini katika mfumo wa vyama vingi, na makundi yaliyokuja huku yalikuja na nia tofauti.
Kama mjuavyo siasa ni suala la uwakilishi na masilahi, hivyo pamoja na kututawala, wakoloni hawa walikuwa wanawakilisha mataifa yao yaliyokuwa yamegawanyika kimasilahi.

Maana yake mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ulikuwapo kabla ya wakoloni, wakati wa ukoloni na baada ya uhuru.

Kwa Tanzania kama tujuavyo, mfumo huu ulifutwa mwaka 1965 ili kutekeleza falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea ambayo kwa namna moja au nyingine ilifeli mwishoni mwa miaka ya 1980 na kurejeshwa kwa demokrasia ya vyama vingi mwaka 1992.
Naomba tujiweke sawa na kuelewa kuwa kwa asili binadamu ameumbwa kuwa mbinafsi kunakomfanya kuwa na mawazo yake na nini anakiamini.

Lakini kutofautiana huko kunafikia wakati mtu mmoja au kikundi kuwashawishi wengine kuwa, pamoja na kujiaminisha kuwa imani yao ni bora kuliko ya wenzao, hivyo wana haki na wajibu wa kuwaongoza wengine.

Mfumo wa chama kimoja ulianzishwa Tanzania na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa sababu zake mwenyewe na kwa ushawishi wake aliweza kulazimisha Watanzania wote kuukubali akijua kabisa alichofanya si sawa kwa binadamu anayejitambua na mwenye fikra timilifu.

Mwalimu alijua si mfumo sahihi na alijua analazimisha kwa sababu zake, na ndiyo maana mwaka 1992 aliishangaza dunia kwa kusema sasa ni wakati wa kuwa na mfumo wa vyama vingi.

Tukubali kwamba Baba wa Taifa alikuwa na upeo mkubwa wa uelewa kuwazidi Watanzania wa umri wake na alijua kabisa anachokifanya si sawa, lakini: “Ngoja nitumie nguvu ya dola nitengeneze katiba ya kusapoti mfumo na itakapofika wakati muafaka tutabadili.”

Hivyo katika mfumo wa chama kimoja nguvu ya dola inakwenda pamoja na nguvu ya kisiasa.

Kwa jinsi Baba wa Taifa alivyokuwa amewaaminisha (brainwash) Watanzania juu ya mfumo huo, Aprili 24, 1992 wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM walibaki midomo wazi alipowaeleza kuwa kutofautiana kimawazo na kisera si dhambi wala usaliti. Ilikuwa ngumu kumeza.

Mwalimu akawaambia wajumbe umuhimu wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi kwa maendeleo ya nchi, na hii ndiyo mada ya leo.
Kwa kawaida ushindani huchochea watu kufikiri zaidi, kuwa wabunifu zaidi ili kwenda na wakati na kushawishi watu kukubaliana na mawazo na ubunifu wako, kwa namna yoyote ushindani huchochea ubunifu na maendeleo kwa ujumla.
Hivyo katika siasa, demokrasia ya vyama vingi hutoa nafasi kwa makundi ya watu wenye itikadi na sera tofauti kushindana kushika dola kwa kuwapa wananchi matumaini ya utumishi bora.

Siku zote wananchi wanahitaji huduma bora kutoka kwa taasisi za umma. Pia wanahitaji uchumi imara na ustawi wa nchi na mtu mmoja mmoja.

Hivyo, vyama vya siasa vinapaswa kushindana kwa sera kuonyesha jinsi gani chama kimoja kinaweza kufanya vizuri zaidi.

Demokrasia ya vyama vingi inasaidia serikali iliyopo madarakani kusugua kichwa ili kuwafanya wananchi waifurahie, tofauti na hivyo wananchi huamua kuchagua sera na chama tofauti kwa matarajio ya maendeleo zaidi.

Kwa mfano, kunaweza kuwa chama kinaamini katika ujamaa na sera zake ni za kijamaa, kama kitatumia sera ya kijamaa kuwapa maendeleo ya kiuchumi na kisiasa wananch haitakuwa tabu kwa kuwa kikifanya vizuri kitaendelea kuchaguliwa.

Lakini kufanya vizuri kwa chama kilichopo madarakani hutegemea sana nguvu ya vyama vya upinzani kujaribu kukionyesha mianya iliyopo katika kuleta maendeleo.

Kuwapo kwa vyama vingi vyenye nguvu na ushawishi ni kitu kizuri sana na afya kwa maendeleo ya wananchi.

Tusidanganyane, tunachohitaji wananchi ni maendeleo, si vinginevyo.

Watanzania bado tupo nyuma sana. Hatuoni umuhimu wa vyama vingi. Kuna watu bado wanaamini kuwa vyama vingi ni vita. 

Tuikatae dhana hii potofu kwa kuwa demokrasia hii ina afya kwa taifa, ilimradi tu kuwepo katiba thabiti, taasisi imara na mifumo madhubuti inayowasaidia wanasiasa kutekeleza sera zao huku haki, amani na maendeleo vikitamalaki.

Itaendelea.

By Jamhuri