Na Bashir Yakub

Leo tunaangalia namna ya kufanya ili uweze kuchukua fedha zilizoachwa kwenye akaunti ya simu na ndugu yako aliyefariki dunia; jinsi ya kufahamu iwapo ameacha fedha kwenye simu au hakuacha, hasa kama haujui namba yake ya siri ya akaunti (nywila).

Kinachotakiwa ni kuwa na nyaraka zifuatazo halafu uende ofisi za mtandao husika wa simu. Nyaraka hizo ni:

1. Hati ya usimamizi wa mirathi. Kwa Wakristo ni fomu Na. 68 na kwa Waislamu ni Fomu Na. 4. Nyaraka hizi hupatikana mahakamani baada ya kukamilisha utaratibu wa mirathi.

2. Cheti cha kifo cha ndugu yako (death certificate) kinachopatikana katika ofisi za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

3. Kiapo cha msimamizi wa mirathi. Hiki hupatikana katika ofisi ya wakili yeyote.

4. Wosia kama upo, kama haupo si lazima.

5. Barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa.

6. Kitambulusho cha msimamizi wa mirathi. Kinaweza kuwa cha taifa (NIDA) au kitambulisho cha mpiga kura (NEC), leseni ya udereva, hati ya kusafiria (passport) nk.

7. Muhtasari wa kikao cha familia ambao hupatikana baada ya familia kukaa, kuuandaa na kufikia makubaliano.

8. Kitambulisho cha mtu aliyefariki dunia. Kinaweza kuwa cha NIDA, cha mpiga kura au leseni.

Kimsingi, kitu kikubwa kinachohitajika katika kufuatilia mirathi iliyopo au inayoweza kuwapo kwenye akaunti ya simu ya ndugu aliyefariki dunia, nyaraka zilizopo katika kifungu cha kwanza hapo juu (namba moja), yaani hati ya usimamizi wa mirathi. 

Kampuni za simu zilizopo nchini, pamoja na hati hii, huhitaji pia na nyaraka hizo nyingine; yaani zilizopo kuanzia kifungu namba 2 hadi namba 7. 

Hata hivyo, hili lisikupe tabu, ukishafanikiwa kuwa na hati ya usimamizi wa mirathi, hivyo vingine lazima uwe navyo tu  kwa sababu ili mahakama ikupatie hati hiyo lazima uwe umewasilisha hivyo vielelezo vingine.

Kwa hiyo, ukishapeleka mahitaji hayo kwenye ofisi za mtandao husika, utapewa namba ya siri ya akaunti ya simu ya ndugu yako aliyefariki dunia, hivyo kufanya miamala au kuangalia kama kuna akiba.

By Jamhuri