(d) Uongozi Bora
TANU inatambua umuhimu wa kuwa na Uongozi Bora. Tatizo
lililopo ni ukosefu wa mipango maalum ya kuwafundisha
Viongozi, na kwa hiyo Ofisi Kuu ya TANU ni budi itengeneze
utaratibu maalum kuhusu mafundisho ya Viongozi tangu wa
Taifa zima hadi Mabalozi ili wailelewe siasa yetu na mipango ya
uchumi. Viongozi ni lazima wawe mfano mzuri kwa wananchi
kwa maisha yao na vitendo vyao pia.
SEHEMU YA NNE
UANACHAMA
Tangu Chama kilipoanzishwa, tumethamini sana kuwa na
wanachama wengi iwezekanavyo. Hii ilifaa wakati wa kupigania
vita ya kumgng’oa mkoloni . Hivyo ndivyo ilivyoibidi TANU
kufanya kwa wakati huo.
Lakini sasa Halmashauri Kuu inaona kuwa wakati umefika wa
kutilia mkazo kwenye imani ya Chama Chetu na siasa yake ya
Ujamaa.
Kifungu cha Katiba ya TANU kinachohusu uingizaji wa mtu
kwenye Chama kifuatwe na ikiwa inaonekana kuwa mtu
haelekei kuwa anakubali imani, madhumuni na sheria na amri
za Chama, basi asikubaliwe kuingia. Na hasa asisahauliwe
kuwa TANU ni Chama cha wakulima na wafanya kazi.
SEHEMU YA TANO
AZIMIO LA ARUSHA
Kwa hiyo basi, Halamashauri Kuu ya Taifa iliyokutana katika
Community Centre ya Arusha kuanzia tarehe 26/1/67, inaazimia
ifuatavyo:
A. Viongozi
1. Kiongozi wa TANU au wa Serikali sharti awe mkulima au
mfanya kazi, na asishiriki katika jambo lo lote la kibepari au
kikabaila.
2. Asiwe na hisa katika makampuni yo yote.

3. Asiwe mkurugenzi katika kampuni ya kikabaila au kibepari.
4. Asiwena mishahara miwili au zaidi.
5. Asiwe na nyumba ya kupangisha.
6. Viongozi tunaofikiria hapa ni wajumbe wa Halmashauri Kuu
ya Taifa, Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa Vyama
vilivyoshirikiwa na TANU, Wakuu wa Mashirika ya
Kiserikali, Viongozi kutokana na kifungu cho chote cha
Katiba ya TANU, Madiwani, na Watumishi wa Serikali
wenye vyeo vya kati na vya juu. (Kwa mujibu wa kifungu
hiki kiongozi ni mtu ay mtu na mkewe au mke na
mumewe.)

B. Serikali na Vyombo Vingine
1. Inaipongeza Serikali kwa hatua zote ilizokwisha chukua
mpaka hivi sasa katika kutimiza siasa ya Ujamaa.
2. Inahimiza Serikali, bila kungojea Tume ya Ujamaa, ichukue
hatua zaidi za kutimiza siasa yetu ya Ujamaa kama
ilivyoelezwa katika Tamko la TANU juu ya Ujamaa.
3. Inahimiza Serikali kutengeneza mipango yake kwa
kutegemea uwezo wa nchi hii kuiendesha mipango hiyo na
wala isitegemee mno mikopo na misaada ya nchi za
ng’ambo kama ilivyofanya katika mpango wa maendeleo
ya miaka mitano.
Halmashauri Kuu ya Taifa inaazimia mpango huo
urekebishwe ili ulingane na siasa ya kujitegemea.
4. Serikali ione kuwa mapato ya wafanya kazi nje ya Serikali
hayapitani mno na yale ya wafanya kazi Serikalini.
5. Serikali itilie mkazo sana njia za kuinua maisha ya
mkulima.
6. Inahimiza NUTA, vyama vya ushirika, TAPA, UWT, TYL,
mashirika yote ya Serikali, kuchukua hatua ili kutekeleza
siasa ya ujamaa na kujitegemea.

C. Uanachama
Wanachama wafundishwe kwa ukamilifu imani ya TANU ili

waielewe, na wakumbushwe wakati wote umuhimu wa
kuishika imani hiyo.

Ujamaa si Ubaguzi
Ilitolewa katika gazeti la Nationalist Februari 14, 1967
Azimio la Arusha, pamoja na vitendo vya juma lililopita vya
kuyafanya makampuni kadha kuwa mali ya Serikali, shabaha
yake ni kuhakikisha kwamba tunaweza kujenga Ujamaa katika
nchi yetu.
Kuyachukua makampuni hayo, ama yote kabisa ama sehemu
yake kubwa, ni kitu cha lazima katika azima yetu ya kubadili
maisha ya watu wetu, ili juhudi zetu ziwafaidie watu wetu wote,
bila ya mtu mmoja kumnyonya mwenzake.
Lakini vitendo hivyo peke yake haviundi Ujamaa. Ni mambo ya
maana kweli, lakini kama Azimio la Arusha linavyosema,
vitendo hivyo vinaweza vikawa ndiyo mwanzo wa utawala wa
nguvu, au uonevu wa kibepari.

Maana maneno ya mwanzo ya kijitabu change Ujamaa
nilichoandika mwaka 1962 yanasema ‘Ujamaa ni moyo’, na
maneno haya yana maana ile ile hata hii leo. Msingi wa Ujamaa
ni kuamini umoja wa binadamu, na kwamba katika historia ya
binadamu watu huinuka pamoja, na huanguka pamoja. Ndiyo
kusema kwamba msingi wa Ujamaa ni usawa wa binadamu.
Kukubaliwa kwa msingi huu ni jambo la maana kabisa kwa
Ujamaa. HAja ya kuwa na Ujamaa inakuwako kwa sababu ya
Binadamu; si kwa sababu ya nchi, wala bendera. Ujamaa
haujengwi kwa faida ya watu weusi, au watu weupe, rangi ya
kahawia, au manjano.
Shabaha ya kujenga Ujamaa ni kuwafaidia Binadamu bila ya
kujali rangi yao, kimo chao, umbo lao, ufundi wao, uwezo wao,
ama kitu kingine cho chote. Na vyombo vya uchumi vya

Ujamaa, kama vile tunavyoviunda sana kutokana na Azimio la
Arusha, shabaha yake ni kumsaidia ninadamu aliyeko miongoni
mwetu.
Mahali ambapo watu walio wengi ni weusi, basi wengi
watakaofaidika kutokana na Ujamaa watakuwa weusi. Lakini
kufaidika huko hakutokani na weusi wao; kunatokana tu na
ubinadamu wao.
Miaka michache iliyopita nilisema kuwa utawala wa nguvu na
ubaguzi vinaweza kuendeshwa pamoja, lakini ubaguzi na
Ujamaa havipatani hata kidogo. Sababu yake ni rahisi kuelewa.
Utawala wa nguvu ndiyo ukatili wa mwisho wa mtu kumnyonya
mtu mwingine; unaendeshwa kwa kugawa binadamu makusudi,
ili kundi moja la watu ligombane na kundi jingine.
Enzi za Nazi huko Ujerumani, walio wengi walishawishiwa
kuwafanyia Wayahudi vitendo vya kikatili. Wayahudi walikuwa
kikundi kidogo cha watu wa dini na asili moja, walioishi
miongoni mwa Wajarumani. ‘Ninawachukia waliounga mkono
Serikali ya Kinazi.
Lakini mtu anayewachukia ‘Wayahudi’, au ‘Wahindi’, au
‘Wazungu’; au hata ‘Wazungu wa Magharibi na Marekani’, si
mtu wa Ujamaa. Anajaribu kuwagawa binadamu katika vikundi,
na anawalinganisha watu kufuatana na rangi ya ngozi yao au
umbo walilopewa na Mwenyezi Mungu. Au anawagawa watu
kwa kufuata mipaka ya mataifa yao. Kwa vyo vyote vile,
anauharibu udugu na usawa wa binadamu.
Bila ya kukubali usawa wa binadamu hakuwezi kuwako
Ujamaa. Hii ni kweli hata kama uataratibu wenyewe ni wa
kijamaa namna gani. Hivyo ndivyo ilivyokuwa wakati Jarumani
ya Kinazi ilipojiundia viwanda vya kampuni ya Krupp.
Wapendao Ujamaa hawangeweza kufurahi, kwa sababu maana
ya hatua hiyo ilikuwa kuimarisha zaidi kuliko zamaini ule
utawala wa nguvu katika Ujarumani. Wala wapendao Ujamaa
hawawezi kufurahi wakisikia kuwa Afrika ya Kusini imeunda
Kampuni ya kusafirisha na kuuza mafuta, ambamo nchi ina
sehemu kubwa ya hisa.

Tunafahamu kuwa hatua hiyo inaufanya utawala ule uwe na
nguvu zaidi za kudhulumu, na uweze kujikinga ukishambuliwa.
Sisi Watanzania hatuna budi kuyakwepa mambo haya, hasa
wakati huu ambapo tunapiga hatua kuelekea katika lengo la
Ujamaa. Maana ni kweli kwamba, kwa sababu ya historia ya
kutawaliwa kwetu, idadi kubwa ya makampuni katika nchi hii
imekuwa mali ya Wahindi au Wazungu, na wao wenyewe ndio
waliokuwa wakiyaendesha makampuni hayo.
Miaka ishirini iliyopita tungweza kusema kuwa mabepari wote
wan chi hii wanatoka sehemu hizo; sasa hatuwezi tena kusema
hivyo. Maana kweli ni kwamba ubepari, na tabia za kibepari,
hazina uhusiano hata kidogo na taifa la mtu au nchi anayotoka
yule anayeamini ubepari na kuishi kibepari.
Na kwa kweli, ye yote atakayekuwako Arusha wakati wa
kuunda Azimio hana haja ya kuthibitishiwa kwamba vishawishi
vya ubepari havijui mpaka, maana hata viongozi wa TANU
walikuwa wamejiingiza kabisa katika maisha ya kibepari na
kikabaila. Wachache walikwisha anza kuzungumza habari za
‘Kampuni yangu’.
Na wengine wengi wangalifanya vivyo hivyo, kama
wandgalikuwa na uwezo; mioyo yao ilitamani sana ubepari,
ijapokuwa hawakuwa na uwezo wa kuwa mabepari. Ndiyo
sababu tukaweka Azimio la masharti ya uongozi; na ndiyo
sababu lazima tutazamie magumu mengi katika kutimiza Azimio
hilo.

<<<<<Itaendelea>>>>

Please follow and like us:
Pin Share