*Ni pambano la ‘Daudi na Goliati’ uwanjani

*Urusi ina kila kitu, makombora mazito, ndege

*Marekani, Uingereza zaitosa Ukraine kijeshi

*Putin aandaa matumizi ya zana za nyuklia

Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

Hali inazidi kuwa tete nchini Ukraine na wananchi wanazidi kuikimbia nchi yao kutokana na vita kati ya majeshi ya Urusi na Serikali ya Ukraine kuzidi kupamba moto.

Pamoja na majeshi ya Urusi kuyataka majeshi ya Ukraine kuweka silaha chini na kujisalimisha, Serikali ya Ukraine imezidi kusisitiza kuwa itaendelea kupambana katika vita hiyo.

Mataifa mengi ya Magharibi yanalaani kitendo hicho huku yakitangaza kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Urusi. Yanaamini vikwazo hivi ikiwamo kushikilia mali na kuzuia viongozi wengi kusafiri nje ya nchi vitaumiza uchumi wa Urusi, hivyo kuimaliza nguvu nchi hiyo yenye nyuklia.

China, Kenya na India pekee ndizo nchi hadi sasa zilizoonyesha bayana msimamo wao wa kuitetea Urusi kwa kukataa kuidhinisha azimio la kupinga vita ya Urusi dhidi ya Ukraine kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Ukraine ambayo ilijimega kutoka mikononi mwa Shirikisho la Umoja wa nchi za Kisovieti (USSR) mwaka 1991, ambako sasa imebaki Urusi, imejikuta kwenye kipindi kigumu tangu Februari 24, mwaka huu baada ya kujikuta ikipigana vita na Urusi bila msaada wa mataifa yaliyokuwa yanaipa hamasa.

Tangu kuanza kwa vita hiyo vifo vya raia, majeruhi wa kivita na wakimbizi wanaoikimbia nchi yao vinazidi kuripotiwa kila siku.

Majeshi ya Urusi yaliyojizatiti kwa silaha kali yanasonga kwa kasi kuelekea mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, na kuna kila dalili kuwa si muda mrefu watauangusha utawala uliopo wa Rais Volodymyr Zelensky ambaye Urusi haitaki awepo madarakani.

Hatua ya majeshi hayo kusonga Kyiv, imemlazimu Zelensky kuyaomba mataifa ya Magharibi na washirika wake kumsaidia kupambana na Urusi.

Kwanini anaomba msaada?

Wachambuzi wa masuala ya kijeshi wanasema vita ya Urusi na Ukraine ni sawa na kisa cha vita ya Goliati na Daudi katika Biblia.

Ufananisho huo unatokana na nguvu za kijeshi za mataifa hayo mawili yaliyomo kwenye mgogoro kutofautiana kwa kiwango kikubwa, kuanzia kwenye bajeti ya ulinzi, silaha walizo nazo na idadi ya vikosi vya nchi hizo.

Kwa upande wa bajeti za ulinzi za mataifa hayo, kwa mujibu wa ripoti ya masuala ya kijeshi kwa mwaka 2021 Ukraine ilitumia dola za Marekani bilioni 4.7 kwenye masuala ya ulinzi.

Kwa upande wake Urusi kwa mwaka huo yenyewe ilitumia bajeti kubwa mara 10 ya bajeti ya Ukraine, ambapo jumla ya dola za Marekani bilioni 45.8 zilitengwa kwa ajili ya maboresho ya jeshi na uundaji wa silaha za nyuklia.

Mbali na matumizi makubwa ya bajeti kwenye masuala ya ulinzi, tangu mwaka 2008 Urusi imeboresha silaha zake na kuzifanya kuwa za kisasa, ikilenga kuondokana na matumizi ya silaha za kizamani ambazo imekuwa ikizitumia tangu kipindi cha Muungano wa nchi za Kisovieti.

Ukraine yenyewe inategemea silaha hizo za zamani, na hiyo ndiyo sababu inayotajwa kwamba inachochea taifa hilo kutaka kujiunga na Muungano wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO) ili iweze kufanya mabadiliko ya kijeshi kwenye silaha, suala ambalo Urusi inapingana nalo kwa nguvu zote.

Vita hiyo inategemewa kuwa nzito kutokana na idadi kubwa ya wanajeshi wa Urusi ambao wanatajwa kuwa 900,000 walio tayari kuingia kwenye vita muda wowote na wanajeshi milioni mbili wa akiba, huku Ukraine yenyewe ikiwa na wapiganaji 196,000 na wanajeshi 900,000 wa akiba.

Upungufu huo wa wanajeshi unatajwa kuwa sababu ya msingi ambayo imemsukuma Rais wa Ukraine kuweka zuio la wanaume wote wenye umri wa miaka 18 hadi 60 kutoondoka nchini humo, badala yake wanatakiwa kushika silaha na wao kuungana na jeshi hilo kupigana vita.

Urusi ina askari wa nchi kavu 280,000, wakati Ukraine yenyewe ikiwa nao 125,600 huku kwa upande wa anga Urusi ikiwa na jumla ya wanajeshi 165,000 na Ukraine ikiwa nao 35,000 tu.

Vita inayoendelea nchini Ukraine inakadiriwa kuendeshwa na wanajeshi takriban 200,000 wa Urusi, ambapo ndani ya idadi hiyo kuna vikundi 60 vya wapiganaji waliogawanyika kulingana na vitengo vyao.

Kutokana na Urusi kuwa na kila kitu kwenye vita hiyo, kwa maana ya ndege za kivita, magari na makombora ya kisasa, inategemewa vita hiyo kuwa na madhara makubwa kwa Ukraine.

Kwa upande wa anga, Urusi inazo jumla ya ndege zenye uwezo wa kufanya mashambulizi makubwa 1,328  wakati Ukraine yenyewe ikiwa nazo 146.

Kwa upande wa helikopta za kivita, wakati Urusi ikiwa nazo 478 Ukraine yenyewe inazo 42 tu.

Pia Urusi inayo mitambo ya kubeba maroketi ya kivita 3,391 wakati Ukraine wenyewe wakiwa nayo 490.

Urusi wana vifaru vya kivita 13,360 wakati Ukraine wenyewe wakiwa navyo 2,870 tu.

Kwa upande wa majini, Ukraine hawako imara kutokana na kukosa meli za kivita zinazotembea chini ya maji (nyambizi), huku kwa upande wa Urusi wakiwa nazo 49.

Kwenye vita hii kuna tofauti kubwa ya vifaa vya kijeshi ilivyo navyo Urusi, huku Ukraine wao wakiwa hawana vifaa vya kisasa, hata vile walivyo navyo vikitajwa kutokuwa bora.

Hata hivyo, majeshi ya Ukraine pamoja na kudhibitiwa pande zote bado yanaonyesha uwezo wa ziada, kwa kuzidi kupambana kwa nguvu na kuulinda mji wa Kyiv, yalipo makao makuu ya mji na Ikulu ya Rais Zelensky.

Kwa upande mwingine jeshi hilo limezidiwa kwa mashambulizi ya anga, ambapo katika mashambulizi makubwa ambayo yamefanyika katika miji kadhaa ya taifa hilo yameharibu majengo na kuua watu takriban 210.

Mwitikio wa mataifa mengine

Hata baada ya Rais Zelensky kuomba msaada wa kila namna kutoka kwa mataifa ya Ulaya, hakuna hata taifa moja ambalo limepeleka majeshi yake moja kwa moja kupambana na majeshi ya Urusi nchini Ukraine.

Nchi za Umoja wa Ulaya, Uingereza na Marekani kwa pamoja zimekubaliana kutoa msaada wa kijeshi kwa kutuma silaha pamoja na huduma nyingine ambazo zinaweza kuisaidia Ukraine katika vita hiyo, lakini si majeshi.

Hatua ya mataifa hayo kutoingiza majeshi yao moja kwa moja inatafsiriwa kama kujilinda dhidi ya vita kubwa inayoweza kuzuka endapo yataingiza majeshi yao katika vita hiyo.

Wakati wa kuivamia Ukraine, Putin ameweka wazi kuwa taifa lolote litakalojaribu kuingilia vita hiyo atapambana nalo kwa nguvu zote na matokeo yake yatakuwa yale ambayo nchi hiyo haijawahi kuyashuhudia.

Kutokana na sababu hiyo, taifa la Marekani na washirika wake wamechagua kuiwekea viwazo Urusi, hasa vikimlenga Rais Putin pamoja na washirika wake, akiwamo Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergey Lavrov.

Hata hivyo kutoingia moja kwa moja kwa mataifa ya Ulaya na Marekani kunatajwa kama njia ya kuepuka Urusi kutumia silaha za nyuklia katika kujihami dhidi ya vita hiyo.

Hofu mataifa hasimu na Marekani kuingilia vita 

Upo uwezekano wa mataifa ya China, Syria, Iran na Korea ya Kaskazini kuingilia vita hiyo na kuipa nguvu Urusi, hali ambayo inatajwa kwamba inaweza kusababisha ‘Vita ya Tatu ya Dunia’.

Hofu hiyo inachochewa na ukweli kuwa mataifa hayo kwa kipindi kirefu yamekuwa kwenye mgogoro wa kimasilahi na mataifa ya Ulaya pamoja na Marekani.

Kuepusha hilo, viongozi wa NATO wamekubaliana kutuma jumla ya wanajeshi 40,000 kulinda mipaka ya nchi washirika zilizoko mashariki mwa Ulaya.

Katika hatua hiyo, Canada imetoa jumla ya askari 3,400 watakaoungana na majeshi ya NATO kuendesha operesheni hiyo.

Chanzo cha vita

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, aliwatangazia wananchi wake Februari 24, mwaka huu kwamba Urusi haiko salama kutokana na vitisho vya mara kwa mara kutoka Ukraine.

Alieleza kuwa lengo lake anataka kuwalinda watu wanaodhulumiwa na kukumbana na mauaji ya halaiki na unazi nchini Ukraine.

Pia aliweka wazi kuwa anapinga kitendo cha Ukraine kutaka kujiunga kwenye Umoja wa Ulaya na Muungano wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO), akidai kuwa hatua hiyo si salama kwa mipaka ya nchi yake.

Wakati akitangaza uvamizi huo, Putin aliweka wazi kuwa NATO inatishia mustakabali wa historia ya taifa hilo huku akiitaka Ukraine kuachana na mpango huo.

Baada ya tamko la Rais Putin, askari wa Urusi waliivamia Ukraine kupitia majimbo ya taifa hilo yaliyojitenga na kuungwa mkono na Urusi ambayo ni Luhansk na Donetsk.

Kwanini ni Ukraine?

Ukraine ni taifa la pili kwa ukubwa likipakana na nchi za Poland, Slovakia na Hungary kwa upande wa magharibi; Romania na Moldova kwa upande wa kusini, huku kwa upande wa mashariki ikipakana na Urusi.

Ukraine yenye ukubwa wa kilometa za mraba 603,628, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2021 ina wakazi milioni 43.6.

Uwepo wa rasilimali ambazo hazijawahi kuchimbwa tangu kuumbwa kwa dunia kunalifanya taifa hilo kuwa na umuhimu mkubwa duniani huku likitajwa kuwa taifa la pili kwa uzalishaji wa gesi baada ya Urusi.

Rasilimali hizo hasa mafuta, gesi na madini aina ya titanium na lithium vinatajwa kuiweka nchi hiyo kwenye njia panda huku ikishindwa kuchagua ni uelekeo upi inatakiwa kuungana nao kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi.

Wakati mataifa ya Magharibi yakiishawishi kujiunga upande wao kwa kuihakikishia ulinzi na masoko mazuri ya bidhaa zake, hatua hiyo inachukuliwa kama usaliti na ukiukwaji wa mikataba ambayo mataifa hayo yameingia na Umoja wa Kisovieti wa mataifa hayo kutojitanua.

Uwepo wa gesi yenye ujazo mkubwa ambayo haijachimbwa yenye uwezo wa kutumiwa na dunia nzima, inatajwa kuyavutia mataifa hayo ya Magharibi na kushawishika kuvunja makubaliano hayo.

Pamoja na taifa hilo kutajwa kuwa na kiwango kikubwa cha gesi kwenye ardhi yake, bado linaongoza kwa kuagiza gesi kutoka kwenye mataifa mengine, hasa kutoka Norway, huku gesi yake ikiendelea kutunzwa.

Hofu ya vita ya Ukraine na Urusi inaziweka kwenye mtego nchi za Ulaya, hasa Ujerumani ambayo kwa kiwango kikubwa inategemea usambazaji wa gesi kwa wananchi wake kutoka Urusi kupitia bomba la gesi la Nord Stream 1.

Hofu hiyo inatajwa kuipa wakati mgumu Ujerumani wakati wa kufikia uamuzi wa kutia saini uwekaji wa vikwazo kwa Urusi kutokana na kitendo chake cha kuivamia Ukraine.

Vikwazo ambavyo mataifa ya Magharibi yameiwekea Urusi vitaiathiri Kampuni yake ya Gazprom’s Nord Stream 11, ambayo kwa mwaka huliingizia taifa hilo kiasi cha dola za Marekani bilioni 7  kutokana na kusafirisha gesi kwenda Ulaya.

Madini ya titanium, chuma, makaa ya mawe na na lithium yanaipa wakati mgumu Ukraine kujinasua kwenye hali iliyo nayo kwa sasa, ambapo mataifa yote yanaivizia kunufaika na madini hayo, hasa lithium na titanium ambayo yanahitajika kwa sasa katika viwanda vya utengenezaji wa ndege  aina ya Boeing na magari yanayotumia betri za umeme.

Lithium na titanium ni madini yanayopatikana katika taifa hilo na yanahitajika kwa wingi duniani huku lithium yakiwa ni madini yanayopatikana kwenye Jimbo la Donbass, Ukraine, ambalo dunia nzima inalitazama kama mkombozi mkubwa wa baadaye wa soko la madini, hasa barani Ulaya.

Kwa upande wa madini ya kemikali za lithium, Ukraine inatazamwa kama chanzo kizuri cha bidhaa adimu katika magari yatakayotumia betri za umeme (EV).

Kampuni kubwa duniani zinazotengeneza magari ya ‘automatiki’ zinaitazama pia Ukraine kama chanzo kizuri cha kuzalisha lithium ambayo ni bidhaa muhimu na adimu.

By Jamhuri