Na Nizar K Visram

Vyombo vya habari vya kimataifa hivi karibuni vimetawaliwa na vita ya Ukraine. Mengi yanasemwa na mengine hayasemwi. Bila shaka wengi wetu watataka kujua nini kinachoendelea na chimbuko lake. Ndiyo maana ni muhimu kujua pia kile kisichosemwa na sababu za kutosemwa. 

Majeshi ya Urusi yameingia Ukraine na mapigano yanaendelea, wakati tunaambiwa mazungumzo yanaendelea baina ya nchi hizo. Urusi imesema hii ni operesheni ya kijeshi wakati wengine wakisema huu ni uvamizi.

Katika mkutano wa wanahabari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi,  Lavrov, aliulizwa na mwandishi wa BBC kwa nini Urusi inatumia neno ‘operesheni’ wakati huu ni uvamizi wa kijeshi. 

Lavrov akamjibu kuwa yeye amejifunza kutoka nchi za NATO ambazo zimekuwa zikitumia maneno kama ‘operesheni za haki za binadamu’ au za ‘kidemokrasia’ wakati wanavamia kijeshi nchi kama Afghanistan, Iraq, Syria na Libya. 

Labda Lavrov angeongeza kuwa NATO ilitumia maneno hayo pia waliposababisha kuvunjika kwa Yugoslavia, kujitenga kwa Kosovo kutoka Serbia na kujitenga kwa Sudan Kusini kutoka Sudan. 

Aidha, NATO ingefurahi sana kuona Taiwan na Hongkong zinajitenga kutoka China na Wakurd kujitenga kutoka Iraq na Syria.

Mjini New York, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) lenye wajumbe 15 limejaribu kupitisha azimio la kuilaani Urusi. Azimio likashindwa baada ya Urusi kutumia kura yake ya turufu (veto). Nchi tatu ziliamua kutopiga kura, nazo ni India, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na China.

Uvamizi umekuja baada ya maeneo mawili katika Jimbo la Donbas, Ukraine mashariki; Donetsk na Lugansk,  kutangaza kujitenga na kujiita ‘jamhuri’. Urusi ikazitambua ‘jamhuri’ hizi na ikaamua kuzisaidia kwa kutuma majeshi yake. 

Donbas imekuwa ikipigana kujitenga tangu mwaka 2014 wakati Serikali ya Ukraine ilipopinduliwa kwa msaada wa Marekani. 

Ni rahisi kumlaumu mvamizi lakini ni muhimu kuwatambua waliochochea uvamizi. Ndiyo maana ni vizuri angalau tukaanza miaka ya 1990 wakati Umoja wa Kisovieti (USSR) uliposambaratika. Ulimwengu ulitazamia huo ndio ungekuwa mwisho wa ‘vita baridi’ baina ya Marekani na USSR. 

Ni kwa sababu Rais wa Marekani wakati huo, George Bush (mkubwa) alimuahidi aliyekuwa Rais wa USSR, Mikhail Gorbachev, kuwa iwapo atavunja Jumuiya ya Warsaw (Warsaw Pact) na iwapo USSR itajitoa kutoka nchi za Ulaya Mashariki, basi NATO haitaziteka nchi hizo wala haitapanua mipaka zaidi ya Ujerumani. 

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, James Baker, naye akamhakikishia Gorbachev kuwa majeshi ya NATO hayatasonga mbele  ‘hata inchi moja’! Maneno haya matatu yaliyosemwa mwaka 1990 ni muhimu sana na ya kihistoria.

Ubalozi wa Marekani jijini Bonn (Ujerumani) ukarejea maneno hayo ya Baker. Katika kavazi (archive) la Chuo Kikuu cha George Washington kuna waraka unaofafanua ahadi hii ya Marekani kama ifuatavyo:

“Katika mkutano wake na Baker, Gorbachev alionyesha wasiwasi wake kuwa NATO huenda ikaikaribia USSR, naye Baker akamhakikishia mara tatu kuwa suala hilo halipo, kwani yeye na Rais wake Bush hawana nia hiyo. Akaongeza kuwa Marekani na Ulaya Magharibi zinaelewa umuhimu wa majeshi ya NATO kutovuka mpaka wa Ujerumani Mashariki hata inchi moja.” 

Siku iliyofuata, aliyekuwa Kansela wa Ujerumani Magharibi, Helmut Kohl, akarudia ahadi hiyo kwa Gorbachev. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Douglas Hurd, naye akasema nchi yake inajiunga na ahadi hiyo. 

Na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Margaret Thatcher, naye akarudia maneno hayo kwa kusema: “Ni muhimu sana kwetu kuihakikishia USSR kuwa usalama wake hautaathirika kwa kujitoa kutoka Ulaya Mashariki.”

Haikuchukua muda Gorbachev akagundua kuwa kumbe ‘ameuziwa mbuzi kwenye gunia’. Ahadi za kina Bush zilikuwa ahadi hewa. Kuanzia mwaka 1999 hadi 2004, NATO ikawa inavuka mipaka na kuingia Ulaya Mashariki. Ikachukua nchi za Jumuiya ya Warsaw na hata za muungano wa USSR mpakani mwa Urusi. 

NATO ikaingia Poland, Jamhuri ya Czech, Slovakia, Romania, Latvia na Lithuania. Majeshi na silaha za Marekani zimekuwa zikisogea karibu na mipaka ya Urusi. Mwaka 2008 ikawa zamu ya Ukraine na Georgia, ndipo Putin akaiambia Marekani: “Haiwezekani.”

Rais Putin akasema: “Haikubaliki kuona Marekani ikisimama na makombora yake nje ya mipaka yetu. Marekani ingejisikiaje kama makombora ya kigeni yangepangwa karibu na mipaka yake na Canada au Mexico?”

Pamoja na ahadi hewa za NATO ni muhimu pia tukaangalia Mkataba wa Minsk. Mwaka 2014 na 2015 Ufaransa na Ujerumani ziliingilia kati wakati mapigano yalipokuwa yakiendelea kati ya Serikali ya Ukraine na wananchi wa Donbas (majimbo ya Luhansk na Donetsk) waliokuwa wakipinga Ukraine kujiunga na NATO.

Maelewano yakafikiwa chini ya Mkataba wa Minsk uliosainiwa na Ukraine, Urusi, Ufaransa, Ujerumani na wapiganaji wa Donbas. Majeshi ya Ukraine yakarudi nyuma na wapiganaji wakaahidiwa serikali yao. Mkataba huu haukutekelezwa. Ndipo mapigano yakaendelea hadi tarehe Februari 21, mwaka huu Urusi ilipoamua kuzitambua jamhuri za Luhansk na Donetsk.

Mwaka 2014 Marekani ilichochea mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Yanukovych wa Ukraine aliyekataa kujiunga na NATO. Badala yake alitaka Ukraine iwe na uhusiano na pande zote mbili – Urusi na Umoja wa Ulaya (EU).

Maandamano yakaanza dhidi ya Yanukovych. Kutoka Marekani wakaja Seneta McCain na makamu waziri wa mambo ya nje, Victoria Nuland. Wakaonekana wakishiriki katika maandamano katika Uwanja wa Maidan (medani). Mtandao ukawaonyesha wakigawa mikate kwa waandamanaji katika uwanja huo ulio mji mkuu wa Kiev.

Mazungmzo ya siri yaliyorekodiwa baina ya Nuland na Balozi wa Marekani nchini Ukraine yakavuja. Walisikika wakijadili jinsi ya kumuangusha Yanukovych na kumtawaza kibaraka wa Marekani. Nuland akampendekeza Arseniy Yatsenyuk. Balozi akamwambia Nuland kuwa huenda EU wasimkubali Yatsenyuk na Nuland akajibu kwa kuitusi EU (akisema “f*ck the EU”). 

Wiki mbili baada ya mazungumzo hayo ya siri waandamanaji takriban 100 walipigwa risasi. Marekani mara moja wakamlaani Yanukovych kuwa ni muuaji. Lakini mazungumzo mengine ya siri yalivuja, mara hii baina ya mkuu wa mambo ya kigeni wa EU na waziri wa mambo ya nje wa Estonia. 

Wakasema yumkini ni wapinzani wa Yanukovych ndio waliotumia risasi ili kuchochea mapinduzi. Hawa ni wanachama wa vikundi vya mrengo wa kulia kama Azov na Right Sector wanaoungwa mkono na Marekani. Hatimaye wakafanikiwa kumuondoa Yanukovych Februari 2014. 

Ni vema tukajua kuwa Yanukovych alikuwa Rais aliyechaguliwa katika uchaguzi uliothibitishwa kuwa huru na wa haki na Shirika la nchi za Ulaya OSCE (Organization for Security and Cooperation in Europe).

Katika makubaliano ya Minsk watu wa Donbas walitakiwa wawe na serikali yao ya jimbo. Hii haikufanyika. Ndipo baada ya mapinduzi ya Maidan mwaka 2014 serikali ikaanza kuwahesabu wananchi wa Donbas kama wageni. Siyo tu wakanyimwa haki za kiraia bali wakaonekana kama magaidi wanaotaka kujitenga na kujiunga na Urusi. 

Baraza la Haki za Binadamu la UN lilisema kuwa “wananchi wa Ukraine wamekuwa wakinyimwa haki zao za kimsingi tangu mwaka 2014.”

Kabla ya 2014 Marekani ilikuwa ikimwaga misaada nchini Ukraine ili kuchochea mapinduzi. Hii ilikuja kupitia shirika lao la USAID pamoja na National Endowment for Democracy (NED).

Desemba 2013, Nuland aliyekuwa naibu waziri wa mambo ya Ulaya alitamka kuwa tangu 1991 serikali yake ilikuwa tayari imemwaga dola bilioni tano kusaidia harakati za ‘kidemokrasia’ nchini Ukraine. Fedha hizi ziligawiwa kwa maofisa wa Serikali ya Ukraine, wafanyabiashara, pamoja na wakuu wa vyama vya upinzani waliokubaliana na “malengo ya Marekani”.   

NED imetumia dola milioni 22.4 nchini Ukraine tangu mwaka 2014 wakati rais aliyechaguliwa kihalali alipopinduliwa na nafasi yake ikachukuliwa na mtu aliyeteuliwa na Marekani. Kwa ujumla imetoa ruzuku 334 nchini humo.  

Mwanzilishi wa NED akasema shirika hilo linafanya kazi iliyokuwa ikifanywa na CIA miaka 25 iliyopita. Litakuwa kosa kwa vikundi vya wanaharakati duniani kupokea ruzuku moja kwa moja kutoka CIA, ndiyo maana kazi hiyo inafanywa na NED, akaongeza: 

“Kazi inayofanywa na NED nchini Ukraine imekuwa ikifanywa katika nchi nyingi duniani, zikiwamo Belarus, Cuba, Hong Kong, Nicaragua, Venezuela na kadhalika.”

Mwandishi David Ignatius wa Washington Post amesema NED inafanya kadamnasi kazi ambazo CIA imekuwa ikizifanya kisirisiri.

[email protected]

0693 555 373  

By Jamhuri