Ushirikishwaji wa Watanzania waleta mabadiliko makubwa sekta ya madini

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa mabadiliko ya Sheria ya Madini mwaka 2017 na kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini yamepelekea mabadiliko makubwa katika Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na ongezeko la ajira kwenye migodi ya madini hadi kufikia asilimia 96 na manunuzi ya ndani kufikia asilimia 92 hali iliyopelekea Sekta ya Madini kuendelea kukua na kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.

Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo tarehe Januari 13, 2023 jijini Dodoma kwenye mahojiano maalum na Idara ya Habari Maelezo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kipindi maalum chenye lengo la kuangalia mchango wa Sekta ya Madini katika kuwawezesha watanzania kiuchumi pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii.

Amesema kuwa kabla ya mabadiliko hayo, kampuni nyingi za madini zilikuwa zikiajiri raia wengi wa kigeni hata kwenye kazi ambazo ziliweza kufanywa na watanzania hali iliyopelekea Serikali kufanya mabadiliko katika Sheria ya Madini mwaka 2017 na kutengeneza kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini ili kutoa fursa kwa watanzania wengi kushiriki katika uchumi wa madini kupitia ajira, utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini kama vile vyakula, usambazaji wa vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji wa madini kwenye migodi ya madini.

Ameongeza kuwa, mabadiliko hayo pia yalipelekea ongezeko la manunuzi ya ndani hadi kufikia asilimia 92 tofauti na awali ambapo manunuzi ya ndani yalikuwa ni chini ya asilimia 50 huku bidhaa nyingi zilizokuwa zikiagizwa nje ya nchi pamoja na kwamba zilikuwa zinapatikana ndani ya nchi.

“Kwa sasa kampuni nyingi zinanunua bidhaa na huduma kutoka ndani ya nchi na kwa bidhaa ambazo hazipatikani nchini, kampuni huomba kibali kutoka Tume ya Madini kabla ya kuagiza bidhaa husika,” amesema Samamba.

Amesema kuwa kupitia usimamizi mzuri wa utekelezaji wa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini, watanzania wengi wameanza kushika nafasi za juu kwenye menejimenti katika migodi ya madini kutokana na kukidhi sifa zinazohitajika.

Katika hatua nyingine, ameongeza kuwa kutokana na elimu ambayo imekuwa ikitolewa na Tume ya Madini kwa wadau wa madini nchini kumekuwepo na mwamko mkubwa kwenye ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini ambapo hadi sasa takribani watu milioni sita wameajiriwa kwenye shughuli za madini.

Akielezea mafanikio kwenye uboreshaji wa huduma za jamii kupitia migodi ya madini, Mhandisi Samamba amesisitiza kuwa kutokana na umakini wa Tume ya Madini kwenye usimamizi wa uboreshaji wa huduma za jamii unaofanywa na kampuni za madini mabadiliko makubwa yamepatikana katika mikoa mingi ikiwa ni pamoja na maboresho ya miundombinu ya barabara, maji, ujenzi wa shule na vituo vya afya.

Ameongeza kuwa awali kampuni za madini zilikuwa zikibuni miradi bila kushirikisha wananchi lakini baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini sasa kampuni za madini zinashirikisha Serikali kupitia halmashauri na wananchi kwenye uainishaji wa miradi yanye manufaa kwa wananchi kabla ya utekelezaji wake.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Samamba amezitaka kampuni za uchimbaji wa madini kuendelea kuimarisha mahusiano na jamii inayozizunguka na wananchi kutoa ushirikiano kwa kampuni ili uwekezaji wao uwe na manufaa kwa upande zote mbili.

Aidha, Mhandisi Samamba ametumia fursa hiyo kuwaalika wawekezaji wengi kutoka ndani na nje ya nchi kujitokeza kwenye uwekezaji katika Sekta ya Madini na kusisitiza kuwa Serikali imeweka mazingira mazuri ya kuhakikisha wananufaika huku Serikali ikinufaika kupitia kodi mbalimbali.