Wiki iliyopita kama ilivyo ada yake, Mpita
Njia (MN) alikuwa miongoni mwa abiria
waliotumia usafiri wa mabasi yaendayo
haraka au maarufu kama ‘mwendo kasi.’
MN alitumia usafiri huo wa mwendo kasi
majira ya saa 12:30 jioni kutoka kituo cha jiji
hadi kituo cha Ubungo ilipo stendi ya
mabasi yaendayo mikoani.
Baada ya kutelemka katika kituo hicho
alipita katika njia maalumu zilizojengwa
(daraja) ili kuvuka upande mwingine wa
barabara kuendelea na safari zake.
Lakini kilichomshangaza MN ni mradi
mwingine haramu uliobuniwa na baadhi ya
vijana wa kumtoza ushuru wa Sh 300 kila

abiria aliyetumia usafiri wa mwendo kasi
anayetumia daraja hilo.
MN akasimamishwa na vijana hao ambao
hawatoi hata risiti za malipo na kutakiwa
alipe Sh 300 ili aruhusiwe kuendelea na
safari zake nje ya kituo cha mabasi cha
Ubungo.
Alipohoji uhalali wa malipo hayo akaelezwa
kuwa yanakwenda serikalini ili kuchangia
shughuli za maendeleo (kodi) lakini tatizo
lake ni kutowapa wananchi risiti za malipo.
MN akahoji kuhusu uhalali wa mapato hayo
kwamba yanakusanywa na nani? Kwa nini
hazitolewi risiti za malipo? Kwa nini abiria
aliyetozwa nauli ya Sh 650 mwendo kasi
atozwe tena Sh 300 kwa ajili ya kuvuka
katika daraja lililojengwa kwa ajili ya abiria
wanaotumia usafiri huo?
Cha kushangaza maofisa hao
wanaokusanya fedha hizo wakatoa majibu
mepesi kwamba fedha hizo ni kodi ya
serikali wanayoikusanya baada ya njia ya
kupitia abiria watumiao usafiri wa mwendo
kasi kufungwa.

“Kama unavyoona mkandarasi
anayeendelea na ujenzi wa barabara eneo
la Ubungo amechimba hapo walipokuwa
wanatokea watu na njia hiyo imefungwa
kwa muda,

” ameeleza mmoja wa

wakusanya mapato hayo kutoka stendi ya
Ubungo.
Wanadai makusanyo hayo wameanza
kukusanya mwanzoni mwa mwezi Julai
mwaka huu na watasitisha shughuli hiyo
mkandarasi atakapokuwa amekamilisha
kazi yake.
MN na baadhi ya abiria wa mwendo kasi
walikataa kutapeliwa na wahuni hao, hivyo
kulazimika kurudi tena upande mwingine wa
barabara kwa ajili ya kuvuka barabara hiyo.
Ni wazi kuwa huu ni wizi wa mchana
kweupe unaofanywa na kikundi hiki cha
wahuni waliojipa jukumu la kuisaidia TRA
kukusanya mapato hewa.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na
uongozi wa Manispaa ya Ubungo
chunguzeni uhuni huu unaofanywa na watu
wachache ambao ni hodari kubuni miradi ya

ovyo kama hii.
Ieleweke ni kiasi gani cha fedha
walichokusanya kutoka kwa abiria wa
mwendo kasi wanaotumia kivuko hicho, na
fedha hizo zinakwenda wapi?
Huku ni kuwaumiza wananchi wanyonge wa
nchi hii. Kwa nini wasijivunie kuwa ndani ya
nchi yao badala ya kuwafanya wajute?
Kama tatizo ni unyonge wao, basi wapeni
haki zao.
Utaratibu huu wa kuwatoza fedha abiria
wanaovuka daraja la mwendo kasi
haukubaliki kamwe, ni uonevu uliovuka
mipaka.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share