Ni kweli tuna matatizo mengi – kuanzia
ukosefu wa ajira, elimu duni, kilimo duni,
huduma duni za afya, miundombinu duni,
ukosefu wa maji safi na salama kwa watu
wetu, demokrasia changa, utawala dhaifu
na kumomonyoka kwa maadili kwa baadhi
ya viongozi.
Wakati mwingine Watanzania wanaonekana
kama watu ambao akili zao zimekusanywa
na kukabidhiwa kwa ‘mtunza akili’. Kama ni
kujipima, tumejipima sana. Kama ni kuona,
tumeona sana. Kama ni kutafakari,
tumetafakari sana. Kama ni kusikia,
tumesikia sana. Kama ni kuchekwa,
tumechekwa sana. Kama ni kuvumilia,
tumevumilia sana. Kama ni kupembua,
tumepembua sana. Kama ni ukimya, sasa
imetosha. Kama ni aibu tumeipata.
Jamii yoyote ni lazima itembee katika
ukweli, haki, maadili, mwanga na elimu.
Hakuna jamii inayoweza kuendelea pasipo
watu wake kuwa wakweli na wenye maadili
na akili tafakari na akili bainifu.
Kiongozi wa madhehebu ya Budha, Dalai

Lama, anasema: “Huwezi kufanya jambo
sahihi kama kichwani mwako umebeba
mtazamo hasi.”
Swali la changamoto, Watanzania tuna
mitazamo gani kwenye vichwa vyetu?
Katika historia yote ya kuyatafakari mawazo
ya mwanadamu na mifumo ya miundo yake,
wanafikra adhimu karibu wote duniani
wanakubaliana kuwa tendo la
kuelewa, hususan kufikiri, huwezekana tu
katika mfumo wa udhanishaji wa mawazo
jumla (universal concepts).
Waafrika na walimwengu kwa
ujumla wanastajabia mapinduzi makubwa
ya kiuchumi ya taifa la China na wanajenga
hoja kwamba tuwaige Wachina, lakini
wanashindwa kufahamu kuwa kile
tunachokiona kwa Wachina leo ni matokeo
ya akili na uwezo wao wa kuyafikiri mambo
kwa kina na kuyaumba kwa vitendo.
Hegel anasema: “Mifumo yote ya kiuchumi
na kijamii ni ujielezo wa ulimwengu wa akili
wa jamii husika.”
Naye Plato anasema: “Kile kionekanacho
katika matukio ni kivuli cha ulimwengu wa
fikra wa jamii husika.” Ninatamani kuiona
Tanzania yenye watu wenye fikra pevu.
Ninatamani kuiona Tanzania yenye watu

wanaothamini tafiti za kisomi. Natamani
kuwaona Watanzania watafiti na wabunifu.
Natamani kuiona Tanzania yenye watu
wanaojikubali na kujitambua. Siku moja
mwanafalsafa Socrates aliwasha taa
mchana (kweupe) na akaenda nayo kwenye
soko la Athens, Ugiriki ya sasa.
Pale sokoni wananchi wengi walimshangaa
mno Socrates wakamuuliza: “Kwa nini
wewe umewasha taa hapa sokoni wakati ni
mchana na mwanga wa taa yako wala
hauonekani kutokana na mwanga wa jua
uliopo?” Socrates aliwajibu hivi: “Pamoja na
nuru hii ya jua, lakini akili za watu wengi
ziko kwenye giza nene.” Ukweli huu
aliousema Socrates unawagusa watu
wanaoishi kwa sababu wanaishi.

.tamati….

Please follow and like us:
Pin Share