Na Alex Kazenga, JAMHURIMEDIA Dar es Salaam

Utafiti wa mbegu za maharage yaliyoboreshwa umeipa ushindi taasisi ya Kenya katika Tuzo ya Chakula Afrika (Africa Food Prize-2023) inayotolewa kila mwaka.


Mwenyekiti wa kamati ya AFP, Dk. Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza mbele ya vyombo vya habari katika ukumbi wa Mkomazi Hall uliopo jengo la Kituo cha mikutano Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, ameitangaza taasisi hiyo kuwa ni Pan- Africa Bean Research Alliance (PABRA).


Kutangazwa kwa tuzo hiyo ni sehemu ya matukio mengi yanayoendelea kati ya mikutano inayoendelea ya Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika (AGRF-2023.)


PABRA imekuwa mshindi kutoka maombi 496 yaliyowasilishwa kwenye kamati ya tuzo hiyo kutoka mataifa 47 barani Afrika na kujizolea dola za Marekani 100,000 sawa na Sh milioni 250.


“PABRA imetumia uwezo wa maharage katika kuboresha lishe na usalama wa chakula Afrika, baadhi ya watu wanajua maharage ni chakula cha watu wa hali ya chini lakini hawajui ni chanzo muhimu cha protini.
“Yana virutubisho muhimu yakiwamo madini ya zinki, kwenye damu madini haya yakipungua ndipo tunasikia mtu amepungukiwa na damu, maharage yana madini ya chuma pia” anasema Dk. Kikwete.


Aidha, anasema wataalamu wa kilimo ndani ya kamati hiyo ya tuzo imeichagua PABRA kutokana na kubaini juhudi zake za kuzalisha aina mpya za maharage na kuzifanya ziwafikie wakulima wengi barani Afrika.
Juhudi hizo anasema zimetoa matokeo chanya katika maisha ya wengi hasa jamii zinazokabiliwa na uhaba wa chakula na utapiamulo.


Ameitaja taasisi hiyo kufanya tafiti aina 650 za maharage zilizoboreshwa na yenye sifa tofauti tofauti ambazo hupandwa na wakulima wadogo takribani milioni 37 barani Afrika na kwamba aina hizo zinaliwa na watu zaidi ya milioni 300 barani Afrika.


Dk. Kikwete anaipongeza PABRA kwa mchango wake mkubwa wa kuwazwezesha familia nyingi kula vizuri huku akitaja kuwa imeimarisha kipato cha wanawake wengi ambao ndio wasimamizi wakubwa wa kilimo na biashara ya zao hilo


“Kazi ya PABRA inalingana kikamilifu na malengo ya tuzo hii, mchango wake ni mkubwa katika uzalishaji wa shamba,” anasema.
Moja ya kigezo kinachozingatiwa kupata mshindi Dk. Kikwete amekitaja kuwa watuma maombi kuonyesha mchango/program ya kupunguza umasikini na usalama wa chakula.


Tuzo hiyo inayotolewa kila mwaka kwa watu wanaonyesha juhudi za kubalisha kilimo barani Afrika thamani yake ni dola za Marekani 100,000.


Imeanzishwa mahusisi kuangazia mipango ya ujasiri na ubunifu inayopaswa kuigwa na bara zima katika kuhakikisha usalama wa chakula na fursa za kiuchumi kwa Waafrika wote.


Akizungumza mbele ya vyombo vya habari mshindi wa tuzo hiyo mara baada ya kutangazwa, Mkurugenzi wa PBRA na kiongozi wa program ya Global Bean, Jean Claude Rubyogo, anasema tuzo hiyo imekuja wakati muhimu na ni tuzo ya kihistoria katika muungano wa taasisi yao.


“Mwaka jana tulisherehekea kutimiza miaka 25 ya kufanya utafiti, maendeleo, kuzindua harakati za maharage na kukuza maharage kama chakula bora, imekuja wakati mwakafaka,” anasema Rubyago na kuongeza ushindi huo ni ushindi kwa wanawake kwa kuwa wao ndio wadau wao wakubwa.

By Jamhuri